29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

MVUA YAZUA KIZAAZAA DAR

  • TMA yatabiri nyingine kubwa Unguja, Pemba, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyara

Na GRACE SHITUNDU- DAR ES SALAAM


MVUA kubwa ilionyesha usiku wa kuamkia jana katika Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani, imeleta athari katika maeneo mbalimbali pamoja na kusababisha adha ya upatikanaji wa usafiri hasa kwa watumiaji wa barabara ya Morogoro.

Athari za mvua hiyo iliyoanza kunyesha saa 12 jioni, zilianza kuonekana alfajiri jana ambako gazeti hili lilitembelea maeneo mbalimbali kushuhudia uharibifu mkubwa ambao umekuwa ukijirudia mara kwa mara.

Baadhi ya mitaa nyumba ziliingia maji, huku nyumba nyingine zikianguka na kusababisha mwanamke mmoja kujeruhiwa wakati akijaribu kutoboa ukuta kutoa maji.

Mapema asubuhi Mwandishi wa gazeti hili alifika katika eneo la Jangwani na kushuhudia eneo hilo likiwa limejaa maji hali iliyofanya magari kushindwa kupita.

Kutokana na hali hiyo, kampuni inayotoa huduma katika mradi wa Mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (Udart), ilisitisha huduma za usafiri wa mabasi hayo kwa saa tano kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa nne asubuhi.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya ofisi zikiwemo zile za umma kuchelewa kuanza kutoa huduma kutokana na wakazi wengi wa kuanzia Mbezi Kimara, Ubungo, Manzese wanaotegemea usafiri huo kutembea kwa miguu, huku wengine wakitumia bodaboda, bajaji na magari binafsi.

Katika kituo cha Mbezi Mwisho, Mwandishi alishuhudia daladala zinazofanya safari ya Mbagala-Kariakoo, Tabata Kinyerezi na Mbezi Gongo la Mboto zikibadili njia pasipo kupitia Jangwani.

Katika Barabara nyingine za jiji kulikuwa na foleni kubwa hali iliyosababisha adha kwa watumiaji wa usafiri wa umma na binafsi pia.

Gazeti hili lilipita katika mitaa ya Ilala ambako baadhi ya nyumba ziliingiliwa na maji ambayo wanadai yalitoka mbali.

Halza Masoud, ni mmoja wa wakazi wa Ilala, aliliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa saa 10 alfajiri waliona maji yanaanza kuingia katika nyumba zao na hivyo kuharibu baadhi ya vitu.

Gazeti hili lilifika pia katika eneo la Gongo la Mboto Mtaa wa Ulongoni A ambako athari ya mvua hizo ni kubwa na kushuhudia baadhi ya nyumba zikiwa zimezingirwa na maji huku mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Mama Biku akijeruhiwa.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Mtaa huo, David Chuma, alisema nyumba hizo zilizopata athari zimejengwa katika hifadhi ya Mto Msimbazi ambazo zote ziliwekewa alama ya X.

“Maji yameingia katika nyumba lakini zilizopata athari zaidi ni nne, mbili zimeanguka na mbili zimepata ufa.

“Lakini pia mwanamke aliyejulikana kwa jina la Mama Biku, alijeruhiwa kwa kuangukiwa na ukuta wakati akijaribu kuutoboa ili maji yatoke nje, alipelekwa katika Hospitali ya Mongolandege na kisha kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Amana,” alisema.

TAARIFA MPYA YA TMA

Wakati huo huo, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imeendelea kutoa tahadhari ya kuwepo kwa mvua kubwa katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Meneja wa Kituo Kikuu cha TMA, Samuel Mbuya, alisema mvua kubwa zinatarajiwa kuanza kunyesha usiku wa Machi 16 hadi 17 katika mikoa ya kanda hizo.

“Tunatarajia ongezeko la mvua kubwa katika Nyanda za Kaskazini mikoa ya Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Kanda ya Nyanda za juu Kaskazini Mashariki ambayo ni mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.

“Ukubwa wa mvua hizi unatokana na msukumo unaotokana na Kimbunga Eliakima ambacho kipo karibu na kisiwa cha Madagascar ambacho kinasababisha ongezeko ya unyevunyevu na kuimarika kwa ukanda wa mvua,” alisema.

Alisema mvua zitakuwa kubwa zenye kuambatana na upepo mkali na radi hivyo wananchi wachukue tahadhari.

Februari 15 mwaka huu, Mkurugenzi wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, akizungumza na vyombo vya habari alitoa mwelekeo wa mvua za masika ambazo alisema zitaanza kunyesha wiki ya kwanza Machi hadi Mei katika maeneo mengi ya nchi kwa wastani mpaka juu ya wastani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles