28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

ZITTO AGONGA MWAMBA EALA

*Spika Ndugai agomea maombi yake kikanuni

*Wagombea ‘wanyukana’ kila kona Dodoma


Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo),  amegonga mwamba baada ya Kamati ya Kanuni ya Bunge kutoa msimamo wake kuhusu uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Hatua hiyo inatokana na Zitto kuwasilisha barua kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, Machi 28, mwaka huu akitaka kamati hiyo kutoa ufafanuzi wa mgombe wa kundi C ili kila chama kiweze kushiriki uchaguzi, badala ya kupewa kwa vyama vilivyokuwa na idadi kubwa ya wabunge.

Kutokana na Tangazo la Bunge kwenye gazeti namba 11 la Machi 17, lililotangaza uchaguzi huo na masharti yake, Zitto, alisema mwongozo wa uchaguzi huo unavunja kanuni mbalimbali na kwamba kitakachofanyika sasa kitakuwa ni uteuzi na si uchaguzi.

Alisema pia mwongozo huo, mbali na kuvunja mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotaka suala la jinsi lizingatiwe kwenye wabunge wanaokwenda kuiwakilisha nchi katika Bunge hilo, lakini pia inavinyima vyama vingine vyenye uwakilishi bungeni haki ya kuchaguliwa.

Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Kanuni, kilichokutana juzi mjini Dodoma chini ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, huku Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson akihudhuria.

Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na  Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Wengine ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe pamoja na wajumbe kadhaa, ambapo baada ya kufunguliwa kwa kikao hicho kilichomalizika usiku wa juzi, Spika Ndugai, alihoji uhalali wa Zitto kuandika barua ya kuhoji mgawanyo huo wa wabunge wa EALA.

“Kifupi ni kwamba Zitto amekwama na hana tena namna maana Spika alimsema sana kutokana na mgawanyo lakini kabla ya kuendelea zaidi kwamba alimuuliza Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Kabudi kama kuna tatizo naye akasema hakuna na Spika hajakosea.

“… ila ni kikao ambacho Spika kwa kweli amesimamia sheria na ni kiongozi asiyeyumba katika kusimamia sheria, sasa tunakwenda kwenye uchaguzi huku ukweli ukiwa umeshajulikana, CCM watakuwa na viti sita, Chadema viwili na CUF kimoja,” alisema mtoa habari huyo ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini.

Baaada ya majadiliano ya kina na ufafanuzi wa kisheria kuhusu mgawanyo huo wajumbe wa Kamati ya Kanuni walikubaliana na Spika Ndugai kwa kauli moja, huku hoja ya Zitto ikitupwa na uchaguzi huo wa EALA  utafanyika kwa kuzingatia uwiano wa idadi ya wabunge wa vyama vyenye uwakilishi bungeni.

Hata hivyo kanuni ya 5(5) ya nyongeza ya tatu ya kanuni za Bunge inaeleza “Chama  chochote cha siasa chenye haki ya kusimamisha mgombea wa EALA kinaweza kuweka wagombea watatu katika  ya wagombea ubunge”.

Kutokana na hilo msingi huo wa kikanuni inaonesha kuwa vyama vingine tofauti na Chadema , CUF na CCM, haviwezi kusimamisha wagombea kwa sababu havikidhi kigezo cha kanuni ya 12 za Kudumu za Bunge.

MTANZANIA ilipomtafuta Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge, Owen Mwandumbya, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema hakuna mabadiliko kwani kanuni ndizo zinazoelekeza mgawanyo huo.

“Ni kweli na ukiangalia kanuni zinasema mgawanyo wa wabunge unategemea na idadi ya uwepo wa wawakilishi  bungeni kutoka vyama husika bungeni. Hivyo hakuna mabadiliko na hapa ninaandaa taarifa ambayo tutaitoa kwa umma,” alisema Mwandumbya.

Hata hivyo baadhi ya vyama ikiwemo CUF kimewasilisha majina ya wagombea kwa Katibu wa Bunge ambao wanatoka kila upande hasa wa Lipumba na Maalim Seif.

Kwa siku ya tatu sasa kampeni za kuwania nafasi hizo zimepamba moto ambapo kwa upande wa CCM walioteuliwa kuwania nafasi hizo ni 12.

Wanawake Tanzania Bara ni Zainabu Kawawa, Happiness Lugiko, Fancy Nkuhi na Happiness Mgalula na kwa upande wa wanaume Dk. Ngwaru Maghembe, Adam Kimbisa, Anamringi Macha na Makongoro Nyerere

Kwa upande wa Zanzibar wanawake ni Maryam Ussi Yahya na Rabia Abdallah Hamid huku wanaume ni Abdallah Hasnu Makame na Mohammed Yussuf Nuh.

Chadema walioteuliwa ni Lawrance Masha  na Ezekiah Wenje huku upande wa CUF Maalim aliyeteuliwa ni Wakili Twaha Taslima na upande wa CUF Lipumba ni Mohamed Habib Mnyaa, Thomas Malima na Sonia Magogo.

Chama cya ACT-Wazalendo kilikuwa kimemteua Mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo kuwania nafasi hiyo jambo ambalo sasa haweza kuomba kura kwa mujibu wa uamuzi wa Kamati ya Kanuni ya Bunge.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles