24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

MIILI 13 FAMILIA YA NAIBU WAZIRI YAAGWA DAR

Na LEONARD MANG’OHA -DAR ES SALAAM

VIONGOZI mbalimbali wa Serikali wamewaongoza wananchi jijini Dar es Salaam kuaga miili ya watu 13, ndugu wa aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Gregory Teu, waliofariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Uganda.

Miili hiyo 13 iliagwa jana katika hospitali ya jeshi Lugalo baada ya kuwasili juzi usiku kwa ndege ikisindikizwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Jiji la Kampala Uganda, Bety Kamya, aliyemwakilisha Rais Yoweri Museveni.

Baada ya kuagwa, miili sita kati ya hiyo ilisafiriswa kwenda Mpwapwa mkoani Dodoma, Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro kwa taratibu nyingine za mazishi huku mwili mmoja wa Digna Mwacha ukitarajiwa kuzikwa kesho Chanika, Dar es Salaam.

Waliohudhuria tukio la kuagwa kwa miili hiyo ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, aliyepokea hati ya kuwasili kwa miili hiyo.

Wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Suzan Kolimba, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na Balozi wa Uganda nchini, Richard Kabonelo.

Akizungumza wakati wa kupokea kuaga miili hiyo, Waziri Kairuki alisema Serikali imepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa msiba huo mkubwa kwa nchini.

Alisema vifo hivy vya watu 13 ni pigo kwa Serikali kwa sababu imepoteza nguvu kazi na watumishi wa umma.

“Kufuatia taarifa ya msiba huu Rais aliagiza Wizara ya Mambo ya Nje kuhakikisha inasimamia usafirishaji wa miili hii kutoka Uganda, kuiihifadhi hapa katika hospitali ya Lugalo na kuisafirisha kwenda sehemu mbalimbali za nchi itakakokwenda kuzikwa.

“Tunashukuru hilo limeweza kufanyika na jana saa 3:00 iliweza kuwasili nchini kwa ndege ya kukodi iliyogharamiwa na serikali ya Uganda …tunaishukuru sana kwa ushirikiano iliouonyesha,” alisema Waziri Kairuki.

Awali, akiongoza ibada ya kugwa miili hiyo, Mchungaji Jackson Sostheness, aliwataka wananchi kuwa tayari kwa vile anayejua maisha ya mwanadamu na kuyamiliki ni Mungu pekee.

Mawazo yao yalikuwa waende kule wakafurahie, washuhudie, wapige picha, warudi waelezee jinsi mambo yalivyofanyika.

“Tena yawezekana waliwasiliana na ndugu zao kuwa sasa tumeanza safari ya kurudi, tena wakasema maneno mazuri Mugu akipenda kesho tutafika huko,” alisema Mchungaji Sostheness.

Alisema ikiwa wangeelezwa kabla kuwa wakwenda huko na watakufa hakuna ambaye angekubali kusafiri.

Naye Mchungaji Jerome Napela aliwataka wanandoa ambao marehemu hao walikuwa wakitoka katika harusi yao kutokata tamaa bali watumie tukio hilo kudumisha mapenzi yao kwa vile hawafahamu sababu ya Mungu kuamua ajali hiyo itokee wakati wa sherehe yao.

Waziri Bety wa Uganda alisema uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles