24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

DUDE LA IPTL LANG’OA KIGOGO

Na ELIZABETH HOMBO

-DAR ES SALAAM

DUDE hatari la IPTL. Ndivyo unavyoweza kusema wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi.

Hatua hiyo imschukuliwa siku chache baada Ewura kutangaza kuwa ingeanza kupokea maoni na mapingamizi ya wadau mbalimbali kuhusu kuongezewa muda wa leseni kwa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Taarifa ya Waziri Mkuu iliyotolewa usiku wa kuamkia jana saa 7:08 usiku kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kusimamishwa kwa kigogo huyo ingawa haikueleza sababu za kuchukuliwa hatua hiyo.

 “Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi  kuanzia leo (jana) Juni 11, 2017,” ilieleza taarifa hiyo.

Wiki iliyopita Ewura ilitoa tangazo ikieleza ilikuwa imepokea maombi ya IPTL ya kutaka iongezewe muda leseni yake ya kuuza umeme nchini.

Wadau mbalimbali wakiwamo wanasiasa, walipinga hatua hiyo kutokana na jinsi   IPTL ilivyokwisha kuibua mjadala mzito  nchini kiasi cha kusababisha baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali ya Awamu ya Nne kuwajibishwa kwa tuhuma za kupokea mamilioni ya fedha kutoka kwa kampuni hiyo kinyume na sheria.

Kampuni ya IPTL imekuwa ikiiuzia umeme Tanesco huku utata wa bei ya umeme huo ukitawala  jambo lililosababisha Bunge la 10 kuazimia ifukuzwe nchini na kunyang’anywa mitambo.

EWURA YASIMAMISHA USIKU

Muda mfupi baada ya Waziri Mkuu kumsimamisha kazi Ngamlagosi, mamlaka hiyo ilitoa taarifa saa 8:02 usiku wa kuamkia jana ya kusimamisha mchakato wa kushughulikia maombi hayo ya IPTL ya kuongezewa leseni.

 “Ewura inasimamisha mchakato wa kushughulikia maombi ya leseni ya mwombaji ikiwa ni pamoja na upokeaji wa maoni/mapingamizi dhidi ya maombi hayo mpaka hapo yatakapotolewa maelekezo mengine,” ilieleza taarifa hiyo.  

Alipotafutwa, Kaimu Meneja Mawasiliano wa shirika hilo, Leila Muhaji, kujua kama hatua hiyo ya kusimamisha  mchakato wa  utoaji leseni kwa IPTL  utaathiri upatikanaji wa umeme alisema: “Hatua hiyo haitaathiri kwa namna yoyote ile kwa sababu umeme upo wa kutosha” .

ZITTO

Naye Mbunge Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema inawezekana mpango wa kuongeza muda wa leseni ya IPTL akawajibishwa mtu wa Ewura kwa kuwa ndiye aliyetoa tangazo hilo.

“Lakini huyo mtu wa Ewura anaweza kuwa ameshinikizwa, mimi naamini Rais kwa jinsi alivyo hawezi kuwa anahusika na haya matapeli.

“Lakini Rais mtumbuaji anakaaje miezi 20 kwenye kiti cha enzi bila kumaliza suala la IPTL ilhali kuna maazimio ya Bunge yanayopaswa kutekelezwa?

“Nawapa kazi ndogo Watanzania, watazame lile tangazo la Ewura kuhusu IPTL. Tazameni umiliki na wamiliki wa IPTL hivi sasa.

“Kuna hisa asilimia 16 kwa kampuni mbili zenye majina ya ujanja ujanja. Kina nani hao wamegawiwa hizo hisa tena wakati wa uongozi wa Rais John Magufuli?

 “Kwenye kesi ya Standard Chartered Bank dhidi ya Tanesco huko Mahakama ya ICSID ambako Tanesco wanatakiwa kulipa Sh bilioni 352 kwa benki hiyo, wanasheria wa Tanesco na wale wa PAP/IPTL wanashirikiana kwa karibu mno.

“Kwenye rufaa, Tanesco wametakiwa waweke fedha hizo kwanza kwenye akaunti ya benki ya nje kabla ya rufaa kusikilizwa.

“PAP/IPTL wanalinda ufisadi wao kwa kujifanya wanashirikiana na Tanesco kwenye kesi. Kwenye taarifa ya PAC kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow tuliweka wazi kuwa PAP/IPTL waliweka dhamana kuwa ikitokea madai yoyote yale dhidi ya Tanesco basi PAP/IPTL italipa.

“Kwa nini Serikali isitumie ile indemnity kuwataka PAP kulipa hizi fedha?  Kwa nini Serikali inayosema inapambana na ufisadi inawakumbatia mafisadi wa PAP/IPTL?

“Kwa nini Serikali iliyoonyesha ujasiri wa kupambana na Kampuni kubwa kama Acacia/Barrick inayumbishwa na matapeli hawa; tena tapeli mmoja tu Harbinder Singh Seth?

“Huko ICSID shirika letu la Tanesco kupitia wanasheria wake wamepeleka hoja kwamba maazimio ya Bunge kuhusu Tegeta Escrow hayana msingi wowote wa  sheria na kwamba Bunge linapiga porojo tu.

“Wanasheria hawa wameomba Ofisi ya Bunge iwape barua kuthibitisha kuwa uamuzi wa Bunge hauna msingi wowote na ni maoni tu yanaweza kudharauliwa na kutupiliwa mbali. Shirika la umma linalosimamiwa na Bunge linapeleka barua kwenye vyombo vya ubeberu kuwa Bunge ni porojo tupu?” aliuliza Zitto.

MBOWE ALIIBUA TENA

Mei 11 mwaka huu, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliihoji lini Serikali itatoa  majibu ya maazimio mbalimbali yaliyotolewa bungeni kutokana na muda kupita.

Mbowe aliyataja baadhi ya maazimio hayo kuwa ni ya Tokomeza, Escrow na IPTL pamoja na mabilioni ya Uswisi, kwamba muda mrefu umepita bila serikali kutoa majibu.

Kutokana na swali hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema wakati ukiwadia atatoa majibu ya maazimio mbalimbali yaliyotolewa na wabunge  hapo bungeni.

“Natambua vikao mbalimbali vilitoa maazimio yanayotaka serikali ilete maelezo kwa baadhi ya maeneo na mambo uchunguzi lakini mambo hayo yanahitaji muda ili kuleta maelezo hapa bungeni,” alisema Waziri Mkuu wakati akijibu swali la papo kwa hapo lililoulizwa na  Mbowe.

MITAMBO YA MAFUTA

Pamoja na   Serikali kuagiza kubadilishwa  mitambo yote ya umeme ibadilishwe   iweze kutumia gesi, Kampuni ya IPTL bado haijafanya hivyo kwa mujibu wa tangazo la Ewura.

  Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ilitakiwa kuipa IPTL   Sh bilioni 100   kuanza mchakato wa kubadili mitambo   iweze kutumia gesi.

Hata hivyo hatua hiyo ilipingwa na wananchi na hakuna fedha iliyotolewa na mitambo hiyo inaendelea kutumia mafuta hadi sasa,   umeme wake ukitajwa kuuzwa kwa gharama kubwa.

WADAU WAJIPANGA

Baada ya taarifa ya Ewura kuwapo mchakato kuhusu IPTL kupewa leseni, wadau mbalimbali walitangaza kupinga uamuzi huo huku wajipanga  kuhamasisha wananchi kuweka mapingamizi.

Hatua hiyo ni kama njia ya kupinga kampuni hiyo kupewa leseni kwa jinsi ilivyoibua mjadala mzito katika Bunge la 10 hasa kutokana na umiliki wake na namna ilivyouzwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles