Wiki tatu za mnyukano

0
811

GRACE SHITUNDU – DAR ES SALAAM

UNAWEZA kusema ni siku 21 au wiki tatu za kibarua kigumu kwa vyama vya siasa kuchanga karata zao sawasawa kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24.

Kuna kila dalili zinazoonyesha kuwa siku hizi zitakuwa za mshike mshike, kwani mikutano ya kampeni ya uchaguzi huo huenda ikatumiwa kuwa ni jukwaa la wanasiasa, hasa wa upinzani kutema nyongo zao baada ya mikutano ya hadhara kuzuiliwa kwa takribani miaka minne sasa.

Mbali na kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara, vyama vya upinzani husuani Chadema, ACT Wazalendo na CUF, vinaelekea uchaguzi huo vikiwa na makovu ya baadhi ya wabunge, madiwani na viongozi wengine kuhamia chama tawala kwa madai ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano.

Kwa upande wake, CUF inaelekea katika uchaguzi huo ikiwa tofauti na ilivyokuwa mara ya mwisho wakati ikishiriki uchaguzi huo, kwani mgogoro wa uongozi kati ya Mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Lipumba na aliyekuwa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad umekiacha chama hicho katika vipande vipande.

Baadhi ya wachambuzi wanaona uchaguzi huu ni jukwaa la pande zote mbili za chama tawala na upinzani kuonyeshana nguvu yao, na namna wanavyokubaliwa na umma iwapo uchaguzi utakuwa huru na haki.

Mara nyingi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unapofanyika katika misingi ya ukweli na uwazi, hutoa taswira ya hali itakavyokuwa Uchaguzi Mkuu unaofuata ambao kwa sasa tunazungumzia wa mwaka 2020.

Katika uchaguzi wa sasa, rekodi ambayo kila upande unaonekana kuumiza kichwa ili kuivuka ni ile ya uchaguzi kama huu wa mwaka 2014.

Katika uchaguzi huo, CCM pamoja na kuongoza, ushindi wake ulipungua kwa asilimia 12 kutoka 96 za mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 84.

MATOKEO YA 2014

Katika nafasi ya wenyeviti wa vijiji, CCM kilipata 9,378 (asilimia 79.81) wakati kwa vitongoji 48,447 (asilimia 79.83) na kwa mitaa 2,583 (asilimia 66.66).

Kwa upande wa wajumbe wa Serikali za vijiji na mitaa, CCM kilipata 100,436 (asilimia 80.24) na wajumbe wa viti maalumu 66,147 (asilimia 82.13).

Vyama vya upinzani wakati huo vikiwa na nguvu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambayo sasa inaonekana itaikosa kutokana na mgogoro ulioikumba CUF, vilichukua viti vingi kwa mara ya kwanza katika historia ya uchaguzi huo.

Chadema walishika nafasi ya pili nyuma ya CCM kwa kupata wenyeviti wa vijiji 1,754 (asilimia 14.93), vitongoji 9,145 (asilimia 15.07) huku wakipata mitaa 980   (asilimia 25.29).

Katika nafasi za wajumbe wa Serikali za vijiji na mitaa, chama hicho kilipata 18,527 (asilimia 14.80) na wajumbe viti maalumu  10,471 (asilimia 13).

CUF wao walikuwa nafasi ya tatu na katika wenyeviti wa vijiji walipata viti 516 (asilimia 4.39), wenyeviti wa vitongoji 2,561 (asilimia 4.22) na wenyeviti wa mitaa 266 (asilimia 6.86).

Katika nafasi ya wajumbe wa Serikali za vijiji na mitaa walipata 5,395 (asilimia 4.31) na viti maalumu wakapata wajumbe 2,676 (asilimia 3.32).

NCCR-Mageuzi katika nafasi ya wenyeviti wa vijiji ilipata 67 (asilimia 0.57), wenyeviti wa vitongoji 339 (asilimia 0.56), wenyeviti wa mitaa 28 (asilimia 0.72), wajumbe Serikali za vijiji na mitaa 598 (asilimia 0.48) na viti maalumu 455 (asilimia 0.56).

Kwa upande wa vyama vingine, TLP walipata wenyeviti wa vijiji 10 (asilimia 0.09), NLD wawili (asilimia 0.02), UDP 14 (asilimia 0.12), NRA mmoja (asilimia 0.01) na vilivyobaki havikupata uwakilishi.

Aidha chama cha ACT Wazalendo ambacho sasa kimeongezewa nguvu kutokana na kundi la Maalim Seif kuhamia ndani ya chama hicho likitoka CUF, wakati huo kilipata wenyeviti wa vijiji nane (asilimia 0.07).

Kwa upande wa wenyeviti wa vitongoji, TLP kilipata 55 (asilimia 0.09), NLD wawili (asilimia 0.00), ACT 72 (asilimia 0.12), UDP 54 (asilimia 0.09), APPT Maendeleo watatu (asilimia 0.00), NRA watatu (asilimia 0.00) na vyama vingine havikupata uwakilishi.

Na kwa wenyeviti wa mitaa, TLP ilipata mmoja (asilimia 0.03), ACT 12 (asilimia 0.31), UDP watatu (asilimia 0.08), NRA mmoja na UMD mmoja (asilimia 0.03).

Katika nafasi ya wajumbe Serikali za vijiji, TLP ilipata 62 (asilimia 0.05), NLD watatu (asilimia 0.00), ACT 106 (asilimia 0.08), APPT Maendeleo mmoja, Chaumma mmoja na NRA wanne (asilimia 0.00).

Wajumbe wa viti maalumu, TLP ilipata 63 (asilimia 0.08), NLD mmoja (asilimia 0.00), ACT 57 (asilimia 0.07), UDP 43 (asilimia 0.05), APPT Maendeleo mmoja na Chaumma mmoja (asilimia 0.0).

Uchaguzi wa mwaka huu unakwenda kufanyika wakati vyama vya upinzani vikiwa na hasira ya majeraha yaliyotajwa hapo juu na CCM vilevile ikiwa na hasira ya kupunguza asilimia 12 katika uchaguzi uliopita.

MALALAMIKO YA FIGISUFIGISU

Wakati uchukuaji na urudishaji fomu ukifikia kikomo kesho, tayari malalamiko ya figisufigisu yameonekana kutolewa zaidi na vyama vya upinzani kuliko CCM.

Viongozi wa vya Chadema, ACT Wazalendo na CUF tayari wametoa malalamikao ya kuhujumiwa katika kipindi hiki cha uchukuaji na urudishaji fomu.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alikaririwa na vyombo vya habari mara kadhaa akiorodhesha mambo sita aliyoyaita kuwa ni makubwa ambayo alidai yamefanyika nchi nzima ili kuwanyiwa haki wagombea wao kuchukua fomu.

Alidai kwanza katika baadhi ya maeneo fomu zilitolewa zikiwa hazina mihuri wala nembo za halmasharui husika, akitolea mfano Karatu mkoani Arusha.

Mrema alisema kujaza fomu ambazo hazina nembo ya halmashauri, kikanuni mgombea anakuwa amekosa sifa, hivyo anakuwa amejiondoa.

Alidai kuwa wagombea wengine walipewa kesi ili baada ya kukamatwa watoe fursa kwa wagombea wengine kuchukua fomu.

Mrema alidai pia kuna waliopewa fomu pungufu ya tatu zinazotakiwa, ikiwamo ya maadili ambazo wanajaza na wakirudisha wanabaki na nakala.

Alitaja maeneo ambayo fomu za maadili hazikutolewa kwa wagombea wao kuwa ni Rukwa, Mara, Shinyanga, Nyamagana mkoaniMwanza, Longido, Karatu na Kigoma.

Aidha alidai katika baadhi ya maeneo vituo havikufunguliwa na hivyo kufanya wagombea wao kushindwa kuchukua fomu.

Alidai katika Jimbo la Vwawa, Kata ya Ilolo, Mbozi wagombea wao walikataliwa kuchukua fomu kwa madai kuwa tayari zimeshachukuliwa huku Kata ya Ibaba, Ileje mkoani Mbeya wagombea wao wakinyimwa fomu kwa sababu ya kutochangia mchango wa Mwenge wa Uhuru.

Mrema pia aliyataja maeneo  mengine zilikojitokeza kasoro hizo kuwa ni Kata ya Tanganyika, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Isimani Iringa, Katavi na Njombe ambako alidai kuwa wagombea wao walikamatwa kwa amri ya Mkuu wa Wilaya.

Malalamiko kama hayo pia yalitolewa na viongozi wa ACT Wazalendo na CUF.

Mkurugenzi wa Habari na mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya alikaririwa na vyombo vya habari alidai kuwa katika kipindi cha uchukuaji wa fomu wagombea wao wanakamatwa na kupewa kesi na kutaja maeneo ya Bagamoyo Pwani na Misungwi Mwanza.

Alisema uchukuaji na urejeshaji fomu umejaa ukiritimba na kudai kwamba huko Simiyu wagombea wao wamejazishwa fomu feki.

Aidha kwa upande wake CCM, wanadai ofisi zao tatu zimechomwa moto na watu ambao tayari Jeshi la Polisi mkoani Songwe limewatia nguvuni.

Mbali na kuchoma moto ofisi hizo, watu hao tisa wanaoshikiliwa polisi, wanadaiwa pia kuchoma ofisi tatu za vijiji, ng’ombe wawili, nyaraka za Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na kukata miti 100 ya zao la kahawa.

JAFO AKIRI DOSARI

Oktoba 30, mwaka huu Waziri katika ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alikiri kutokea dosari katika siku ya kwanza ya uchukaji wa fomu na kuwataka watendaji kujirekebisha.

Pia alikiri kutolewa kwa malalamiko katika kata 72 nchini na kusema tayari timu ya uchaguzi ya Tamisemi inayashughulikia.

Hata hivyo, Novemba 1, mwaka huu ACT Wazalendo ilikuja na tamko kuwa kinachotokea si dosari bali ni hujuma dhidi ya vyama vya upinzani.

Mratibu wa Mawasiliano wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa ACT Wazalendo, Mbarala Maharagande alisema wanachama wao wanaojitokeza kuchukua fomu wanakatishwa tamaa na vikwazo wanavyokumbana navyo.

Akiwa hatofautiani sana na vyama vingine, Maharagande alisema Waziri Jafo anapaswa kuwawajibisha watendaji wake wanaofanya hujuma za makusudi.

KANUNI ZINAZOWABANA WAGOMBEA

Pamoja na hayo, suala jingine ambalo ni ngoma ngumu katika uchaguzi huu ni la kanuni 24 zinazowabana wagombea.

Miongoni mwa vifungu vinavyowabana wagombea ukiacha kile kilichozua gumzo cha kupaswa kuwa na kazi inayoeleweka, kipo kinachompa msimamizi wa uchaguzi mamlaka ya kumchukulia sheria mgombea au mwakilishi wake ambaye atatumia jukwaa la siasa kukashifu mgombea mwingine.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo, kifungu cha 27(4); “Endapo vyama vya siasa vitashindwa kuridhiana wakati wa uunganishaji wa ratiba za mikutano ya kampeni, Msimamizi wa Uchaguzi ataunganisha ratiba ya mikutano ya kampeni na uamuzi wake utakuwa wa mwisho.”

 Mbali na hilo, kanuni hizo pia zimebainisha masharti ya kufanya kampeni kwa mgombea au chama, huku zikipiga marufuku kampeni za ubaguzi, matusi na zile zinazoweza kuchochea vurugu.

“30 (2) Mgombea au mwakilishi wa mgombea au chama cha siasa chenye mgombea, hakitaruhusiwa kuendesha kampeni za uchaguzi kwa: (a) kutumia rushwa, (b) kutoa maneno ya kashfa au lugha za matusi, (c) kufanya ubaguzi wa jinsia, maumbile, ulemavu, dini, rangi, kabila au ubaguzi mwingine wa aina yoyote au (d) kutoa maeneo ambayo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kusababisha vurugu,” inaeleza kanuni hiyo.

Hata hivyo, suala hilo linakwenda kuwekewa mkazo na sura ya 11 ya makosa ya adhabu kwa mgombea ambapo kifungu 47 (2) kinasema kuwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia kwa kosa lolote chini ya kanuni ndogo ya (1) atahukumiwa adhabu ya faini isiyozidi Sh 300,000 au kifungo kisichozidi miezi 12 au vyote kwa pamoja, yaani faini na kifungo.

SABABU ZISIZOBADILI MATOKEO

Kanuni hizo zimefafanua masuala ambayo kwa namna yoyote hayawezi kubadilisha matokeo ya uchaguzi. Kanuni ya 42 imetaja; “(a) Kutokuwapo kwa mgombea au wakala wa mgombea wakati wa kupiga kura, kuhesabu kura au kutangaza matokeo au (b) mgombea au wakala wa mgombea kukataa kusaini fomu ya matokeo.”

Kuhusu makosa ya uchaguzi, kanuni ya 47 inaeleza kuwa mtu yeyote atakuwa ametenda kosa la uchaguzi endapo; (a) ataharibu orodha ya wapigakura au nyaraka zozote zinazohusiana na uchaguzi, (b) atatoa taarifa za uongo ili aweze kupiga kura au kugombea nafasi ya uenyekiti wa mtaa au ujumbe wa kamati ya mtaa, (c) atajiandikisha au kupiga kura zaidi ya mara moja kwa wagombea wa nafasi moja.

Hata hivyo baada ya kupiga kura watu wanatakiwa kusimama mita 200 kutoka eneo la kituo ambapo kifungu kinasema mtu yeyote atakuwa ametenda kosa la uchaguzi endapo; “(f) ataonyesha ishara au kuvaa mavazi yanayoashiria kumtambulisha mgombea au chama cha siasa katika eneo la mita 200 kutoka kwenye kituo cha kupigia kura.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here