23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

BIASHARA YA MKAA YAHUSISHWA NA UGAIDI

Na DENNIS LUAMBANO- TANGA


BIASHARA ya mkaa inayofanywa na wahamiaji haramu kutoka Kenya, inadaiwa kuhusishwa na vitendo vya kigaidi.

Akizungumza mjini hapa juzi wakati wa ziara ya ukaguzi wa shughuli za uhifadhi wa mazingira, Meneja Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Wilaya ya Mkinga, Frank Chambo, alisema taarifa za biashara hiyo kujihusisha na ugaidi walizipata kutoka kwa mamlaka za Kenya.

Chambo alisema wahamiaji hao haramu kutoka Kenya wanaojulikana kwa jina la Waduruma, wanaandaa mkaa huo katika msitu uliopo Kata za Mwakijembe, Duga, Daruni na Bwiti wilayani Mkinga, jirani na mpaka wa Horohoro.

"Wahamiaji hao wanatoka Kenya, wamevamia maeneo ya msitu huo ambao zamani yalikuwa ya wazi yakiwa na idadi ndogo ya watu, lakini ardhi ni kubwa na wanaharibu mazingira kwa kukata miti na kuchoma mkaa.

“Mwanzoni mkaa huo walikuwa wanauchoma kama kilomita tano kutoka mpakani, lakini sasa hivi wameshafika kilomita 100.

"Kwa kawaida huwa tunafanya vikao vya pamoja na wenzetu wa Wakala wa Misitu wa Kenya (KFS) na taarifa za kiintelijensia walizotupa Oktoba mwaka jana, ni kwamba biashara hiyo ya mkaa inahusishwa na vitendo vya kigaidi kwa maana fedha inayopatikana baada ya mkaa huo kuuzwa nchini humo au unaposafirishwa kwenda kuuzwa nchi nyingine, ndiyo inayofadhili shughuli hizo," alisema Chambo.

Alisema kwamba, karibia maeneo yote ya kata hizo yanakaliwa na wahamiaji hao baada ya kuhamia muda mrefu.

"Karibu watu wote wanaoishi katika maeneo hayo ni wahamiaji haramu na wengine hadi wamekuwa viongozi wa vijiji. Kwa hiyo, hata kupata taarifa za namna wanavyoharibu misitu yetu inakuwa ni vigumu," alisema Chambo.

Alisema wahamiaji hao pia wanakata miti iliyopo katika Msitu wa Kisiwa cha Kirui kwa ajili ya kuchoma mkaa, kuchonga vinyago na kutengeneza samani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Yona Maki, alisema inawezekana fedha za biashara ya mkaa huo zikatumika kufadhili vitendo vya ugaidi nchini Kenya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles