25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MBOWE AWATAKA VIONGOZI WA DINI KUKEMEA UOVU

NA RAYMOND MINJA -IRINGA

MWENYEKITI wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, amesema hawatakubali kuona Rais John Magufuli akizuia uhuru wa demokrasia kwa kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa kwa sababu hana mamlaka hayo kikatiba.

Mbowe alidai Chadema imejengwa kwa maumivu makubwa sana na wanawake na wanaume kujitoa mhanga zaidi ya miaka 25 iliyopita na chama hicho sasa kimeonyesha kuwa na sura ya kitaifa, kwani mpaka sasa Chadema ina wabunge karibu mikoa yote nchini.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni za udiwani katika Kata ya Kitwiru, Manispaa ya Iringa jana, Mbowe alisema kuwa, siasa ni maisha ya watu na watu wanaendesha maisha yao kupitia siasa, hivyo kuwanyima kufanya siasa ni kuminya uhuru wa Watanzania.

Kufuatia hali hiyo, Mbowe aliwataka wapiga kura wa Kata ya Kitwiru, mjini Iringa, kupeleka ujumbe wa hali ngumu ya maisha kwa Rais Dk. John Magufuli kwa kumchagua mgombea wa chama chake kuwa diwani wa kata hiyo.

“Wakati wananchi wakilalamika vyuma vimekaza, watu hawana hela mifukoni, manunuzi yanapungua na baadhi ya biashara ndogo, za kati na za wawekezaji wakubwa zikifungwa, kuna baadhi ya madiwani wa upinzani wananunuliwa kwa kati ya Sh milioni 2 na milioni 5, halafu hela za kodi zinazolipwa na Watanzania masikini zinatumika kuitisha chaguzi ndogo kwa gharama kubwa,” alisema.

Mbowe alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikitumia hadi Sh milioni 200 kugharamia uchaguzi wa kata moja ambayo diwani aliyekuwapo amenunuliwa kwa Sh milioni 5.

Akizungumzia hali ya maisha ya Mtanzania kwa sasa, Mbowe aliwauliza mamia ya wanachi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni uliomnadi mgombea wao wa udiwani wa kata hiyo, Bahati Chengula, tofauti ya kipato na hali ya maisha wanavyoiona sasa na wakati wa utawala wa Jakaya Kikwete; wote walinyoosha vidole wakiashiria wakati wa Kikwete hali ya maisha ilikuwa nafuu.

Akiomba kura, mgombea wa udiwani wa kata hiyo aliwaomba wapiga kura wa kata hiyo wamchague kuwa diwani wao ili akaungane na madiwani wanaounda Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kupitia chama chake hicho kushughulikia changamoto mbalimbali za kimaendeleo.

“Nayafahamu matatizo ya kata hii katika sekta zote, ikiwamo ya afya, elimu, miundombinu ya barabara, maji, maeneo ya biashara na mengine mengi, nipeni kura nikawatumikie,” alisema.

Naye Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Peter Msigwa, alisema ataanza kupiga kambi katika kampeni za kata hiyo kuanzia leo ili aweze kuchukua kata hiyo.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles