24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

KOCHA WA MBWANA SAMATTA ATIMULIWA

NA MWANDISHI WETU


KLABU ya soka ya Koninklijke Racing Club Genk, imetangaza kumtimua kazi kocha wake, Mholanzi Albert Stuivenberg, kutokana na mwenendo mbaya wa kikosi hicho tangu kuanza kwa Ligi Kuu ya nchini Ubelgiji msimu huu.

KRC Genk ndiyo klabu anayochezea nahodha wa timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta.

Stuivenberg mwenye umri wa miaka 47, ameifundisha klabu hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja, huku akiiwezesha msimu uliopita kufanya vizuri kwenye Ligi ya Europa, ingawa msimu huu ameshindwa kufuzu.

Genk inaonekana kukosa nguvu msimu huu chini ya Mholanzi huyo, kwani mpaka sasa ipo katika nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji ikiambulia pointi 23 pekee baada ya kushuka dimbani mara 18.

“KRC Genk inamshukuru Albert Stuivenberg kwa weledi na kujitoa kwake, tunamtakia kila la heri huko aendako,” ilisema taarifa ya klabu hiyo.

Taarifa ya klabu hiyo iliongeza kuwa timu hiyo kwa sasa itakuwa chini ya Jos Daerden, akiisimamia katika mazoezi na mechi wakati uongozi wa klabu hiyo ukiwa katika mchakato wa kutafuta kocha mpya.

Stuivenberg aliyezaliwa Rotterdam, Uholanzi, aliwahi kuwa msaidizi wa Louis van Gaal katika klabu ya Manchester United kwa kipindi cha miaka miwili.

Huyu anakuwa kocha wa pili kutimuliwa tangu Samatta alipojiunga na timu hiyo akitokea klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), kocha mwingine ni Peter Maes ambaye alitimuliwa Desemba 26, mwaka jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles