24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yajipanga kuanza kuhesabu mataji

THERESIA GASPER – DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba imejipanga kuanza kuhesabu mataji katika mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, unaotarajiwa kuchezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wekundu wa Msimbazi hao ndio wanaoshikilia ngao hiyo waliyoitwaa msimu uliopita baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Kikosi cha Simba kiliingia kambi rasmi jana Dar es Salaam na kuendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana, jijini ili kujiweka fiti kabla ya kuvaana na Wanalambalamba hao.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, alisema wachezaji wote wanaonekana kuwa na morali ya juu kuelekea mchezo huo.

“Tumeendelea na mazoezi leo (jana) asubuhi hapa Gymkhana na tunaingia kambi moja kwa moja kujiandaa na mchezo huo, ambao utakuwa na ushindani mkubwa kwani kila mmoja anahitaji kushinda,” alisema.

Alisema wachezaji wote waliokuwa kwenye programu ya Kocha Mkuu wao, Patrick Aussems, wapo vizuri.

Rweyemamu alisema wanahitaji kuanza mahesabu ya ligi vizuri kwani mchezo huo utazidi kuwapa mwanga wa kufanya vizuri msimu unaokuja.

Kocha wao Aussems aliweka wazi pia mchezo huo atatumia kama maandalizi ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo, inayotarajiwa kuchezwa Agosti 23, mwaka huu, Uwanja wa Taifa.

Wachezaji ambao wataukosa mchezo huo ni Aishi Manula, Ibrahim Ajib na Wilker Henrique Da Silva hadi hapo hali zao zitakapoimarika.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, wamejipanga kufanya kweli msimu ujao ikiwa pamoja na kutetea taji lao kwa mara ya tatu mfululizo, lakini pia kufika mbali zaidi Ligi ya Mabingwa Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles