23.2 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

YANGA YAPEWA SIRI KUIUA WELAYTA


NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM    |    

YANGA imepewa mbinu zote za kuing’oa Welayta Dicha ya Ethiopia, katika mchezo wa mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Droo ya michuano hiyo ilichezeshwa juzi makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) yaliyoko jijini Cairo, Misri.

Yanga itaivaa Welayta na mchezo wa kwanza utachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Aprili 6 na 8, kabla ya ya ule wa marudiano kufanyika mjini Wolaita Sodo, kati ya Aprili 17 na 18, mwaka huu.

Yanga iliangukia Kombe la Shirikisho baada ya kuondolewa Ligi ya Mabingwa Afrika, ikichapwa jumla la mabao 2-1 na Township Rollers ya Botswana.

Vigogo hao wa Jangwani walitunguliwa mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya kulazimishwa suluhu jijini Gaborone, Botswana.
Lakini Welayta Dicha imefika hatua hiyo baada ya kuiondosha Zamalek ya Misri kwa penalti 4-3, ikianza kushinda mabao 2-1 nyumbani, kabla ya kuchapwa 2-1 ugenini.

Welayta Dicha wao walianza safari yao ya Kombe la Shirikisho kwa kuimwaga Zimamoto ya Zanzibar jumla ya mabao 2-1, ikilazimisha sare bao 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Ethiopia.
Mara ya mwisho Yanga kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shrikisho Afrika ilikuwa mwaka 2016, baada ya kutimuliwa na Al Ahly ya Misri raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga ilifuzu hatua hiyo ya makundi baada ya kuiondosha mashindanoni Sagrada Esperanca ya Angola jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, kabla ya kufungwa bao 1-0 Angola.

Katika hatua ya makundi, Yanga ilipangwa kundi A pamoja na timu za TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mo Bejaia ya Algeria na Medeama SC ya Ghana.
Katika kundi hilo, Yanga ilicheza mechi sita na kuambulia pointi nne, baada ya kushinda mechi moja tu dhidi ya Mo Bejaia 1-0 na sare ya 1-1 dhidi ya Medeama, huku ikipoteza mechi nyingine nne zilizosalia.

Iliangukia hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho mwaka jana, lakini ilishindwa kufuzu hatua ya makundi, baada ya kutolewa na MC Alger ya Algeria, ilipolazwa jumla ya mabao 4-1, ikishinda 1-0, Uwanja wa Taifa kabla ya kuchapwa mabao 4-0 jijini Algiers.

Kocha wa Zimamoto anena

Kocha Abdoulghan Msoma ambaye aliiongoza Zimamoto kuivaa Welayta na kuondolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho, ameliambia MTANZANIA jana kuwa Yanga ina nafasi kubwa ya kuwang’oa wapinzani wao kutokana na kuwa na safu bora ya ushambuliaji.

“Yanga wasiwe na wasiwasi, Dicha ni timu ya kawaida na inafungika, safu yao ya ulinzi haina maelewano mazuri, pia wadhaifu katika kucheza mipira ya krosi, Yanga kutokana na ubora wa safu ya ushambuliaji, naamini watafanikiwa kupata matokeo.

“Chamsingi Yanga wawe macho na nyota wao, Arafat Djako, huyu ndiye mchezaji tegemeo kwenye kikosi chao, anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, anavaa jezi namba 10 mgongoni,” alisema Msoma na kuongeza.

“Pia inatakiwa kuwahi mapema Ethiopia katika mchezo wa marudiano ili kuzoea hali ya hewa ya kule, wenzetu wako juu mita 600 kutoka usawa wa bahari, hali ya hewa ya kule ni tofauti na Dar es Salaam au Zanzibar, kama wanataka kufanikiwa wawahi siku nne kabla ya mchezo, vinginevyo waweke kambi Arusha, kwa vile hali ya hewa ya kule inafanana na kwao,” alisema Msoma.

Yanga yaanza mawindo

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Hussein Nyika, alisema kamati yake inatarajia kuwa na kikao kizito leo kwa ajili ya kupanga mikakati ya kushinda mchezo huo.

Alisema baada ya kumjua mpinzani wao, sasa wanakwenda kukaa na kocha George Lwandamina, kujadili mikakati ya ushindi.

“Kamati, Katibu Mkuu na benchi la ufundi, leo tutakuwa na kikao kitakacholenga kupanga mikakati ya kuhakikisha tunashinda mchezo huo, ilikuwa tukutane jana ikashindikana, hatutakuwa na muda wa kupoteza, uongozi unaingia msituni kuweka mipango madhubuti ya kufuzu hatua ya makundi.

“Tutaanza maandalizi mapema, tayari tumepenyezewa fununu za wapinzani wetu ambazo zitatusaidia hata tukapotuma mtu wa kwenda kufuatilia nyendo zao atakuwa anajua afuatilie nini, tumejipanga kupambana kwa ajili ya kulinda heshima ya nchi ukizingatia sisi pekee ndio tumebaki tukipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa,” alisema Nyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,244FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles