23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

NYUMA YA PAZIA KIFO CHA TAJIRI WA MABASI

Na FREDRICK KATULANDA – MAGU


UCHUNGUZI wa mwili wa mfanyabiashara mmiliki wa mabasi ya Super Sami, Josiah Mzuri, umebainisha kuwa, aliuawa kwa kuchinjwa shingo, kukatwa miguu yote miwili na kufungwa kwenye viroba na kisha kutupwa ndani ya Mto Rubana, Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara.

Akizungumza jana na Mtanzania, msemaji wa familia, Yusufu Kijika, alisema mwili wa marehemu umekutwa na majeraha mengi ambayo yanaonyesha wahusika walimtesa, ikiwa ni pamoja na kumtoboa mbavu, kujaribu kumchinja shingo na kumkata miguu yote.

Alisema majeraha hayo yanaonyesha huenda marehemu aliuawa kabla ya kufungwa ndani ya viroba na kutupwa mtoni, kisha gari lake kuteketezwa kwa moto.

“Inavyoonesha ni kuwa marehemu aliuawa ndani ya gari lake au nje na mwili wake kubebwa na gari hilo, kwa hofu ya wauaji kubainika, waliamua kulichoma moto gari ndani ya hifadhi (ya Serengeti), inawezekana wamefanya hivyo kujaribu kuharibu uchunguzi,” alisema.

Naye kaka wa marehemu, Amini Mzuri Sambo, alikiri kukamilika kwa uchunguzi (postmortem), lakini hakutaka kuuzungumzia kiundani, kwa maelezo kuwa, anaweza kuharibu uchunguzi wa suala hilo.

Alisema yeye alikwenda kuwakilisha familia, hivyo hana mamlaka ya kueleza taarifa ya uchunguzi huo.

“Ni kweli nilishiriki uchunguzi, nao umebainisha hali halisi ya kifo cha ndugu yetu, lakini siwezi kuweka wazi hapa, maana haya ni mambo ya uchunguzi na kazi ya upelelezi inaendelea…, kwa kifupi aliuawa,” alisema Amini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Jafari Mohamed, alisema hawezi kuzungumza jambo lolote kuhusiana na uchunguzi wa mwili wa mfanyabiashara huyo, kwa kuwa bado Jeshi lake halijakabidhiwa taarifa na madaktari waliohusika na uchunguzi wa mwili wake.

“Uchunguzi uliofanyika ni muhimu kwetu, maana huu ni uthibitisho au kielelezo cha muhimu kuhusi kifo cha Josiah, ambao tutautumia kama ushahidi mahakamani.

“Sasa kuhusu kilichobainishwa hicho sijui kwa sasa, maana bado hatujapokea taarifa rasmi kutokana na waliohusika na uchunguzi, ila ninachojua bado wanaendelea kuandika taarifa ya uchunguzi wao,” alieleza.

Vifaa vya marehemu

Mpaka sasa haijabainika mahali ilipo bastola yake ambayo alikuwa akiimiliki na kwamba familia ilikuwa ikiendelea kuitafuta ili kubaina kama aliondoka nayo au la.

“Bastola yake bado tunaendelea kuitafuta, hatujui kama aliondoka nayo au aliiacha, hata polisi wanafuatilia hili, kuhusu simu naomba tuachane nayo, maana waliokamatwa walionekana kufanya mawasiliano naye mpaka dakika ya mwisho anatoweka,” alisema Kijika.

Mmoja akamatwa msibani Magu

Josiah alizikwa jana katika makaburi ya Magu Mjini, yaliyopo Mtaa wa Itumbili, wilayani Magu, mkoani Mwanza na kuhudhuriwa na watu mbalimbali, wakiwamo wafanyabiashara wakubwa.

Hata hivyo, wakati maziko yakiendelea makaburini hapo, mtu mmoja, mwanamume, ambaye hajatambulika jina lake, alikamatwa na polisi na kupandishwa katika gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser namba PT 1899.

Akizungumzia kukamatwa kwa mtu huyo, Kijika alisema Februari 28, mtu huyo alionekana nyumbani kwa Josiah, akiulizia iwapo yupo na alipoulizwa shida yake alitoweka mbio.

“Tukiwa makaburini alionekana, hivyo hatukuwa na namna nyingine zaidi ya kuwaonyesha polisi, ambao walimkamata kusaidia uchunguzi,” alieleza.

Mfanyabiashara huyo anadaiwa kutoweka Februari 27, mwaka huu, nyumbani kwake eneo la Mwananchi-Buzuruga, Kata ya Mahina, Wilaya ya Nyamagana, Jijini Mwanza na gari lake kupatikana Machi 9, mwaka huu, likiwa limeteketea kwa moto ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Ilielezwa kuwa, siku hiyo ya kutoweka, Super Sami alikuwa katika harakati za ununuzi wa nyumba katika mji mdogo wa Ramadi, Wilaya ya Busega, Mkoa wa Simiyu, eneo ambalo ni njia kuu ya kwenda mkoani Mara na jirani na lango la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Mawasiliano yake ya Mwisho:

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya Jeshi la Polisi, watu watano walionaswa imebainika ndio waliwasiliana na marehemu siku ya mwisho na mtandao wa mawasiliano yake unaonesha aliondoka Mwanza saa 4 usiku kuelekea Ramadi.

“Mpaka saa 3 usiku alionekana maeneo ya Buzuruga Nyakato, Mwanza na alipiga simu kwa mkewe, lakini hakurudi, mawasiliano yanaonyesha aliondoka usiku kwenda Ramadi,” zilieleza taarifa za polisi.

Awali kaka wa marehemu alikaririwa akieleza kuwa, siku hiyo (Februari 27), mwaka huu, Josiah alivyoondoka nyumbani kwake alipiga simu kwa mkewe majira ya saa 3 usiku akimueleza kuwa alikuwa akirejea na mgeni, lakini hakufika hadi Machi 9, mwaka huu, gari lake lilipopatikana likiwa limeteketea kwa moto.

Mpaka sasa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limetangaza kuwashikilia watu watano, ambao majina yao hayajatajwa kwa uchunguzi wa kifo cha Super Sami, huku habari za ndani zikieleza kuwa, wanaoshikiliwa ni pamoja na watu waliohusika na kuwasiliana naye siku ya tukio, ikiwa ni pamoja na kutaka kuuziana naye nyumba.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles