23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

BoT, NBS YASISITIZA UMUHIMU WA TAKWIMU SAHIHI

Na Mwandishi Wetu


 

MKURUGENZI wa Uchumi BoT, Johnson Nyella, amesema uchumi wa Tanzania ulikua kwa wastani wa asilimia 6.7 mwaka 2016, wakati pato la taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 7, sawa na ilivyokuwa mwaka 2015 na 2014.

Nyella alisema hayo wakati wa sherehe ya Siku ya Takwimu Afrika (2017), iliyofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa BoT, kwa miaka minne mfululizo, mfumuko wa bei wa Taifa umeendelea kupungua na kubaki katika kiwango pendwa cha tarakimu moja.

“Mwaka 2016 mfumuko wa bei ulipungua na kufikia wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6 mwaka 2015 na asilimia 6.1 mwaka 2014,” alisema.

Kwa vigezo hivyo Mkurugenzi huyo wa Benki Kuu (BoT) amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye viwango vya juu vya ukuaji wa uchumi na kupendeza katika kipindi cha muongo mmoja uliopita (2007 – 2016).

Nyella alisema takwimu sahihi za uchumi zinahitajika katika kupanga mipango ya maendeleo na utungaji wa sera kwa ajili ya kuboresha maendeleo endelevu ya mwaka 2030.

Kwa mujibu wa Nyella, takwimu bora za kiuchumi zinasaidia kuongeza tija serikalini katika kupanga mipango yake ya maendeleo na kukabiliana na changamoto kadiri zinavyojitokeza.

Alisema takwimu bora pia zinawasaidia watunga sera na watekelezaji wa programu mbalimbali wakati wa  kupanga mikakati mipya ya kuboresha maisha ya wananchi.

Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa, alisema kwenye sherehe hizo takwimu bora za uchumi ni muhimu katika kufikia ajenda ya Bara la Afrika ya mwaka 2063 inayosisitiza ukuaji wa uchumi wa Bara hilo.

Katika kufikia ajenda hiyo, baadhi ya mambo yanayosisitizwa ni amani, utulivu, kuboresha uchumi wa Afrika, kukusanya mapato ya Afrika ili Afrika iweze kujitegemea.

Kwa mujibu wa Dk. Albina, ajenda ya Afrika ya mwaka 2063 haiwezi kufanikiwa bila takwimu bora za uchumi ili kujua mwendelezo kamili wa shughuli na matokeo yake.

Alisema Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi ya Afrika (UNECA) kwa kushirikiana na Ofisi za Takwimu za Afrika, ina kaulimbiu isemayo; “Takwimu Bora za Uchumi kwa Maisha Bora,” ikisisitiza umuhimu wa takwimu za kiuchumi katika kuleta maendeleo endelevu hivyo kuboresha maisha ya wananchi.

Dk. Albina alisema kaulimbiu hiyo inarandana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais, John Magufuli, kwa kuwa na dhamira ya kujenga uchumi wa viwanda. Alisema kwa sababu hiyo, takwimu rasmi za uchumi za Serikali lazima zitolewe kwa weledi na kwa kufuata kanuni na sheria.

“Takwimu bora za uchumi kwa nchi yetu ni za muhimu sana, hasa wakati huu ambao Serikali yetu inaimarisha uchumi wa viwanda ili Tanzania iweze kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 na kuboresha zaidi maisha ya wananchi wake.

Takwimu hizi za uchumi ni pamoja na takwimu za kilimo, viwanda, ujenzi, usafirishaji, nishati, biashara, mazingira, mfumuko wa bei na uwekezaji,” alisema Dk. Albina  na kuongeza kuwa; “ili takwimu zitumike kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi, zinatakiwa kuwa bora na za kuaminika.”

Alifafanua kwa kusema kuwa takwimu bora ni zile zilizo sahihi, zinazotolewa kwa wakati, linganifu na za kina, zinazozalishwa mara kwa mara na zenye ufanisi.

Dk. Albina alionya kuwa sifa hizo zote zinaendana na kanuni za msingi za takwimu rasmi za Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Takwimu wa Afrika, ambazo zinajali maisha ya wananchi na kutekeleza ajenda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles