33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Lipumba amng’oa mpambe wake CUF

Elizabeth Hombo-Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amemtumbua aliyekuwa Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Abdul Kambaya.

Agosti mwaka 2015, wakati wa mgogoro ndani ya CUF, uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili na kusababisha chama hicho kupasuka vipande viwili, chanzo chake kilikuwa ni Profesa Lipumba kutangaza kujivua uenyekiti na mwaka mmoja baadaye alitaka kurejea katika nafasi hiyo.

Hatua yake ya kutaka kurejea katika nafasi hiyo, ililalamikiwa na upande wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad huku waliokuwa upande wake akiwamo Kambaya walisimama kumtetea hadi dakika za mwisho.

Katika hali ambayo imewashangaza wafuatiliaji wa siasa hapa nchini, ni baada ya jana taarifa kusambaa katika mitandao ya kijamii kuwa Profesa Lipumba amemtumbua Kambaya.

Kutokana na taarifa hizo, MTANZANIA ilimtafuta Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, Magdalena Sakaya ambaye pamoja na mambo mengine alisema hayo ni mabadiliko ya kawaida ndani ya CUF.

Alisema kwa mujibu wa katiba yao, mwenyekiti wa chama ana mamlaka ya kuteua na kutengua wakati wowote anaoona inafaa, hivyo hakuna jambo la kushangaza.

“Ni kweli Kambaya uteuzi wake umetenguliwa na baadaye akaandika barua ya kujiuzulu na ataendelea kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Mkutano Mkuu wa Taifa,” alisema Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua.

Alisema nafasi ya Kambaya imechukuliwa na Mohamed Ngulangwa ambaye awali alikuwa Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bunge na Sera.

Kutokana na hilo, alisema Mneke Jafar ameteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bunge na Sera, huku Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi anakuwa Juma Kilaghai.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Profesa Lipumba, mabadiliko hayo yatakamilika yatakapothibishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa katika kikao chake kijacho.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa uongozi wa kurugenzi nyingine unabaki kama ulivyo hivi sasa.

Hata hivyo taarifa kutoka ndani ya CUF zinaeleza kuwa siku tatu zilizopita Profesa Lipumba alifanya kikao cha ndani na wakurugezi wake kwa kile kilichoelezwa kusikiliza mgogoro unaofukuta ndani ya chama.

Inaelezwa kuwa mmoja wa wakurugenzi hao anadaiwa kuwa alikuwa kwenye mikakati, ikiwamo kuandaa makundi ya kumpinga Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Maftaha Nachuma, jambo ambalo linaonekana kuibuka kwa mpasuko mwingine baada ya ule wa aliyekuwa Katibu Mkuu wake Maalim Seif.

Mwaka 2015 wakati wa Uchaguzi Mkuu, CUF ilikumbwa na mgogoro baada ya Profesa Lipumba kutangaza kujivua wadhifa wa uenyekiti wa chama hicho, akipinga ujio wa Edward Lowassa kugombea urais kupitia Chadema na kuviwakilisha vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo ni CUF, Chadema, NCCR na NLD.

Profesa Lipumba alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Ukawa baada ya vyama husika kujitoa kwenye vikao vya Bunge maalumu la katiba jijini Dodoma, Aprili mwaka 2014.

Baada ya Profesa Lipumba kujitoa, CUF chini ya Katibu mkuu, Maalim Seif ilimteua Julius Mtatiro (sasa amehamia CCM) kuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi.

Chama hicho kilikwenda katika uchaguzi bila ya kuwa na mwenyekiti wa chama. Hata hivyo, kilipambana na kufanikiwa kupata wabunge 42 Zanzibar na Tanzania bara wakiwamo wa viti maalumu.

Jambo kubwa ambalo wachambuzi wa siasa waliulaumu upande wa Maalim Seif, ni kutoitisha mkutano mkuu mapema ili kuziba pengo la Profesa Lipumba alipotangaza kukaa pembeni.

Mkutano mkuu ulipoitishwa mwaka mmoja baadaye, Agosti 2016, Profesa Lipumba aliandika barua ya kurejea kwenye nafasi yake na kuhudhuria mkutanoni hatua iliyolalamikiwa na upande wa Maalim Seif.

Hatua hiyo ilisababisha mkutano huo uliotakiwa kufanya uchaguzi, kuvunjika kutokana na mvutano wa pande mbili.

Siku chache baadaye, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilimtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF, jambo lililoongeza ‘chumvi’ kwenye mgogoro huo.

Baadaye upande wa Maalim Seif ukafungua kesi Mahakama Kuu kumpinga Profesa Lipumba.

Hata hivyo, Machi 18 mwaka jana, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa hukumu inayotambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.

Kutokana na uamuzi huo wa mahakama, Maalim Seif na wafuasi wake wakajiondoa na kujiunga na chama cha ACT Wazalendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles