23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

WEZI WATEKA AKAUNTI YA PADRI, WAIBA MAMILIONI

Na EVANS MAGEGE – Dar es Salaam

GENGE la kimataifa la wezi wa fedha kwa njia ya mtandao limevamia akaunti ya barua pepe ya Padri Paschal Luhengo wa Kanisa Katoliki nchini na kufanikiwa kuiba mamilioni ya fedha yaliyotumwa na marafiki zake wanaoishi nje ya nchi.

Padri Luhengo ambaye ni Paroko wa Parokia ya Lupiro, Jimbo la Mahenge mkoani Morogoro, aligundua wizi huo, Oktoba mwaka jana wakati tayari wezi hao wakishirikiana na wengine wa hapa nchini, walikuwa wameishachukua zaidi ya Dola za Marekani 18,000 sawa na Sh milioni 36 kutoka kwa marafiki zake mbalimbali wanaoishi barani Ulaya.

Taarifa ambazo Padri Luhengo amezithibitisha, zinaeleza kuwa genge hilo la wezi liliingilia barua pepe (E-mail) yake na wakatumia mwanya huo kuwasiliana na marafiki zake walioko Ulaya na kuwaomba msaada wa fedha za matibabu ya figo.

Kwa kutumia akaunti hiyo ya barua pepe, wezi hao waliwaelekeza marafiki wa Padri Luhengo kutuma michango yao ya fedha kwa njia ya Western Union.

MTANZANIA Jumapili lilizungumza na Padri Luhengo katikati ya wiki katika eneo la Kanisa Katoliki Msimbazi, Dar es Salaam ambaye alifafanua jinsi alivyobaini wezi hao.

Padri Luhengo alisema kuwa siku za nyuma alibaini majaribio kadhaa ya kuingiliwa kwa akaunti yake ya barua pepe.

Alisema alijitahidi kukwepa majaribio hayo kwa kubadilisha nywira (password) ya akaunti yake.

Kwa mujibu wa maelezo yake, baada ya kufanya hivyo mara kwa mara, ulifika wakati akaunti yake ikawa haifunguki kila akiingiza nywira.

Alisema kuwa kitendo hicho hakikumshtua kama akaunti yake ya  barua pepe imeingiliwa,  bali alijua imefungiwa.

Hata hivyo, alibaini kama kuna tatizo Oktoba 27, mwaka jana baada ya kuomba msaada wa fedha kidogo kwa rafiki yake, Padri Leopold Mlimbo anayeishi nje ya nchi.

Padri Mlimbo alimtumia Dola za Marekani 545.25 (Sh. milioni 1.2) kwa njia ya Western Union.

“Baada ya Padri kuniambia ameishanitumia, nilikwenda posta Ifakara kuchukuwa fedha hizo. Nilipofika wakaniambia muamala huo haupo mtandaoni,” alisema.

Padri Luhengo alisema baada ya tukio hilo, siku chache baadaye akapigiwa simu na rafiki yake ambaye ni daktari huko nchini Austria.

Alisema kuwa rafiki yake huyo alikuwa anaulizia maendeleo ya matibabu yake ya kubadilishiwa figo.

“Nilishangaa na nikamwambia mimi ni mzima kabisa, sina tatizo lolote la afya, rafiki yangu akaniambia kwamba alipokea barua pepe kutoka kwangu nikiomba msaada wa fedha za matibabu ya kubadilishiwa figo na yeye alikuwa ameishatuma mchango wake, pia baadhi ya marafiki zangu wengi huko Ulaya wametuma,” alisema Padri Luhengo.

Alisema baada ya taarifa hizo, Desemba 5 mwaka jana alikwenda kuripoti katika kituo cha polisi kinachohusika na mambo ya uhalifu wa fedha (Financial Crime Unit) ambacho kipo Kamata, Dar es Salaam.

Padri Luhengo alisema kuwa aliwaeleza askari wa kituo hicho kwamba akaunti yake ya barua pepe imevamiwa na wezi ambao wanaiba fedha kwa njia ya Western Union.

Baada ya maelezo hayo, polisi wa kituo hicho walimwambia aende kuripoti Kituo cha Polisi Msimbazi, Kariakoo, Dar es Salaam.

Alisema kuwa wakati anakwenda kuripoti, alipata taarifa nyingine kwamba rafiki zake huko Ulaya wanataka kumtumia dola 200,000 (zaidi ya Sh milioni 400) za ujenzi wa kanisa.

Kwamba rafiki zake walielekezwa na wezi hao walioingilia akaunti yake ya barua pepe, watume fedha hizo  kupitia Benki ya BOA.

Aliitaja anwani na akaunti hiyo kuwa ni:

Bank Name (Jina la benki): BOA Bank

Bank Adress (Anuani ya benki); NDC Dev’t House, Ohio Street/Kivukoni Front

P.O Box 3054, Dar es Salaam, Tanzania

Branch (Tawi): Msimbazi Branch

Account Name (Jina la akaunti): LUPIRO MAHENGE PARISH

Account No (Akaunti namba): 01646030005

Swift Code(Namba maalumu): EUAFTZT

Alisema baada ya kuripoti taarifa hizo mbili katika kituo cha Msimbazi, akafunguliwa jalada MS/RB/9245/2016 na MS/RB/9244/2016.

Padri Luhengo alisema baada ya kufunguliwa kwa majalada hayo, polisi wa Msimbazi walifanikiwa haraka kuzima mpango wa fedha zaidi ya milioni 400 ambazo zilitakiwa kutumwa kupitia Benki ya BOA.

“Polisi Msimbazi waliwataarifu BOA na wakachukua nyaraka kubaini wamiliki wa akaunti iliyofunguliwa kwenye benki hiyo. Kesi na vielelezo vyote vikapelekwa kitengo cha polisi kinachoshughulika na mambo ya Finance Crime Unit ambacho kipo Kamata jijini Dar es Salaam, lakini ninavyokwambia mpaka leo hawajamkamata mtu yeyote.

“Wamenipa picha za mtu aliyefungua akaunti BOA Bank na wakaniambia ni jamaa mmoja anamiliki shule ya sekondari huko Tabata, na wameishamwita wakamuhoji, akasema yeye sio mwizi ila akawataja watu wanaohusika na wizi wa aina hiyo, baada ya maelezo hayo polisi wakamwachia,” alisema Padri Luhengo.

 

BOA WAFAFANUA

MTANZANIA Jumapili lilifika makao makuu ya Benki ya BOA yaliyopo jengo la NDC, Mtaa wa wa Ohio na Kivukoni Front, Dar es Salaam ili kupatiwa uthibitisho wa akaunti inayodaiwa kufunguliwa na wahalifu hao ili kupitisha dola 200,000( zaidi ya Sh milioni 400).

Baada ya maelezo ya tukio hilo, ofisa wa benki hiyo ambaye alikataa kujitambulisha kwa kusema suala hilo ni la kisheria zaidi, alimwelekeza mwandishi kuwa akazungumze na Meneja wa benki hiyo tawi la Msimbazi ambako akaunti hiyo ilifunguliwa.

MTANZANIA Jumapili lilifika lilipo tawi hilo na kufanikiwa kumpata meneja ambaye aliyejitambulisha kwa jina la Ferdinand Urasa.

Katika mazungumzo yake na MTANZANIA Jumapili, Urasa alikiri kutokea kwa tukio hilo na akasema ameishaandika maelezo, kwamba mambo yote yapo kwenye ngazi ya polisi kwa upelelezi zaidi.

“Ni kweli huyu Padri alishakumbwa na kadhia hii, polisi walikuja hapa nikawaeleza kila kitu na kweli akaunti hii ilifunguliwa hapa na uchunguzi wa awali ulionyesha akaunti hii ilifunguliwa na mtu binafsi na mtu huyo aliitwa na akathibitisha kuwa ni akaunti yake, sisi kama BOA mwisho wetu ulikuwa hapo, mambo zaidi yako kwenye ngazi ya polisi,” alisema Urasa.

 

MAENDELEO YA UPELELEZI

Padri Luhengo alisema Machi mwaka huu, aliwauliza polisi kuwa wamefikia wapi upelelezi wao na wakamjibu kwamba tayari wamepata miamala aliyoibiwa na wamemtambua mtu aliyehusika na wizi huo.

Katika hatua nyingine, Padri Luhengo alisema baada ya kubaini kuwa akaunti yake ya barua pepe imetekwa, aliandika maombi Google International kuomba wamrejeshee akaunti yake ya awali na walipomrejeshea, alibaini mawasiliano ya barua pepe zote yalikuwa yamefutwa kasoro barua pepe moja tu ambayo mawasiliano na maelekezo ya kupata fedha yalikuwa kati ya mtu aliyejulikana kwa jina la Mila Ledesma ambaye anaishi Marekani na Paulina Mkama ambaye anaishi hapa nchini.

Kulibainika kuwapo kwa muamala wa fedha ambao Ledesma ametuma dola 1,500 (zaidi ya Sh milioni 3) kwenda kwa Paulina.

Alisema uchunguzi zaidi umeonyesha miamala mingine miwili ya fedha ambayo Ledesma alimtumia Paulina.

Muamala wa kwanza ulionyesha kuwa Ledesma alimtumia Paulina dola 3,300 (zaidi ya Sh milioni 7) kupitia kwa wakala APH051022, Desemba 6, 2016 na muamala wa pili alituma kiasi hicho hicho kupitia wakala APH227793, Desemba 5, 2016.

Padri Luhengo alisema kwa inavyoonekana, Ledesma anaishi Toms River nchini Marekani na fedha zote alizotuma zilipokewa na Paulina. Muamala wa kwanza ulipokewa kupitia wakala ACP10036, Desemba 7, 2016, mwingine kupitia wakala ACPO10036, Desemba 6 mwaka jana, huku muamala mwingine akiupokea Desemba 3 mwaka jana kupitia kwa wakala ACP001094.

“Naamini huyu Mila Ledesma ambaye anaishi nchini Marekani ndiye aliyeingilia (hacking) akaunti yangu ya barua pepe. Nashindwa kuelewa, vitambulisho vyake vinaeleweka, lakini sijapewa taarifa kama kuna juhudi zozote za kuwatumia polisi wa kimataifa kumkamata,” alisema Padri Luhengo.

 

MIAMALA ILIYOIBWA

Padri Luhengo alitoa nakala zinazoonyesha jumla ya miamala sita ya fedha ambazo rafiki zake walituma kwa njia ya Western Union na kuchukuliwa na wezi.

Alisema rafiki zake hao walituma fedha hizo kama mchango wa matibabu ya figo baada ya kupata barua pepe ya kuwataka kufanya hivyo kutoka kwa wezi hao.

Aliwataja majina marafiki waliomtumia kuwa ni pamoja na Claudia Ehrhardt ambaye Novemba 14 mwaka jana alituma dola 271.2 (Sh 604,859) kupitia wakala A2G290012.

Wengine ni Christoph Doppelreiter ambaye Novemba 3 mwaka jana alituma dola 3,328.79 (Sh milioni 7.4) kupitia kwa wakala A20047913, Padri Leopold Mlimbo Oktoba 27 mwaka jana alituma dola 545.29 (Sh milioni 1.2) kupitia kwa wakala A20031743 na Christoph Doppelreiter  kwa mara nyingine Oktoba 20 mwaka jana alituma dola 2632.07 (Sh milioni 5.8) kupitia kwa wakala A20047913.

Mwingine ni Gabriella Bare aliyetuma mara mbili, Oktoba 18 mwaka jana dola 5747.83 (Sh 12.8) kupitia wakala AAU001218 na Oktoba 16 mwaka huo huo dola 3353.89 (Sh milioni 7.4) kupitia wakala AAU001218.

 

VITAMBULISHO

Padri Luhengo alitoa nyaraka nyingine iliyokuwa inaonyesha vitambulisho vilivyokuwa vinatumiwa na wezi hao kuchukua fedha kwenye miamala mbalimbali iliyotumwa kwa njia ya Western Union.

Kitambulisho No. 32654879 ambacho  kinaonyesha mmiliki alizaliwa Januari Mosi, 1980, kilitumika kuchukua fedha Novemba 14, mwaka 2016.

Kitambulisho kingine ni T 100498765074 ambacho kilitumiwa kuchukuwa fedha Novemba 4 mwaka 2016 na mmiliki wake kazaliwa Julai 22, 1980. Kitambulisho hicho hicho pia kilitumiwa kuchukuwa fedha Oktoba 28, 2016.

Kitambulisho kingine kina No. T 100498765072, muamala ulifanyika Oktoba 21, 2016 na kinaonyesha mtumiaji alizaliwa Aprili 13, 1973. Pia kitambulisho hicho kilitumika kuchukuwa fedha Oktoba 19 mwaka jana.

Kitambulisho kingine kina namba 5072 ambacho kilitumiwa kutoa fedha Oktoba 17 mwaka jana na mmiliki wake anaonekana kuzaliwa Aprili 13, 1973.

 

WALIKOTOA  FEDHA

Padri Luhengo alitaja maeneo ambayo fedha hizo zilichukuliwa na wahalifu hao ni Benki ya Equity tawi la Mbagala, Temeke, Eco Bank na Benki ya UBA.

 

POLISI WATOA UFAFANUZI

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kitengo cha Financial Crime Unit,  Deusdedit Mataba, ambaye alikiri kwamba Paulina Mkama ndiye anaonekana kupokea fedha hizo, lakini Jeshi la Polisi bado halijafanikiwa kumpata.

Alifafaua zaidi kwamba watu wanaweza kutumia majina tofauti kutenda uhalifu ingawa Jeshi la Polisi linajitahidi kushughulikia suala hilo la Padri Luhengo.

“Ni padri wa kwanza kutulalamikia, lakini na sisi tupo kama yeye, ambavyo kuna waumini ambao wanatenda dhambi kila siku, wanatubu mbele yake na kwenye madhabahu, lakini hajaweza kuwafanya wasiendelee kutubu. Kwa mantiki hiyo na sisi tunaendelea kumtafuta huyu mtu.

“Atupe muda, badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari na kutuchafua kana kwamba sisi ndio tumeshirikiana na mhalifu kumwibia fedha, kwa kweli inakuwa haifurahishi sana na mara ya mwisho alitutishia kwamba ataenda kulala na waumini wake Ikulu. Sasa jamani sisi tumekuibia? Na sisi tunatumia utaalamu wa watu wengine, angekuwa ameiba yupo kwenye kituo cha polisi sawa,” alisema Kamanda Mataba.

Aliongeza kwamba Jeshi la Polisi bado linahitaji msaada wa Western Union ili kuweza kumpata mhalifu huyo.

Alipoulizwa kuhusu mtu waliyemkamata ambaye alifungua akaunti BOA na wakampa picha yake Padri Luhengo, alisema kuna mambo mengine ya kipelelezi bado yanaendelea, hivyo akamsihi Padri Luhengo awapatie muda kuliko kukimbilia kwenye vyombo vya habari.

“Mwambie kwamba atuvumilie, tunaendelea kumtafuta huyo Paulina na watu wa kuweza kutusaidia ni huko alikochukulia fedha, ujue Western Union imesambaa na karibu kila benki kuna huduma ya Western Union, kwa hiyo bado tunafuatilia kwa sababu hawa wahalifu wana mbinu nyingi, kama ambavyo waliweza kuingilia (hack) akaunti yake ya barua pepe (e-mail) na kuchukuwa nywira,” alisema Kamanda Mataba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles