29.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

ZAHERA, NYOTA WAKE MAJARIBUNI

MOHAMED KASSARA – DAR ES SALAAM

KIKOSI cha Yanga leo kinatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi, kucheza mchezo wa kirafiki na Polisi Tanzania, ukiwa ni mtihani mwingine wa benchi la ufundi na nyota wa timu hiyo kuelekea mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Katika mechi ya kwanza dhidi ya Rollers iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita, Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 hivyo kuhitajika kufanya kazi ya ziada ugenini wiki ijayo ili kushinda au kupata sare ya zaidi ya mabao 2-2 iweze kusonga mbele.

Kwa kufahamu hilo, kikosi cha Yanga chini ya Kocha Mkuu wake, Mwinyi Zahera, kimeweka kambi mjini Moshi kuwawinda Rollers ambapo kitacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania leo kabla ya kuwavaa AFC Leopards ya Kenya kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha keshokutwa.

Mchezo wa leo ni pendekezo la Zahera baada ya kuona kikosi chake bado kina walakini, hasa kwenye eneo la ushambuliaji.

Hali hiyo inatokana na Zahera kuchelewa kujiunga na kikosi hicho kambini Morogoro, akitua nchini ikiwa ni wiki moja na nusu kabla ya mchezo na Rollers, akitokea mapumzikoni Ufaransa, alikokwenda baada ya kumaliza majukumu ya timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) katika fainali za Afcon 2019 nchini Misri.

Kocha huyo alianza kubaini kasoro kwenye kikosi chake katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Kariobang Sharks ya Kenya uliochezwa Agosti 4, mwaka huu na kumalizika kwa sare 1-1.

Baada ya kuona kasoro hizo, Zahera alihitaji michezo mingine miwili ya kirafiki ambayo timu hiyo ilicheza dhidi ya timu za Malindi FC na Mlandege zote za Zanzibar ili kuhakikisha anazishughulikia haraka kabla ya kuivaa Rollers.

Licha ya Yanga kushinda mchezo mmoja na mwingine kupata sare, tatizo la umaliziaji liliendelea kuitesa timu hiyo dhidi ya Rollesrs ambapo pamoja na kutengeneza nafasi nyingi, ilishindwa kuzitumia.

Juu ya mchezo wao wa leo dhidi ya Polisi Tanzania, Zahera alisema atautumia kutengeneza muunganiko mzuri wa washambuliaji wake, Juma Balinya, Sadney Urikhob na Patrick Sibomana.

Mkongoman huyo anajua kazi nzito iliyopo mbele yake ya kuhakikisha analiongoza kikosi chake kufunga mabao ya kutosha ili kuiwezesha kupata ushindi ugenini utakaowapeleka hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika kuhakikisha anatimiza lengo hilo, Zahera tayari amenasa video za wapinzani wao hao ambazo ataanza kuzifanyia kazi katika mchezo huo wa kirafiki.

Zahera hataki masihara kabisa, kwani amecharukia wachezaji ambao walikuwa wanaleta utani kwenye mazoezi, akiwataka kuongeza umakini katika mazoezi hayo ili kushika kwa haraka mbinu anazowapa ili ziwakae kichwani kwa ajili mchezo dhidi Rollers.

Akizungumzia na MTANZANIA jana, Zahera alisema wanaendelea kuwasoma wapinzani wao na kufanyia kazi katika michezo hiyo ya kirafiki.

“Kesho tutakuwa mechi ya kwanza kirafiki, lakini kikubwa tunaangalia namna gani tutacheza Botswana na kuibuka na ushindi, tumeangalia video ya Township mara ya kwanza na tunaendelea kuangalia kuona ni sehemu gani tunatakiwa kurekebisha.

 “Nimepanga kumaliza tatizo la ushambuliaji mapema iwezekanavyo kabla ya mchezo huo, michezo hii miwili ya kirafiki itatupa picha halisi ya namna tutakavyoza huko na kupata ushindi ugenini,” alisema Zahera.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles