24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

GBP INAVYOJIPANGA KUTUMIA FURSA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA

Na WAANDISHI WETU

Gulf Bulk Petroleum (GBP), ni kampuni ya kizalendo iliyoanzishwa mwaka 2000, ambayo inajishughulisha na uagizaji na usafirishaji wa nishati ya mafuta ya petroli, dizeli, ya taa na ya ndege.

Tangu Januari 2012 Serikali ilipoanzisha mfumo wa pamoja wa uagizaji mafuta, Julai mwaka huu kwa mara ya kwanza, GBP imekuwa kampuni ya kwanza ya kizalendo kushinda zabuni hiyo na sasa itaingiza nchini tani 37,975 za petroli na 30,031 za mafuta ya ndege (Jet A-1).

GBP yenye zaidi ya vituo 40 vya kuuza mafuta kwa rejareja nchi nzima, imekuwa pia kampuni ya kwanza ya kizalendo kuwa na bohari yenye uwezo wa kuhifadhi lita 122,600,000 za mafuta kwa wakati mmoja, ambayo ufanisi wake umeanza baada ya meli za mafuta kuanza kupakulia bandari ya Tanga.

GBP ambayo kwa sasa inajivunia kuwa miongoni mwa makampuni ya kizalendo yenye mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi, huagiza wastani wa tani 20,000 hadi 25,000 za mafuta kwa mwezi.

Fursa kubwa

Mkurugenzi mtendaji wa GBP, Badar Sood anasema mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanzania, ni fursa kubwa kwa kampuni yake na Mkoa wa Tanga kwa ujumla.

“Tumeufurahia, tunaipongeza sana Serikali yetu kwa kuuleta mradi huu hapa Tanga kwa kuwa ni fursa kwetu.

“Sisi kama GBP tumejipanga kuuza mafuta kwa meli zote za kigeni zitakazokuja kuchukua mafuta ghafi hapa Tanga, ni wazi kuwa zitahitaji mafuta ya kuondokea, sisi tupo tayari kuzipatia huduma hiyo,” anasema.

Aidha anasema kampuni yake pia imejiandaa vyema kutoa huduma ya mafuta kuanzia kipindi cha ujenzi wa bomba hilo hadi litakapokamilika miaka mitatu ijayo.

“Kama ambavyo nimeeleza hapo awali, tuna mpango wa kupanua uwezo wetu wa kuhifadhi mafuta hadi kufikia lita milioni 300. Hii ni katika jitihada za kuhakikisha kuwa pamoja na mambo mengine, tunatumia fursa zitakajitokeza kutokana na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi,” anasema.

Dk. Magufuli aguswa

Alipokuwa katika ziara yake ya kiserikali mkoani Tanga, Rais Dk. John Magufuli, alizindua rasmi bohari kubwa ya kuhifadhi mafuta iliyojengwa na kampuni hiyo kuhudumia mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kupunguza mlundikano wa malori Dar es Salaam.

Akizindua bohari hiyo, Rais Magufuli alitamka wazi kuwa  ameguswa na mchango wa kampuni hiyo inayomilikiwa na wazawa na kuahidi kuwa Serikali ipo nyuma yake kuhakikisha inakua zaidi ili iweze kutoa ajira zaidi na kuchangia katika uchumi wa nchi.

Rais Magufuli ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kutoa upendeleo wa pekee kwa uwekezaji wowote unaofanywa na wazawa, alisema serikali yake itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa wawekezaji wote, huku wazawa watapewa kipaumbele.

Akizindua matenki yenye uwezo wa kuhifadhi lita 122,600,000 za mafuta kwa wakati mmoja yanayomilikiwa na kampuni hiyo jijini Tanga, Rais Magufuli aliahidi kuwa nyuma ya jitihada kubwa inazozifanya.

Akisoma hotuba yake mbele ya Rais Magufuli, Sood, alisema wamelipa kodi inayofikia shilingi bilioni 208  katika kipindi cha mwaka 2015/2016 na shilingi bilioni 293.2 kwa kipindi cha mwaka 2016/2017.

Mipango ya kujitanua

 Sood alimweleza Rais Magufuli kuwa kampuni yake ina lengo la kufanya upanuzi zaidi na kufikia uwezo wa kuhifadhi lita milioni 300 kwa wakati mmoja.

Pamoja na upanuzi wa bohari ya kuhifadhia mafuta, alisema kampuni yake pia imeweza kujipenyeza hadi katika nchi jirani ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako inauza mafuta na kwamba wana mpango wa kuwekeza zaidi katika nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, GBP kwa sasa ina sehemu ya kuhifadhi mafuta (depo) moja yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni nne ambazo hupokewa kabla kusambazwa sehemu mbalimbali nchini humo.

Kuhusu mpango wa kupanua shughuli zake DRC, Sood anasema watasafirisha mafuta kwa njia ya reli kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma na baadaye yatapakiwa kwenye meli kupitia Ziwa Tanganyika hadi Bandari ya Kalemii.

Akiwa mwenye furaha, Rais Magufuli alimwahidi mkurugenzi huyo kuwa atazungumza na Rais wa DRC ili kuona uwezekano wa kurahisisha na kuharakisha lengo lake la kuwekeza na kufanya biashara zaidi katika nchi hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na MTANZANIA ofisini kwake jijini Tanga, Sood alisema ujenzi wa matenki aliyoyazindua rais ni wa awamu ya kwanza, ambao umewawezesha kulipa kiasi kikubwa cha kodi serikalini.

Kuhusu mchango wake kupitia ajira, Sood anasema kampuni yake imeajiri zaidi ya watu 1,000 kwa sasa na kuongeza kuwa awamu ya pili ya upanuzi itakapomalizika ajira zaidi zitaweza kupatikana.

Aidha mbali na uwekezaji huo, anasema GBP ina mpango wa kuwekeza kiwanda cha kutengeneza vilainishi vya mitambo (lubricants) na cha kusindika gesi (LPG).

“Uwekezaji ambao tumepanga kuufanya unatarajia kugharimu takribani Sh bilioni 60,” anasema.
Changamoto

Akizungumzia baadhi ya changamoto ambazo wanakumbana nazo katika sekta ya mafuta, Sood anasema ni pamoja na wingi wa kodi katika bidhaa hiyo muhimu.

Kuhusu kupanda na kushuka kwa mafuta, anasema “Wakati mwingine utakuta umehifadhi mzigo mkubwa na kabla haujakwisha bei zinashuka ghafla. Kutokana na hili unalazimika kushusha bei kuendana na bei mpya elekezi japokuwa ulinunua kwa bei ya juu,” anasema.

Hata hivyo anasema kwa asili ya biashara ya mafuta hili si tatizo kubwa sana kwani wakati mwingine hupanda wakati wakiwa na hifadhi kubwa ya mafuta ambayo wameinunua kwa bei ya chini.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles