RIPOTI YA PILI MAKINIKIA KUTIKISA TAIFA

0
785

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

WAKATI mjadala wa ripoti ya kwanza ya uchunguzi wa mchanga wa madini (makinikia) ukiwa bado mbichi, leo Rais Dk. John Magufuli anatarajiwa kupokea ripoti ya pili ya uchunguzi huo.

Katika ripoti ya kwanza iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli Mei 24 mwaka huu, kamati ilibaini kontena 277 za mchanga huo zilizokuwa Bandari ya Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi, zina dhahabu na madini mengine yenye thamani ya takriban  Sh trilioni 1.441.

Wakati kamati hiyo ikibaini hayo, taarifa za Wakala wa Serikali wa Ukaguzi Madini (TMAA) na nyingine za kusafirisha mchanga huo zilizokaguliwa na kamati, zinaonyesha mchanga huo una madini yenye thamani ya Sh bilioni 112.1.

Kwa sababu hiyo, Rais Magufuli alimwondoa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na viongozi waliokuwa wakiongoza  TMAA.

Ni kwa muktadha huo, macho na masikio ya wengi yamejielekeza kufuatilia ripoti ya pili na kutaka kusikia nani ataondoka safari hii na nani atakayebaki huku wengine wakiitazama ripoti hiyo ya pili kuwa itaibua mjadala mpya katika sekta ya madini nchini.

Wafuatiliaji wa mambo pia wanabashiri kwamba huenda ripoti hiyo ya pili ya uchunguzi, ikaibua mazito zaidi hususan kiwango cha fedha ambacho Serikali ama imekipata au kupoteza kupitia usafirishaji wa makinikia nje ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, taarifa ya kamati ya pili ya wachumi na wanasheria iliyofanya uchunguzi wa madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga wa madini yaliyopo katika maeneo mbalimbali   nchini, itakabidhiwa kwa Rais Magufuli leo.

“Tukio hili litarushwa hewani moja kwa moja (mubashara) kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya redio, televisheni, mitandao ya  jamii na tovuti rasmi ya Ikulu kuanzia saa 3:30 asubuhi.

“Wananchi wote mnakaribishwa kufuatilia matangazo hayo kupitia vyombo mbalimbali vya habari ama simu zenu za mikononi kwa kutembelea tovuti rasmi ya Ikulu,” ilisema taarifa hiyo.

Ikumbukwe kwamba Kampuni ya Acacia ambayo ndiyo wamiliki wa mgodi wa Bulyanhkulu iliyopo mkoani Shinyanga, ilipinga taarifa ya kwanza ikisema kamati hiyo haikutangaza madini yote yaliyokuwa katika makinikia.

“Hatukubaliani na matokeo ya tume ambayo inaeleza kuwa madini yaliyo katika mchanga katika makontena ambayo yamezuiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam yana thamani zaidi ya mara 10 ya kiwango tulichotangaza.

“Tuna imani na usahihi wa taarifa zetu ambazo zilikaguliwa na kutathiminiwa na SGS, ambayo ni moja ya kampuni kubwa  duniani za upimaji,”alisema Ofisa Msemaji wa Mkuu wa Acacia, Brad Gordon.

Wakati mjadala kuhusu ripoti ya kwanza ukiendelea, Mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Issa Shivji, aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema Serikali ilikosa njia ilipopitisha sheria ya madini mwaka 1998.

 “Tulikosea njia tulipopitisha sheria ya madini ya mwaka 1998 iliyofanya mikataba iwe na nguvu zaidi kuliko sheria, tukajifunga pingu. Nani wa kumlaumu,” alisema.

Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), Tundu Lissu, naye alipinga akisema amekuwa akihoji matatizo ya mikataba ya madini miongoni mwake ikiwamo Sheria ya Madini ya Mwaka 1998  ambayo Serikali iliipeleka bungeni kwa hati ya dharura na ikapitishwa ndani ya siku moja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here