Simba kujipoza, kujiongezea machungu leo?

0
989

MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

KIKOSI cha Wekundu wa Msimbazi, Simba leo kitashuka dimbani kumenyana na Mbeya City, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Simba itashuka dimbani ikiwa na jeraha ililolipata baada ya kupoteza mchezo wake uliopita dhidi ya Mwadui ya Shinyanga,  ilipokubali kichapo cha bao 1-0, mchezo uliochezwa  Uwanja wa Kambarage.

Mabingwa hao watetezi wa taji hilo,  bado wanaendelea kushikilia usukani,  wakiwa na pointi 18 walizovuna baada kucheza michezo saba, wakishinda  sita na kupoteza mmoja.

Mbeya City wanayokutanayo,  inashika nafasi ya 16 miongoni mwa timu 20 zinazochuana, ikiwa na pointi nane,  ilivovuna baada ya kucheza michezo nane, ikishinda mara moja, sare tano na kupoteza mara mbili.

Wagonga Nyundo hao wa Jiji la Mbeya, wana kiu ya kuvuna pointi tatu, kwani mchezo wao uliopita walilazimisha suluhu na Alliance, Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Lakini rekodi zinaipa nafasi kubwa Simba ya kuibuka mbabe.

Katika michezo miwili ambayo timu hizo zilikutana msimu uliopita, Simba ilikomba zote.

Ikianza kushinda mabao 2-0 nyumbani Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kabla ya kupata ushindi wa mabao 2-1, Uwanja Sokoine, Mbeya.

Mbeya City inayofundishwa na kocha, Juma Mwambusi, imekuwa ikisuasua  tangu msimu huu umeanza.

Lakini Mwambusi ana rekodi chanya dhidi ya Simba, kwani msimu wake wa kwanza akiwa na Mbeya City hakuwahi kupoteza.

Mbeya City ilianza kuilazimisha Simba sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa, kabla ya kupata matokeo kama hayo Uwanja wa Sokoine.

 Simba itakuwa imesheheni,  baada ya nyota wake watatu waliokuwa majeruhi kurejea kundini, hawa ni nahodha John Bocco na mabeki Shomari Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, waliokosekana mechi mbili zilizopita.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amesema wana kila sababu ya kuondoka na pointi tatu kwa kuwa watacheza kwenye uwanja ambao wameuzoea.

“Tunacheza nyumbani  tena kwenye uwanja ambao tumeuzoea,

“Ikiwezekana tufunge mabao mengi kwa sababu tutakuwa katika eneo letu la kujidai, Uwanja wa Uhuru ambao tumeuozoea tofauti na viwanja vya mikoani,” alisema.

Kwa upande wake, Mwambusi alisema amejipanga vilivyo kukabiliana na Simba na lengo lao kubwa ni kuhakikisha hawatoki mikono mitupu.

Mbali na mchezo huo, kivumbi kingine cha ligi hiyo kitatimka Nangwanda Sijaona  mkoani Mtwara ambapo, Ndanda FC itakuwa nyumbani kupambana na Ruvu Shooting,Polisi Tanzania itaikaribisha Alliance FC, Uwanja wa Chuo cha Ushirika, Moshi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here