23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Lugola atoa neno baada ya kutumbuliwa

Andrew Msechu – Dar es Salaam

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, amesema anaunga mkono hatua alizozichukua Rais Dk. John Magufuli, kutengua uteuzi wake akisema ni nzuri zinazolenga kujenga safu ya Serikali ya awamu ya tano.

Alisema pamoja na hatua hiyo, yeye akiwa mbunge aliyewahi kupata nafasi ya kumsaidia Rais, ataendelea kumsaidia na kutumikia Serikali ya awamu ya tano kwa heshima kwa kuzingatia heshima ambayo alimpatia.

“Kwa hiyo mimi niko vizuri tu na wala msidhani kuwa kuna shida imenitokea katika hatua hizo, kwa kuwa hatua alizochukua Rais ni nzuri na njema kabisa, naomba muelewe hivyo,” alisema Lugola.

Alisema kwa sasa hawezi kurudia kuelezea tuhuma zilizosababisha Rais achukue uamuzi wa kutengua uteuzi wake kwa kuwa tayari ameshazungumza na Watanzania na ameshaziweka wazi.

“Siwezi kurudia kuzungumzia tuhuma hizo, Rais amezungumza na Watanzania, kwa hiyo amewaeleza na mimi sioni sababu ya kuendelea kurudia kwa sababu ameshazungumza na umma wa Watanzania.

“Mimi ninaomba Watazannia waendelee kumwamini Rais na waendelee kumuunga mkono katika juhudi za Serikali na sisi tutaendelea kumuunga mkono,” alisisitiza.

Kwa mawaziri waliobaki, Lugola aliwaasa waendelee kuchapa kazi.

“Sisi wabunge wa CCM wakichukuliwa wachache kuunda Baraza la Mawaziri, wengine wanaokuwa kwenye benchi ni kama wachezaji, wakati wote wanaendelea kupiga jaramba na wanaweza kuingia uwanjani,” alisema Lugola.

Alisema kwa maana hiyo mawaziri waliobaki na kwa walioko benchi (akiwemo yeye) wataendeela kuwatia moyo na kuwasaidia waendelee kuchapa kazi na waendelee kumsaidia Rais hadi watakapomaliza awamu hii na kuingia kwenye uchaguzi.

“Ninaamini mawaziri waliopo wanafanya vizuri na tunaenda vizuri,” alisema Lugola.

WAKATI WA HUKUMU

Wakati Rais Magufuli akiueleza umma kuhusu namna anavyoshangaa kumwona Lugola kwenye mkutano huo akiwa haonyeshi hata kuwajibika kwa tuhuma alizozitaja, mbunge huyo alionekana kuwa mkimya.

Hata hivyo, kadiri Rais Magufuli alivyokuwa akiendelea kutaja tuhuma hizo na kueleza kwanini anaona hawezi kuendelea kumwacha Lugola na Kamishna wa Zimamoto, Thobias Andegenye katika nyadhifa zao, aliendelea kumsikiliza kwa makini, lakini akionyesha kuishiwa nguvu.

Hata baada ya Rais Magufuli kumaliza hotuba yake na kushuka jukwaani, Lugola aliinuka taratibu akishikwa mkono na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba, ambaye alizungumza naye maneno machache kisha kusogea taratibu kuelekea kwenye ngazi za jukwaa kuu.

Baada ya Rais Magufuli kushuka jukwaani, alielekea kuwasalimia maofisa wa Serikali na kuwapongeza wanamuziki wa bendi za Magereza na Jeshi la Wananchi (JWTZ), na Lugola alisogea akiambatana na viongozi wengine, kusubiri kiongozi huyo amalize mzunguko huo kisha waagane naye.

Rais Magufuli alimalizia mzunguko wake na kuwaaga viongozi waliokuwa wakimsubiri kwa kuwapungia mkono  kisha akaingia katika gari na kuondoka.

LUGOLA AKIHUTUBIA

Awali, katika hotuba yake kwa Rais Magufuli na umma uliokusanyika katika uzinduzi huo wa nyumba za Magereza, Lugola alianza kwa kumsifia Rais Magufuli na kusema ‘hakuna kama Magufuli’.

“Tanzania hoyoee, Magufuli hoyeee, nani kama Magufuliiii?…,” aliuliza Lugola huku akijibiwa na umati uliokusanyika hapo “hakunaaaa…”

Baada ya kujibiwa salamu hiyo, alianza kwa kujibu utani wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kusema hata waliofungwa katika mchezo wa mpira wa miguu kule Singida wana amani kwa kuwa wamejifunza kupokea matokeo, baada ya kufungwa 3-1 na Yanga juzi.

Alisema jambo muhimu la kuwakumbusha Watanzania ni kuhusu Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015 ambayo ndiyo mkataba baina ya CCM na wapigakura.

Lugola alisema kwamba kwa mujibu wa ibara ya nne, aliwaahidi Watanzania kuwa Serikali itahakikisha kuna usalama, utulivu na maisha na mali zao vitalindwa kwa nguvu zote.

Alisema wakati wizara yake ikiendelea kuwathibitishia Watanzania kuwa japokuwa bado muda mfupi, Rais Magufuli ameweza kutekeleza ilani hiyo na sasa hakuna tena matukio ya ujambazi, ajali za barabarani zimepungua.

Lugola alisema zamani wananchi walikuwa wakiogopa majambazi kusafiri safari za usiku na kufikia hatua majambazi yakawa yanapanga ratiba za Watanzania na sasa anathibitishia umma kuwa wananchi wanasafiri popote bila wasiwasi.

Alisema katika ibara ya 146 ya Ilani imewahakikishia kuwa itajenga makazi kwa ajili ya vyombo vya usalama na kwamba kama kuna wakati Rais amewasaidia makazi vyombo vya ulinzi na usalama ni katika Awamu ya Tano.

Lugola alisema tangu mkoloni alipoondoka nchini, Jeshi la Magereza halikuwa na nyumba hata moja ya ghorofa katika eneo hilo, lakini sasa ina majengo 12 ya ghorofa ambayo yanaweza kuhifadhi askari wengi wa kutosha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,411FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles