29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Yametimia

Pg 1*Kangi, Mwambalaswa, Murad kortini kwa rushwa

*CCM yaja juu, yatangaza kuwachukulia hatua

 

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

HATIMAE yametimia. Hii ni baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwapandisha kizimbani wabunge watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh milioni 30.

Kufikishwa kwa wabunge hao mahakamani, kulivuta hisia za wananchi ambao walifurika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kushuhudia tukio hilo.

Wabunge hao walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Maghela Ndimbo.

Ndimbo aliwataja wabunge hao kuwa ni  Mbunge wa Mvomero, Ahmed Saddiq Murad (53), Mbunge wa Mwibara,  Kangi Lugola (54) na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa, ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Walipofikishwa mahakamani, washitakiwa hao walionekana kuwa ni wenye furaha, ambapo muda mwingi walikuwa wakicheka sana wakiwa katika benchi la mahakama wakisubiri hakimu aingie wasomewe mashtaka yanayowakabili.

Ndimbo alidai kwamba, washtakiwa hao walitenda kosa hilo Machi 15, mwaka huu kati ya saa 20:00 na 22:00 usiku katika Hoteli ya GoldenTulip, iliyopo Masaki Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alidai washtakiwa wakiwa kama wajumbe wa Kamati ya Bunge ya LAAC waliomba rushwa ya  Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Mbwana Magotta.

Wabunge hao waliomba rushwa hiyo ili watoe upendeleo chanya  kuhusiana na taarifa ya fedha ya wilaya hiyo ya mwaka wa fedha 2015/16.

Baada ya kusomewa, washtakiwa walikana shitaka, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo waliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Simba, alikubali kuahirisha kesi hiyo na kuwapa washtakiwa masharti ya dhamana kwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana ya Sh milioni tano.

Washtakiwa walitimiza masharti ya dhamana wakaachiwa huru, kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 14 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

 

Wengine kupelekwa

Taarifa za ndani kutoka Takukuru, zinaeleza kwamba watawafikisha wabunge wengine mahakamani hapo kwa mujubu wa sheria.

“Hii ni awamu ya kwanza tumeanza kuwafikisha hapa mahakamani lakini tutaendelea kuwaleta wengine kati ya kesho (leo) na wiki ijayo ili kuweza kulinda heshima ya Taifa letu,” alisema mmoja wa maofisa wa juu wa Takukuru.

CCM yaibuka

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeibuka kwa mara ya kwanza tangu lilipoibuka sakata la rushwa kwa wabunge wake, ambapo kimesema hakitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu wabunge wake wote watakaobainika na vitendo vya rushwa.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa CCM kwa vyombo vya habari jana, Christopher ole Sendeka, ilieleza kwamba chama hicho kinasikitishwa na tuhuma hizo hasa pale zinapowahusu wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi.

“CCM inaunga mkono jitihada za vyombo vya dola katika kutafuta ukweli wa tuhuma hizo. Lazima ifahamike vitendo vya rushwa havikubaliki kwa namna yoyote kwani vina madhara makubwa kwa Taifa.

“CCM inavishauri vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina na kuwachukulia  hatua stahiki wabunge wote watakaobainika kuhusika na vitendo vya rushwa,” alisema ole Sendeka katika taarifa yake.

Sakata lilivyoanza

Baada ya gazeti hili kuripoti hatua ya baadhi ya wabunge kuomba rushwa katika taasisi za Serikali, Machi 22, mwaka huu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alifanya mabadiliko ya baadhi ya wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge huku akiwaondoa wenyeviti na makamu wenyeviti watano katika kamati walizokuwa wakiziongoza.

Katika mabadiliko hayo yaliyowagusa jumla ya wabunge 27, Spika Ndugai, alitoa maelekezo ya kujazwa kwa nafasi zilizoachwa wazi za wenyeviti na makamu wenyeviti walioguswa na panga pangua hiyo na kusititiza utekelezaji wa maagizo yake kuanza mara moja.

Taarifa ya Ofisi ya Bunge, Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ya Umma, ilieleza kwamba uamuzi wa  Spika umezingatia mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuundwa kwa Kamati za Bunge, Januari mwaka huu.

Taarifa hiyo ilieleza kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa Spika ya kuteua wabunge na kuunda kamati za Bunge, alizingatia kanuni ya 116 (3) ya kanuni za kudumu za Bunge kuwaondoa viongozi watano wa kamati na kwamba kamati ambazo zitaathirika na uamuzi wake zitapaswa kufanya uchaguzi wa viongozi walioondolewa kwa mujibu wa kanuni ya 116 (10).

Wenyeviti walioguswa la rungu la mabadiliko yaliyofanywa na Spika Ndugai ni Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini aliyehamishiwa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji (PIC), aliyehamishiwa kamati ya Katiba na Sheria.

Mwingine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa (CCM),  ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ambapo amejikuta akihamishiwa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Makamu wenyeviti walioondolewa kwenye kamati zao ni Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Sambamba na hao, wabunge wengine 22 nao wamehamishwa kutoka kamati walizokuwapo na kwenda katika kamati nyingine.

Taarifa za Bunge ambazo gazeti hili ilizipata zilieleza kuwa mabadiliko hayo yamelenga kuwaondoa waliokuwa wakilalamikiwa kuhusu mienendo yao ya kikazi kwenye kamati walizokuwa huku wengine wakihamishwa kwa ajili ya kwenda kujenga taswira mpya ya kamati zinazonyooshewa vidole.

Panga pangua hiyo ya kamati za Bunge iliyofanywa na Spika Ndugai, imekuja siku mbili baada ya gazeti hili kuwa la kwanza kuripoti kuhusu tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi wabunge wakiwemo viongozi wa kamati pamoja na uwezekano wa kuwepo kwa mabadiliko ya wajumbe na viongozi wa kamati hizo yaliyofanyika jana.

Gazeti hili liliripoti kuwa, ripoti ya uchunguzi wa mwenendo wa wabunge iliyofikishwa mezani kwa Spika, iliwatuhumu viongozi wa kamati ambao ni Mlata, Ndassa, Dk. Mwanjelwa, Dk. Chegeni na Lugola pamoja na baadhi ya wabunge kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Kutokana na hali hiyo Spika Ndugai, alilazimika kufanya kikao na wabunge hao ambapo pamoja na mambo mengine aliwaeleza jinsi majina yao yanavyohusishwa na tuhuma hizo na kuwataka kuwafikishia ujumbe wajumbe wa kamati zao kwa kuwataka kujisahihisha kutokana na  baadhi ya wajumbe wa kamati hizo kudaiwa kutumia jina la Bunge vibaya.

Gazeti la MTANZANIA lilikariri taarifa za kibunge zilizoeleza kuwa taasisi zilizofikiwa na wabunge wanaotuhumiwa kuombwa rushwa kuwa ni Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Hata hivyo, walipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, Mlata, Dk. Mwanjelwa na Lugola walikanusha kuhusika nazo huku wakieleza kuwa alichofanya Spika baada ya kuwaita ofisini kwake ni kuwapa maelekezo ya kikazi na kuwatuma kufikisha ujumbe wa kujisahihisha kwa wajumbe wa kamati zao.

Badwel

Juni 2, mwaka 2012,  Takukuru ilimpandisha kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mbunge wa Bahi, Omar Ahmed Badwel (CCM),  kwa tuhuma za kudai rushwa ya Sh milioni 8 na kupokea kianzio cha Sh milioni moja.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Faisal Kahamba, Mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Janeth Machullia na Ben Lincolni walisema mshtakiwa anakabiliwa na makosa mawili ya rushwa, mosi ikiwa ni kosa la rushwa ambalo ni kinyume cha kifungu cha 15 (1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana  na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Imeelezwa kuwa, mnamo Mei 30,  2012, mtuhumiwa alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga, Pwani, Sipora Liana ampe kiasi hicho cha fedha ili aweze kupitisha ripoti ya taarifa ya fedha ya mwaka 2011/2012 ya halmashauri hiyo.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa na maofisa wa TAKUKURU tarehe tajwa ya kosa kutendeka, saa 9 alasiri, katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam, wakati anapokea rushwa kutoka kwa maofisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles