23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kangi Lugola atumbuliwa jukwaani

Nora Damian – Dar es Salaam

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ametumbuliwa akiwa jukwaani na Rais Dk. John Magufuli, ikiwa ni siku 572 tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.

Lugola amehudumu kwenye wizara hiyo kwa mwaka mmoja na miezi sita na siku 23 tangu Julai Mosi mwaka juzi alipoteuliwa kushika wadhifa huo baada ya mtangulizi wake, Mwigulu Nchemba kutumbuliwa.

Anakuwa waziri wa tatu kuondolewa katika wizara hiyo tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, baada ya Charles Kitwanga na Mwigulu.

Kitwanga aling’olewa Mei 20, 2016 kwa tuhuma za kuingia bungeni akiwa amelewa na Mwigulu aling’olewa Julai Mosi 2018, kwa kushindwa kushughulikia azimio la Bunge kuhusu suala la kufunga mashine za kielektroniki za utambuzi wa alama za vidole (Afis) katika vituo 108 vya polisi, mradi uliofanywa na Kampuni ya Lugumi kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa nyumba za makazi ya askari Magereza, Ukonga, Rais Magufuli alisema wizara hiyo ni miongoni mwa wizara zinazomtesa sana.

“Kazi ya uongozi saa nyingine ni ngumu sana, ni ngumu, tuna changamoto nyingi. Kama kuna wizara inanitesa ni Wizara ya Mambo ya Ndani, nataka muelewe inanitesa sana.

“Tangu tumeingia madarakani, kuna tume nyingi zimeundwa kuchunguza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa miradi ya ovyo iliyokuwa ikifanyika, na mimi nilitegemea watu watakuwa wanajifunza,” alisema.

MKATABA WA OVYO

Rais Magufuli alisema viongozi wa wizara hiyo walitia saini makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Euro milioni 408.5 (sawa na zaidi ya Sh trilioni 1) kutoka kampuni moja ya nje bila kufuata sheria.

 “Kulikuwa na mkataba wa ovyo unaotengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya Euro milioni 408.

“Umetayarishwa na kusainiwa na Kamishna Jenerali wa Zimamoto, haujapangwa kwenye bajeti, haujapitishwa na Bunge.

“Wakati wa vikao na kampuni moja ya Romania, wahusika wa Tanzania walipokuwa wanakwenda kwenye majadiliano wanalipwa ‘seating allowance’ (posho ya vikao) ya Dola 800 (Sh 1,832,170) na hata tiketi za ndege walilipiwa.

“Yanayokwenda kununuliwa kule kwenye mkataba ni ya ovyo, ni ya ajabu, ukitaka kuuvunja, yale ambayo yameshaanza kutekelezwa lazima yaendelee kutekelezwa,” alisema Rais Magufuli.

Pia alisema maofisa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliohusika kupitisha makubaliano hayo wajitafakari.

Maofisa hao wanadaiwa kupitisha makubaliano hayo wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Andelardus Kilangi alipofiwa na mkewe.

LUGOLA NI MWANAFUNZI WAKE

Rais Magufuli alisema licha ya kwamba Lugola alikuwa ni mwanafunzi wake wakati akifundisha Shule ya Sekondari Sengerema, lakini hafai kuendelea na wadhifa huo.

“Lugola nampenda sana, ni mwanafunzi wangu nimemfundisha Sengerema Sekondari, lakini kwenye hili hapana. Nilitegemea hata hapa sitamkuta.

“Nakueleza Lugola, Kamishna Jenerali (Thobias Andengenye) ninawashangaa kuona mko hapa, sitaki kuwa mnafiki, trilioni moja na zaidi mnasaini wakati sheria zote zinajulikana.

“Kwa hiyo mwanafunzi wangu Lugola nasema kwa dhati nakupenda sana, lakini kwenye hili hapana.

“Umenisifia sana hapa nakushukuru, lakini kwenye hili hapana, ni lazima niwe mkweli,” alisema Rais Magufuli.

Alisema wapo wanaohusika kwenye wizara hiyo, hasa kitengo cha Zimamoto, hivyo akawataka wasaidizi wa Andengenye wajitathmini.

“Andengenye nampenda sana ni mchapakazi, umejenga nyumba mpaka Chato, lakini kwenye hili hapana, nilitegemea asiwepo hapa.

“Unakwenda Ulaya unasaini mradi ambao haujapitishwa hata na Bunge… ‘no’, nitaendelea kuwapenda, lakini kwenye ‘position’ hii ‘no’,” alisema Rais Magufuli.

Alisema chini ya utawala wake anataka watu wafaidi na kwamba urafiki na upendo utaendelea, lakini katika suala la kazi hataki mchezo.

KUJIUZULU KWA KATIBU MKUU

Rais Magufuli pia ameridhia kujiuzulu kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu.

“Katibu Mkuu Mambo ya Ndani nampongeza sana kwa kuwajibika na hii imempa heshima, inawezekana hakuyafanya yeye, ninampongeza.

“Yule atakayekuwa anajikwaa iwe kwa makusudi au bahati mbaya, sasa ukianguka nenda ukajipange vizuri.

“Urafiki, upendo uko palepale lakini katika suala la kazi no way…that’s me, utawala wangu hapana nataka watu wafaidi kwelikweli,” alisema.

NYUMBA ZA MAGEREZA

Rais Magufuli alilitaka Jeshi la Magereza lijitathmini upya na kuacha kufanyiwa kazi na majeshi mengine wakati lina nguvu kazi ya kutosha.

“Magereza nawapenda, lakini siwezi nikaacha kuwasema. Kambi za JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) ziko 24, wenye kambi 24 wanakwenda kuwajengea wenye kambi 129, tuna wajibu wa kujitathmini.

“Tulishindwa kujijengea sisi wenyewe nyumba, udongo, kuni zipo, ukichoma matofali yatapatikana, tumeshindwa nini?” alihoji Rais Magufuli.

Alisema kwa takwimu za jana kuna mahabusu 32,208 na wafungwa zaidi ya 13,000 ambao ni nguvu kazi inayoweza kutumiwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Kila mahali wanaposhindwa wengine unapeleka JKT, ninachojiuliza, Magereza mmeshindwaje kujifunza huko? Kwanini msichukue hata askari magereza mkawapeleka JKT wakajifunze huko, mbona kozi ni zilezile?” alihoji.

Alilitaka jeshi hilo kujipanga kuimarisha makazi ya askari kwani baadhi yao wanateseka kwa kuishi kwenye nyumba zinazovuja na wakati mwingine wanaweka plastiki kuzuia mvua.

 “Unapofika mahali nyumba zilizojengwa tangu enzi za ukoloni lakini hazikarabatiwi wakati kuna wafungwa wanakula na kulala bure, ni jambo la kusikitisha.

“JKT wamevuta maji mpaka hapa, lakini Magereza hawajayaingiza kwenye nyumba, kwa hiyo hawajataka kupanga mikakati ya kuingiza maji… kazi ipo. Hakikisheni maji yanaingia kabla askari hawajahamia.

“Anayetaka kufanya kazi na mimi afuate yale ninayotaka, haiwezekani askari magereza unakuta wamekaa kama watumwa kwenye manyumba ya ajabu ajabu ya miaka na miaka, kama kuna mahali pa kwenda kuombewa tukaombewe,” alisema Rais Magufuli.

Nyumba hizo zina uwezo wa kuchukua familia 172 na kupunguza changamoto ya makazi kwa asilimia 48.8.

KIWANDA CHA BIDHAA ZA NGOZI

Rais Magufuli alishangazwa kuona jeshi hilo linashindwa kukamilisha kwa wakati mradi wa kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi kilichopo mkoani Kilimanjaro licha ya kwamba nao una ubia.

Alisema Magereza iliingia ubia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) mkataba wa Sh bilioni 9 kwa mradi huo, lakini hadi sasa jengo halijamalizika.

“Mashine zilifika bandarini Januari 18, wamejenga jengo asilimia 49 na mradi huo wana ubia.

“PSSSF wameniomba, wanaomba JKT, nyumba mmejengewa, sasa hata kiwanda mtakachozalisha fedha nacho mjengewe na JKT?

“Nimeshazungumza na Kamishna Jenerali zaidi ya mara tatu, nimeona nizungumze hapa hapa ili upele unaoniwasha muusikie unawasha sehemu gani.

“Ni mara kumi mimi nisiwe rais nikakae kwetu Chato, lakini kwa wakati huu lazima tuelezane ukweli, mbona Jeshi la Wananchi wanafanikiwa,” alisema Rais Magufuli.

ATISHIA KUIVUNJA TBA

Aidha, Rais Magufuli aliwaonya Wakala wa Majengo (TBA) huku akitahadharisha kuwa wasipobadilika huenda ikavunjwa.

“TBA ninyi siwapongezi kwa sababu mlipewa kazi na hamkupanga ‘structure’ ya kufanya kazi.

“Mlitumia miezi 20 kujenga asilimia 40 – 45, JKT wametumia miezi sita kujenga asilimia 55.

“TBA isipobadilika siku zijazo itavunjwa, tuwe na watu wanaojituma kufanya kazi,” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles