29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Zana haramu za uvuvi zaendelea kuteketezwa Muleba

Na Renatha Kipaka, Muleba

Zana haramu za uvuvi, zenye thamani ya Sh bilioni 1.25 kutoka katika Kata za mwambao wa Ziwa Victoria, Ziwa Burigi na Visiwani, zimeteketezwa eneo la mwalo wa Katunguru, uliopo kijiji Katunguru, kata ya Gwanseli, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Akizungumza leo Juni 23, 2022 kabla ya zoezi la uteketezaji wa zana hizo, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila ameendelea  kuwasisitiza viongozi na wananchi kuwa mstari wa mbele kupambana kutokomeza uvuvi haramu ili kuwa na uvuvi endelevu wenye manufaa katika Wilaya ya Muleba.

“Msikubali kamwe wavuvi haramu wakaendelea kuvua na timba na makokoro zana ambazo zinavua mpaka samaki wachanga tusipopambana na kuhakikisha tunawabaini wavuvi haramu na kuwachukulia hatua tutabaki na maji matupu bila samaki” amesema Nguvila.

Aidha, amewataka wananchi kulinda ziwa na raslimali zake kama wanavyolinda mboni za macho yao kwa manufaa yao na vizazi vijavyo ambapo amewaeleza kuwa uvuvi haramu ukitokomezwa wataweza kukua kiuchumi na biashara ya samaki itakua zaidi.

“Mfanyabiashara yeyote anayewaletea nyavu haramu huyo ni muuaji mkimuona mfanyabiashara anayewaletea nyavu haramu mtoe taarifa haraka ili achukuliwe hatua za kisheria” ameendelea kueleza Nguvila.

Sambamba na hayo amewasihi wananchi kuanzisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na kuwaeleza kuwa Serikali tayari imetoa kipaumbele kwenye bajeti inayokuja kuanzisha ufugaji wa samaki kwa vizimba hivyo kuwafanya wavuvi kufuga samaki na kuendela kunufaika na uvuvi halali.

Akisoma taarifa fupi kabla ya uteketezaji wa nyavu hizo Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba, Wirfred Tibendelana amesema zoezi hili ni mwendelezo wa kutokomeza uvuvi haramu kwa wavuvi wanaotumia zana haramu kwa kuzingatia Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 zilizofanyiwa marekebisho mwaka 2020 ambazo zinamtaka mvuvi kutotumia zana haramu ikiwemo nyavu za chini ya inchi 6 katika shughuli za uvuvi.

Agripina Joas Matungwa, mkazi wa Katunguru ameonyesha kuchukizwa na uvuvi haramu na kueleza kuwa kutokana na uvuvi haramu samaki hawapatikani kama zamani hivyo ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa na kuhakikisha uvuvi haramu unatokomezwa katika Wilaya ya Muleba.

Uchomaji wa zana hizi ni mwendelezo wa zoezi la kupambana na uvuvi haramu ambapo zana haramu zilizochomwa ni pamoja na kokoro 44, nyavu chini ya inchi 6 nyavu 11, timba 356 katuli 2 na Kamba za  kuvuta kokoro zenye urefu wa mita 810 ikiwa watuhumiwa waliokamatwa ni wavuvi 34.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles