28.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 19, 2022

Yanga yanoga, shooting yaiangamiza Mwadui FC

Na MASYNENE DAMIAN

-MWANZA

KINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, imevuna pointi tatu nyingine dhidi ya Alliance FC, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Bao pekee la ushindi la Yanga lilifungwa na Amisi Tambwe dakika ya 75.

Ushindi huo unaifanya Yanga kujizatiti kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, baada ya kufikisha pointi 64, kupitia michezo 26, ikishinda 20, sare nne na kuchapwa mara mbili.

Mchezo huo ulikuwa na vibweka kadhaa nje ya uwanja, ikiwemo mashabiki wengi kushindwa kuushuhudia kutokana na kukosa tiketi, sababu kuu ikiwa ni mfumo wa kielektroniki uliotumika katika kuchapa.

Ilibainika kuwa mfumo huo wa kielektroniki uliwezesha kuchapwa tiketi 11,000 pekee, wakati uwanja huo una uwezo wa kuingiza watazamaji 30,000.

Hatua hiyo iliwafanya viongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), kulazimika kutafuta tiketi za vishina ili kumaliza kadhia hiyo.

Dakika ya tano tu ya mchezo, mwamuzi Shomari Lawi, aliizawadia Yanga penalti, baada ya mshambuliaji, Heritier Makambo, kuangushwa eneo la hatari na nahodha wa Alliance, Siraji Juma.

Hata hivyo, Makambo alishindwa kuiandikia Yanga bao la kuongoza baada ya mkwaju wake wa penalti kupanguliwa na kipa wa Alliance, John Mwanda, kabla ya kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Dakika ya 21, Mkwaju wa Mapinduzi Balama, aliyepokea pande la kichwa la Bigirimana Blase, ulitoka nje ya lango la Yanga.

Dakika ya 25, Dickson Ambundo wa Alliance, aliipangua ngome ya Yanga, lakini mkwaju mkali ulipanguliwa na kipa, Klaus Kindoki na kuzaa kona ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Dakika ya 29, Blaise alipoteza nafasi ya kuiandikia timu yake bao, baada ya kushindwa kuunganisha vema mpira wa kona uliochongwa na Ambundo.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika kwa timu hizo kwenda mapumziko nyavu za kila moja ikiwa salama.

Kwa ujumla kipindi cha kwanza, timu hizo zilishambuliana kwa zamu, lakini  umakini mdogo wa safu ya ushambuliaji ya kila upande ulisababisha kukosekana kwa mabao.

Dakika ya 49, Kindoki, alifanya kazi nzuri baada ya kupangua kiki ya Ambundo kabla ya mpira kumfikia Blaise ambaye naye alipaisha.

Dakika ya 58, Kocha wa Alliance, Malale Hamsini, alifanya mabadiliko, alimtoa Hussein Javu na kumwingiza Michael Chinedu, kabla ya kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, kumtoa Mrisho Ngassa na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Issa na Haruna Moshi ambaye nafasi yake ilizibwa na Amisi Tambwe.

Dakika ya 63, Blaise alilimwa kadi ya njano baada ya kupinga maamuzi ya mwamuzi ambaye alikataa bao alilofunga kwa madai kwamba alikuwa ameotea.

Dakika ya 75, Tambwe aliiandikia Yanga bao la kuongoza kwa shuti kali, baada ya kutengewa mpira na Makambo.

Katika kutafuta namna ya kuchomoa  bao, dakika ya 81, Alliance ilifanya mabadiliko, alitoka Sameer Vicent na kuingia Richard John, kabla ya Yanga kufanya mabadiliko, ambapo alitoka Deus Kaseke na kuingia Said Juma.

Dakika ya 86, Mohamed Issa, alilimwa kadi ya njano, baada ya kumchezea rafu Juma Nyangi wa Alliance.

Alliance ilizidisha mashambulizi wakati huo kwa lengo la kutaka kuchomoa, lakini washambuliaji wake, Blaise, Ambundo na Chenedu, walikosa maarifa ya kuukwamisha mpira kimiani.

Dakika ya 90, beki wa Alliance, Wema Sadoki, alilimwa kadi ya njano, baada ya kumsukuma, Feisal Salumu. 

Hadi kipenga cha mwamuzi Lawi kinasikika kuashiria kumalizika kwa pambano hilo, Yanga ilitoka kifua mbele  kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji.

Katika michezo mingine, Ruvu Shooting iliutumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-2 dhidi ya Mwadui FC, Uwanja wa Mabatini, Pwani.

JKT Tanzania ilitakata nyumbani Uwanja wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo, Dar es Salaam, baada ya kuitungua Coastal Union bao 1-0, wakati KMC ililazimishwa suluhu na wageni wao Biashara United Uwanja wa Uhuru.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,312FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles