31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

Magufuli amtumbua Mnikulu

JohnMagufuliNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli, amefanya mabadiliko mengine Ikulu jijini Dar es Salaam kwa kumwondoa aliyekuwa Mnikulu, Jumaa Bwando.

Vyanzo vya habari kutoka Ofisi ya Rais vimesema Bwando, aliondolewa katika wadhifa huo Machi 14, 2015, ambapo kwa sasa nafasi hiyo inakaimiwa na mmoja wa maofisa wa juu wa Ikulu.

Julai 10 mwaka jana, Bwando aliteuliwa kushika wadhifa huo na Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, kuchukua nafasi ya Shaban Gurumo, aliyeng’olewa baada ya kukiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma inayokataza kiongozi wa serikali kupokea zawadi zaidi ya zawadi ndogondogo na ukarimu wa kawaida.

Kazi ya Mnikulu ni kusimamia majengo yote ya Ikulu kwa maana ya shughuli za utawala. Yeye ndiye anayehusika na usafi, samani na mapambo yote katika ofisi hiyo kuu ya nchi.

Ni mtu anayeweza kuamua mwonekano wa Ikulu uonekanaje, hata kupanga na kuamua aina ya nguo, mashuka, mapazia yanayopaswa kutumiwa na Rais. Kwa majukumu husika anapaswa amjue vizuri Rais.

Hatua hiyo ya Rais Magufuli ni mwendelezo wa mabadiliko aliyoanza kuyafanya Ikulu siku chache baada ya kuingia madarakani.

Tayari amezifumua na kuziunda upya baadhi ya ofisi za Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam pamoja na kuwaondoa baadhi ya watumishi ambao hawana ulazima katika mfumo wa utumishi wa Ikulu.

Rais Magufuli alianza kufanya ukaguzi wa ofisi moja baada ya nyingine zilizopo Ikulu, huku akitaka maelezo ya kina kuhusu shughuli zake na aina ya watendaji waliopo.

Katika ukaguzi huo, Rais Magufuli aliamuru kufungwa mara moja kwa baadhi ya ofisi alizobaini kuwa hazina tija na kwamba zina watumishi ambao ni mizigo.

Baadhi ya ofisi zinazodaiwa kufungwa ni pamoja na iliyokuwa ikishughulikia chakula cha Rais na ile iliyokuwa ikijihusisha na kupokea wageni binafsi wa Rais.

Wakati akifanya mabadiliko hayo, Ofisa mmoja wa Ikulu alinukuliwa na gazeti hili akisema. “Rais Magufuli alipoingia tu Ikulu alifanya ziara ya kukagua ofisi zote zilizopo Ikulu, alitaka kujua utendaji kazi wa ofisi hizo, lakini alipofika kwenye kitengo maalumu cha lishe ya Rais, alisema haoni umuhimu wa kuwepo kwa ofisi hiyo kwa sababu suala la lishe yake siku zote linasimamiwa na mkewe Janeth.

“Akaamuru ifungwe na watumishi wake warejeshwe walikotoka. Ofisi nyingine aliyoamuru ifungwe ni kupokea wageni binafsi wa Rais. Alisema haoni tija ya kuwepo kwa ofisi hiyo kwa sababu mgeni anatakiwa kufika Ikulu baada ya kutoa taarifa, nayo aliamuru ifungwe,” alisema ofisa huyo.

Taarifa zilisema aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Lishe Ikulu alirudishwa katika ajira yake ya awali Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, huku watumishi wengine wakipelekwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

MTANZANIA ilipomtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Gerson Msigwa, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alijibu kwa kifupi kuwa

“Nalifanyika kazi swali lako kisha nitakupatia ufafanuzi baada ya muda,” alisema Msigwa, ambapo baada  ya muda alipopigiwa simu hakupokea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles