32.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

WASOMI WACHAMBUA UCHUMI WA VIWANDA

Na JOHANES RESPICHIUS – DAR ES SALAAM

IMEELEZWA kuwa ili kufikia uchumi wa kitaifa lazima kila mtu ashirikishwe kikamilifu hususani katika kupata elimu na njia bora za uzalishaji wa bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko.

Hayo yalibainishwa na wasomi wa kada mbalimbali, wakati wakijadili mada ya Uchumi wa Viwanda na Uchumi wa Kitaifa katika mkutano wa Kavazi ya Mwalimu Julius Nyerere uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano huo, Mtafiti Mwandamizi wa Shirika la Utafiti wa Kupunguza Umasikini (Repoa), Blandina Kilama, alisema haitoshi kusema tunataka uchumi wa viwanda kwamba kila mtu awe na kiwanda bali watu wanapaswa kujua ni viwanda gani vinahitajika ili kila mmoja ashiriki kwa nafasi yake.

“Rais Dk. John Magufuli amekuja na sera ya viwanda katika muda mwafaka kwani dira ya mpango wa pili wa maendeleo ulikuwa unasema hivyo si kwamba ni jambo jipya ameanzisha.

“Lakini ili kufika uchumi wa kitaifa lazima uwe jumuishi, sina maana kwamba jumuishi ni kusema kwa kuwa watu fulani wana kipaji cha kupika waungane waanze kupika, hapana kinachohitajika ni kuwapa elimu ya uzalishaji wa bidhaa bora zinazokidhi masoko,” alisema Blandina.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi, alisema misingi ya uchumi wa kitaifa inajengwa kupitia dira shirikishi ya maendeleo ambapo kila kada na kundi la jamii fulani linapaswa kushiriki kwa kutoa maoni yao.

“Tanzania si kwamba hatuna dira ipo, lakini watu walishindwa kuitumia ndiyo maana Dk. Magufuli kwa kuwa ni mfuatiliaji aliiona na kuamua kuitumia, hii sera ya ujenzi wa viwanda ipo kwenye dira si kwamba ameianzisha yeye.

“Ili tufike tunakoelekea katika kufikia uchumi wa kitaifa, lazima tuangalie hata watu wakutusaidia maana lazima uombe misaada kwenye nchi zinazokubaliana na dira yako,” alisema Profesa Moshi.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka UDSM, Profesa John Jingu, alisema katika kutekeleza sera ya viwanda ni vyema ikajulikana ni viwanda vipi vinavyohitajika ambavyo vitalipeleka Taifa katika kujitegemea na kujihudumia.

Alisema uchumi wa viwanda ni vita hivyo ili kushinda lazima nchi yenyewe itengeneze mikakati madhubuti ya kutekeleza sera hiyo.

Kwa mujibu wa Profesa huyo, huko nyuma Tanzania ilishindwa kutekeleza vyema sera hiyo  kutokana na kukaribisha na kukumbatia maoni ya watu ambao wasingependa kuona uchumi wa nchi unakuwa.

“Katika hotuba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alizungumzia kuhusu vita ya kiuchumi kwamba inawezekana ikawa haina bunduki lakini ikawa na madhara makubwa kuliko kutumia risasi.

“Mfano hivi karibuni Serikali ilikuwa inajaribu kuweka mambo sawa katika sekta ya madini kupitia suala la makinikia, mihemko iliyojitokeza ndiyo vita yenyewe,” alisema Profesa Jingu.

Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi, Rehema Tukai, alitaka mpango wa kuhakikisha fedha zinazotumika kwenye miradi ya maendeleo zinabaki nchini.

Alisema asilimia 60 ya fedha zote zinazotolewa kutengeneza miundombinu zinatumika nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na kukosa bidhaa zenye ubora hivyo jitihada zaidi zinapaswa kuelekezwa kwenye kutengeneza bidhaa bora ili fedha zote zitumike hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles