24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAOFISA WA KUDHIBITI DAWA ZA KULEVYA KUANZA KUTUMIA SILAHA ZA MOTO

GABRIEL MUSHI NA ESTHER MBUSSI -DODOMA

BUNGE limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa mwaka 2017, unaoruhusu maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kumiliki na kutumia silaha ikibidi ili kujiwekea kinga ya kiulinzi dhidi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

Pia marekebisho hayo yamependekeza watumiaji wa dawa za kulevya kupata tiba hospitali au kituo cha afya kinachohudumia waraibu wa dawa za kulevya baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kutumia dawa hizo.

Akiwasilisha muswada huo bungeni jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema lengo la marekebisho hayo ni kuiwezesha DCEA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Alisema hatua ya kuruhusu umiliki wa silaha kwa maofisa hao ni kutokana na nguvu za kifedha walizo nazo wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambao humiliki silaha na hivyo kufanya mazingira ya kiutendaji ya mamlaka kuwa hatarishi wakati wa kuwakamata.

“Mamlaka imekuwa ikitumia Jeshi la Polisi kwa ajili ya ulinzi wakati wa kufanya operesheni zake za ukamataji watuhumiwa ambapo wakati mwingine taarifa hupatikana usiku na kuhitaji utekelezaji wa haraka, hali inayowalazimu maofisa wa mamlaka ama kujitoa mhanga na kuhatarisha maisha yao.

“Wakati mwingine huahirisha ukamataji na hivyo kutoa mwanya kwa wafanyabiashara hao kuendelea kufanya biashara hizo kwa uhuru.

“Lengo la marekebisho hayo ni kuiwezesha mamlaka kutekeleza majukumu yake ya kukamata, kupekua na kuzuia mali na vielelezo vya watuhumiwa wa dawa za kulevya na pia kuhakikisha usalama wa watendaji wake na mali,” alisema.

Kuhusu watumiaji wa dawa za kulevya kupelekwa hospitali baada ya kutiwa hatiani, alisema kwa sasa sheria inaitaka mahakama yenyewe kufanya uchunguzi kuhusiana na tabia na mwenendo, afya ya mwili na akili ya mraibu au mtuhumiwa, badala ya kuweka hitaji la taarifa ya daktari na jinsi ya kuipata ili iweze kuisaidia mahakama kufikia uamuzi sahihi na wa haki.

Pia alisema marekebisho hayo yanakusudia kumpa uwezo Kamishna Jenerali wa DCEA kushikilia akaunti za watuhumiwa benki kwa muda ili kurahisisha, kuimarisha na kuboresha taratibu za uchunguzi na kuweka uhakika wa fedha haramu kutotoroshwa nje ya nchi kwa urahisi au kutoharibiwa.

“Sheria ilivyo sasa haimpi uwezo kamishna kuweka zuio au kushikilia akaunti za benki za watuhumiwa, hali inayoathiri utendaji kazi wa mamlaka na kuongeza mwanya wa watuhumiwa kutorosha au kuhamisha fedha haraka wakati wa uchunguzi.

“Sheria ya kutaifisha mali na mazalia ya uhalifu, Sura ya 256 kwa sasa inampa uwezo Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), kuzuia akaunti kwa siku saba, katika kuchunguza mashauri hayo Kamishna humtegemea IGP au Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kuweka zuio hilo,” alisema.

Pia alisema utaratibu huo hufanywa kwa maandishi na hivyo mazingira hayo huweza kumsaidia mtuhumiwa kuhamisha fedha zake kwa haraka na hivyo kupoteza ushahidi.

Kuhusu kifungu cha 53, kinachohusu utaifishaji mali za watuhumiwa wa dawa za kulevya, alisema kifungu kipya kinampa mamlaka Kamishna Jenerali wa DCEA kutoa amri ya kutaifisha mali kwa njia ya kiutawala ili kuepusha uwezekano wa matumizi mabaya ya mamlaka hayo.

“Kifungu hiki pia kinaainisha utaratibu utakaofuatwa wakati wa kukata rufaa kupinga uamuzi wa amri ya utaifishaji mali, sheria hiyo kwa sasa inaweka utaratibu kiutawala kwa kulipa fedha yenye thamani ya mali inayokusudiwa kutaifishwa badala ya mali husika, utaratibu ambao utasimamiwa na Ofisa wa DCEA.

“Aidha, kifungu cha 55 kinafanyiwa marekebisho kwa kufuta kifungu kidogo cha (1) kwa lengo la kuweka utaratibu mzuri wa kufanya makubaliano baina ya nchi yetu na nchi za nje namna ya kusaidiana kutaifisha, kubaini au kukamata mali kwa ajili ya utaifishaji, Sheria ilivyo sasa inaweka utaratibu namna ya kufanya makubaliano baina ya nchi yetu na nchi za nje,” alisema Mhagama.

Pamoja na mambo mengine, alisema sheria mpya inaweka utaratibu rafiki wakati wa kukamata, kupekua, kuzuia mali na vielelezo, kuchukua maelezo ya watuhumiwa na mashahidi na kupeleleza kesi za dawa za kulevya.

Katika kuboresha utaratibu huo, alisema inapendekezwa kifungu hicho kifanyiwe marekebisho kwa lengo la kuboresha utaratibu wa ukusanyaji wa ushahidi kwa njia za kisasa ambazo ni pamoja na kurekodi maelezo kwa njia ya sauti na video.

MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Masoud Abdallah Salum, alisema kwa ujumla marekebisho hayo ni ya kudhibiti kwa kuongeza adhabu kuwa kali zaidi kuliko ilivyokuwa awali na inamaanisha sheria mpya inaweza kupandisha thamani ya dawa la kulevya.

Alisema marekebisho hayo yanaweza yakawa njia ya kumtafuta mchawi badala ya kutibu tatizo la dawa za kulevya.

“Hii ni kwa sabaabu Serikali inaonekana kupunguza kasi ya utoaji wa elimu ya kudhibiti dawa za kulevya badala ya kutoa elimu kwa vijana na kutoa matibabu kwa walioathirika na matumizi ya dawa hizo.

“Kambi Rasmi ya Upinzaani inaona kuwa, mapendekezo ya marekebisho hayo yamelenga watumiaji wa kawaida wa dawa za kulevya badala ya kushughulika na wazalishaji na wasafirishaji wakubwa wa dawa hizo,” alisema.

Kuhusu maofisa kumiliki silaha na kutumia inapobidi, alisema ibara hiyo ni hatari, kwa sababu inaweza kutumiwa vibaya na kusababisha madhara makubwa.

“Tukumbuke kuwa, mwenye mamlaka ya kukamata raia yeyote anayehisiwa au aliyetenda kosa kinyume cha sheria ni askari aliyepewa mafunzo.

“Kitendo cha kuruhusu maofisa hawa ambao haijaelezwa kwenye muswada kama wanayo mafunzo ya kukamata au utaalamu wa kushughulika na wahalifu kama vile askari au maofisa usalama, jambo ambalo ni hatari.”

MAONI YA WABUNGE

Mbunge wa Wawi, Ali Salehe (CUF), aliitaka Serikali kuandaa mikakati maalumu ya kupambana na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya.

Alisema muswada huo unalenga zaidi kutoa adhabu kuliko kutoa elimu kwa umma ili kudhibiti tatizo hilo.

“Hili suala la dawa za kulevya ni la kidunia, lakini kuna utata kati ya Kenya na sisi kuhusu mirungi kwa sababu kwao mirungi ni halali, kwetu si halali. Tusipokuwa makini na unga unaweza kuuzwa kwenye mitandao kama biashara ya ngono inavyouzwa kwenye mitandao.

Naye Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk (CUF), alisema bado ipo mianya mingi ya kuingiza dawa za kulevya.

Alitolea mfano kuwa, viwanja vya ndege hutumika na baadhi ya watumishi wasio waaminifu kwa kuharibu mashine za uchunguzi kwa makusudi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Mlowe (Chadema), aliitaka Serikali kuhakikisha viongozi wanaohusika kupambana na dawa hizo hawatumii mamlaka yao vibaya.

“Kwa mfano Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alipoingia madarakani alianza kukamata watu ovyo. Tafsiri yake ilionekana kama mtu  mwenye chuki. Hivyo naiasa Serikali ihakikishe suala hili halitumiki kisiasa.

“Wafanye kwanza utafiti kabla ya kutoka na kumchukulia mtu hatua ili kuweza kujua kama kweli huyu mtu anatumia au anafanya biashara ya dawa za kulevya,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles