24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TRA YAFANIKIWA KUKUSANYA MAPATO MAKUBWA ZAIDI  

Na KOKU DAVID


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) hivi karibuni ilizindua mradi wa pamoja wa TRA na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).

Mradi huo uliozinduliwa na Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere.

Katika uzinduzi wa mradi huo, wawakilishi watano kutoka JICA walishiriki ikiwa ni pamoja na baadhi ya watendaji wa juu wa mamlaka hiyo.

Kupitia mradi huo, TRA itakuwa ikiendesha mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wake ili kuwajengea uwezo, ikiwa ni pamoja na kukumbusha wajibu wa kufanya kazi kwa uadilifu pindi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kazi.

Mafunzo hayo yatakuwa yakifanyika katika Chuo cha Kodi (ITA) kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam na kwamba kupitia mradi huo, JICA itakuwa ikidhamini mafunzo hayo.

Sambamba na mradi huo, pia mamlaka hiyo kupitia Kamishna wake Mkuu pamoja na baadhi ya watendaji wa juu wa mamlaka, ilikutana na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne-Marie Kaarstad na kujadili masuala mbalimbali ya namna bora ya ukusanyaji wa mapato.

Katika mkutano huo, masuala mbalimbali ya kodi yalijadiliwa na kwamba lengo lilikuwa ni kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu za ukusanyaji mapato.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, anasema mamlaka hiyo imejiwekea utaratibu wa kukutana na wadau wa kodi kutoka nchi mbalimbali ili kubadilishana utaalamu na uzoefu katika suala zima la ukusanyaji wa mapato.

Anasema pia imedhamiria kuhakikisha inatimiza malengo yake katika suala la ukusanyaji wa mapato, hivyo kupitia wataalamu wa kodi kutoka nchi ambazo TRA imekuwa ikikutana nao wanaamini watafanikisha lengo.

Anasema kutokana na mikutano hiyo ya wataalamu kutoka nje ya nchi pamoja na elimu ya mara kwa mara wanayopewa watumishi wa mamlaka hiyo, TRA imekuwa ikifanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ambapo tangu kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Tano, ukusanyaji wa mapato haujashuka chini ya trilioni moja.

Anasema katika mradi wa kuwajengea uwezo watumishi wa mamlaka ya mapato, JICA imeahidi kutoa udhamini wa mafunzo kwa watumishi wa TRA yatakayowasaidia kuongeza utaalamu.

Kayombo anasema mamlaka hiyo ilishakutana na makamishna wa Upelelezi wa Kodi kutoka nchi za Afrika Mashariki, lengo likiwa ni kuendeleza ushirikiano katika mambo ya upelelezi wa kodi, kuzuia ukwepaji wa kodi, ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa za kipelelezi katika masuala ya kodi.

Anasema pia walijadili namna bora ya uboreshaji wa utendaji kazi hasa katika mbinu za uchunguzi pamoja na kupigana vita dhidi ya wakwepa kodi.

Anaongeza kuwa lengo kuu la TRA kukutana na wadau hao ni kutaka kuangalia namna bora itakayoiwezesha mamlaka kuweka juhudi zitakazofanikisha ushindi dhidi ya vita na wakwepa kodi, ikiwa ni pamoja na kuongeza mwamko kwa wananchi kulipa kodi kwa hiyari.

Anasema ili kuongeza uhiyari wa kulipa kodi kwa wananchi, TRA itaendelea kutoa elimu ya kodi kwa walipakodi kabla ya kuwachukulia hatua za kisheria kwa kosa la kukwepa kulipa kodi.

Anasema sambamba wa wananchi kutakiwa kulipa kodi, pia watumishi wa mamlaka wanatakiwa kuwa waadilifu kazini ikiwa ni pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa vinavyoweza kuichafua mamlaka.

Anasema TRA ya sasa inafanya kazi kwa kufuata maadili na kwamba uadilifu kazini ndio msimamo wa mamlaka na iwapo mtumishi atabainika kukiuka maadili, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles