23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

KAIRUKI ASEMA TPSC KUWA NA MAJENGO YAKE 

NA MWANDISHI WETU –  MBEYA


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, amesema Serikali itahakikisha Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) Tawi la Mbeya, kinapata majengo yake ili kupunguza gharama za uendeshaji.


Kwa sasa chuo hicho kinatumia majengo ya kukodi ambayo ni mali ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya yaliyopo eneo la Soko Matola, huku kikihudumia wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.


Akiwasilisha taarifa ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala na Serikali za Mitaa, Waziri Kairuki alisema gharama ya kodi inayofikia Sh milioni 24 kwa mwezi ni kubwa mno.


Kutokana na hilo, alisema Serikali iko katika mchakato wa kuhakikisha chuo hicho kinamilikishwa majengo hayo ili kupunguza gharama za uendeshaji.


Kairuki alisema: “Serikali itahakikisha kwamba chuo kinakuwa na wakufunzi wa kutosha ili kuendesha kozi zake kwa ufanisi. 
Mkuu wa TPSC, Dk.Henry Mambo, aliiambia Kamati hiyo kuwa, tawi hilo lililozinduliwa mwaka 2014 likiwa na wanafunzi 453, linaendelea kukua kwa kasi ambapo kwa sasa wana wanafunzi 1236.


 “Tawi linakua kwa kasi na sisi kama chuo, tunaziona changamoto hizo na tunajitahidi kukabiliana nazo, baadhi ya changamoto hizo ni mahitaji ya miundombinu ya kufundishia,” alisema Dk. Mambo.


Aidha, aliongeza kuwa mbali na changamoto hizo, Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha chuo kinafanya kazi zake kwa ufanisi kwa kutoa elimu kwa watumishi wa umma na tarajiwa.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala na Serikali za Mitaa, Josson Rweikiza, alikipongeza chuo hicho na kusema kuwa kina mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.
“Changamoto ni muhimu katika uhai wa kila kitu, kama hakuna changamoto basi hakuna maisha, tunawapongeza na kuwatia moyo katika kutekeleza majukumu yenu,” alisema. 

Awali Waziri Kairuki alisema TPSC hutoa ushauri wa kitaalamu kwa wizara, idara, wakala za Serikali, mamlaka za Serikali za mitaa na sekta binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles