KAGERE AANZA LIGI NA REKODI YA KIPEKEE

0
924

 

NA MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Meddie Kagere, ameanza kwa kishindo baada ya kuweka rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi katika michezo iliyochezwa siku ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kagere, ambaye amejiunga Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya, alifunga bao hilo dakika ya pili katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, uliochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Simba ilichomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya askari jela hao.

Mabao mengine siku hiyo yalifungwa dakika ya tisa na mshambuliaji wa Mwadui FC, Salumu Ijee, katika mchezo kati ya timu hiyo na Kagera Sugar katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba. Mchezo huo ulimalizika kwa Kagera Sugar  kushinda mabao 2-1.

Mshambuliaji Omary Mponda aliyejiunga na Kagera Sugar akitokea Ndanda FC, alifunga mabao mawili, dakika za 20 na 29.

Zawadi Mauya aliifungia Lipuli bao dakika ya 59 katika mchezo ambao wenyeji Coastal Union walilazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Bao la kusawazisha la Coastal Union lilifungwa na Bakar Mwamnyeto dakika ya 68.

Wengine ni Vitalis Mayanga wa Ndanda FC, aliyeifungia timu hiyo bao dakika ya 68 katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini, mkoani Pwani, wakati Evageristus Mujwahuki aliifungia Mbao bao pekee dakika ya 80 katika mchezo dhidi ya Alliance Academy kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here