WINGU ZITO MAUAJI RUFIJI

0
958

NA VERONICA ROMWALD

-DAR ES SALAAM

WINGU la mauaji limezidi kutanda katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Taarifa zinasema  kiongozi mwingine wa CCM ambaye ni mjumbe wa shina ameuawa katika Kijiji cha Ikwiriri na watu wasiojulikana na mwili wake kutekelezwa eneo la Daraja tatu wilayani humo.

Akizungumza na MTANZANIA jana ndugu wa marehemu, Isika Hamis alimtaja ndugu yake aliyeuawa kuwa ni Masunga Mayuka.

“Nilipokea taarifa za tukio hilo leo (jana) asubuhi, wakati huo nilikuwa nyumbani kwangu.

“Mdogo wangu ambaye anaishi Ikwiriri ndiye wa kwanza kunijulisha juu ya tukio hilo, alinipigia simu,” alisema Isika.

Alisema kwa mujibu maelezo ya mdogo wake huyo, ndugu yao aliuawa akiwa njiani kwenda  msikitini  kufanya ibada.

“Mdogo wangu alinieleza, inadaiwa Mayuka alikutana na wauwaji njiani ambao walimpiga risasi na baada ya kitendo hicho walitokomea kusikojulikana,” alisema.

Alisema saa chache baada ya kuzungumza na mdogo wake huyo alipokea tena simu ya ndugu yake mwingine ambaye naye alimjulisha jambo hilo la kusikitisha.

“Nilielezwa kwamba ndugu yangu aliuawa huku akiwa anajitetea mbele ya watu hao wasimdhuru, sasa tupo msibani tunajiandaa kwa maziko,” alisema Isika.

Akizungumza na MTANZANIA, Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, alisema  hajapokea taarifa hizo na kuahidi kuzifuatilia.

“Sina hizo taarifa, sijazipokea labda na mimi nizifuatilie hivi sasa,” alisema.

Tangu mauaji hayo yatokee, inadaiwa   watu takriban 38 wamekwisha  kuuawa.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro, jana aliandika katika ukursa wake wa Facebook kwamba wenyeviti wao wawili wa serikali za vijiji wameuawa wilayani Rufiji.

Aliwataja waliouawa kuwa ni Kazi Mtoteke wa Mtaa wa Ikwiriri Kati na Jumanne Kilumike wa Mtaa wa Ikwiriri (wilayani Rufiji) ambao walitekwa na watu waojulikana.

“Tofauti na wale wauaji wa polisi, watekaji wa sasa wanakuja na magari hadi jirani na nyumba ya mtekwaji kisha wanaingia nyumbani kwake wakiwa wamejifunika nyuso na wakishampata kiongozi waliyekuwa wanamsaka wanaondoka naye.

“Hii ni oparesheni ya vyombo vya dola na mimi on the truth I will speak it as it is maana unaishi kwenye nchi ambayo uongo na unafiki are the orders of the day.

“Wakishaondoka eneo la mji wa mtekwaji wanaingia kwenye gari walilokuja nalo na kuondoka,” alisema Mtatiro katika andiko lake.

Alisema siku sita zilizopita chama chao kilianza kuripoti masuala ya Rufiji, Kibiti na Mkuranga lakini wapo watu walianza kuwakejeli bila sababu.

“Sisi kila tunachozungumza ndiyo hali halisi. Kinachoendelea kwenye wilaya hizo hivi sasa siyo wale wauaji walioleta madhara makubwa.

“Kwa sasa matukio ya utekwaji wa viongozi na uumizaji wa raia yanafanywa na vyombo vya dola, na tuna ushahidi huo. Hivi sasa idadi ya viongozi 12 wa CUF hawajulikani walipo, wanafuatwa majumbani na kutekwa,” alisema.

Kutokana na mfululizo wa mauaji mkoani humo, Rais Dk. John Magufuli hivi karibuni alifanya mabadiliko ndani ya Jeshi la Polisi ambako alimuondoa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo (IGP) Ernest Mangu.

Badala yake nafasi hiyo aliteuliwa Simon Sirro ambaye siku chache baada ya uteuzi huo, alitangaza mikakati ya kuhakikisha anakomesha mauaji hayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here