27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

NABII ALIYEITABIRIA UPINZANI USHINDI AFUTIWA USAJILI

Na AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM


KIONGOZI wa Kanisa la Bethel Ministry nchini,  Nabii Daniel Shilla, amefutiwa usajili wa huduma hiyo kwa madai ya kujihusisha  na  siasa.

Nabii Shilla, kijana mdogo ambaye kanisa lake limekuwa gumzo kutokana na staili yake ya mavazi, nywele na maisha yake kwa ujumla kwa mfano kwenda kwenye kumbi za starehe na kugawa fedha mtaani, amefutiwa usajili huo kwa madai ya kumtabiria ushindi mgombea wa chama cha upinzani katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Kinondoni, uliofanyika Februari 17, mwaka huu.

Akizungumza  jana na tovuti moja, Nabii Shilla ambaye kanisa lake limesajili chini ya mwavuli wa Kanisa la Great Revival Mission Christian linaloongozwa na Askofu Peter Mlai, alisema  taarifa ya kufungiwa huduma hiyo alipatiwa na Askofu aliyemfanyia usajili huo kwa malalamiko ya kwamba amekuwa akijihusisha na siasa.

Nabii Shilla pasipo kufafanua, alisema kabla ya kupatiwa taarifa hizo alikuwa akifuatiliwa na Serikali kwa takribani wiki mbili.

“Askofu wangu aliniambia amesumbuliwa sana na Serikali, ninajihusisha na siasa nikamwambia nimejihusishaje na siasa mbona sihubiri siasa, akaniambia uchaguzi wa Kinondoni uliposti kwenye akaunti yako kwamba mshindi atatoka upinzani na ni kweli maana mpaka sasa sijafuta kwa sababu sio binadamu ni Mungu ndiye amenionyesha.

“Mimi nasema niliongozwa na Mungu kwa sababu sijasema ni uhakika wala sijatangaza kisheria kama wameshinda upinzani, ni haki yangu kikatiba kwa sababu mimi nilikuwa  mtumishi wa Mungu, ni mchungaji ni prophet (nabii) kwa wakati ule nilikuwa na kibali kwanini wameenda kumtishia Bishop (Askofu)?” alihoji Nabii Shilla.

Alisema haamini kama sababu hiyo inatosha kumzuia kutoa huduma hiyo ya kiroho kwa kuwa yeye ni mtu wa maombi na kila anachoongea kinakuwa kimetokana na maombi aliyoyafanya.

Alisema askofu huyo alimweleza kuwa amechukuwa hatua hiyo ili aweze kuokoa huduma yake kwa kuwa amekuwa akisumbuliwa na Serikali.

Nabii Shilla ambaye pia alionyesha vyeti vitatu vya usajili wa huduma yake, alisema ameamua kuweka wazi suala hilo ili Watanzania wajue kwa sababu pia anahofia usalama wake.

“Nimeweka hivi ni kwa usalama wangu, kama nafanyiwa hivi na Watanzania wasipojua naweza nife hata kesho nikaokotwa kwenye kiroba, katika kitu kibaya ambacho Serikali wasiguse watumishi wa Mungu mimi sijawahi kuipinga Serikali, huwa namwombea Magufuli (Rais Dk. John Magufuli), Mkuu wa Mkoa, chama tawala, wapinzani na Watanzania wote,” alisema Nabii Shilla.

Alisema yeye ni nabii wa ukweli hivyo hawezi kukaa kimya akiona kama kuna kifo cha Mtanzania aliyepigwa risasi na akifanya hivyo atakuwa mtumishi wa uongo.

“Nabii wa ukweli anaitabiria Serikali au nabii wa ukweli anaongea kitu anachoongozwa  na Mungu, mimi ni nabii wa Mungu simtumikii binadamu ndiyo maana si mwoga,” alisema Nabii Shilla.

Alisema kutokana na hali hiyo, amepata taarifa ya wito wa kwenda mkoani Dodoma kuonana na Msajili wa Vyama na Jumuiya.

Gazeti hili lilimtafuta kwa njia ya simu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Christina Mwangosi, ili kuzungumzia suala hilo lakini alisema yupo sehemu mbaya na atapiga chumba cha habari atakapopata nafasi.

Kanisa la Bethel Ministry lenye namba ya usajili 14783, lilisajiliwa Aprili 19, 2008 chini ya mwavuli wa Kanisa la The Great Revival Mission Christianity Church.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles