26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

ELIMU BURE ZANZIBAR KUANZA MWAKANI

Na Mwandishi Maalumu – Pemba

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ametangaza rasmi kuwa kuanzia Julai Mosi, mwakani, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itatekeleza mpango wake wa kutoa elimu bure kwa shule za sekondari za Serikali na michango yote wanayotozwa wazazi haitokuwapo tena.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana katika kilele cha Sherehe za Tamasha la Elimu Bila ya Malipo zilizofanyika katika Uwanja wa Gombani na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, mawaziri, viongozi wengine wa Serikali, wananchi na wanafunzi kutoka Unguja na Pemba.

Dk. Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alisema kuanzia bajeti ya mwaka 2018/2019, shule zote za Serikali za sekondari zitatoa elimu bila ya malipo na kwamba ile azma ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume ya elimu bure, itakuwa imekamilishwa.

Alisema Serikali yake inao uwezo huo na ndani ya bajeti yake bila ya kumkopa ama kumwazima mtu na hiyo ndiyo ahadi yake na ataitangaza siku itakapoanza kutekelezwa rasmi.

“Hatuna sababu ya kushindwa kutoa elimu bure, iwe ya maandalizi, msingi ama sekondari na naiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Wizara ya Fedha na Mipango, wawe makini katika kuipanga Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya mwaka 2018/2019,” alisema.

Kuhusu elimu ya juu, alisema utaratibu wa kutoa mikopo utaendelea kama ilivyo hadi pale zitakapofanywa taratibu nyingine.

Alisema katika kipindi cha miaka 53 ya mapinduzi, mafanikio makubwa yamepatikana katika kuyatekeleza malengo yake na katika kipindi chote hicho, Serikali imeendelea kutoa elimu bila ya malipo, ingawa si kwa kiwango cha miaka 15 ya mwanzo baada ya mapinduzi.

Dk. Shein alisema hatua hiyo inatokana na sababu za matatizo ya uchumi na ongezeko la idadi ya watu yaliyoikumba nchi na Serikali ililazimika kuwaomba wananchi wachangie elimu kwa utaratibu maalumu ulioandaliwa kuanzia shule za msingi hadi sekondari.

Pia alisema kuanzia Julai, mwaka juzi, suala la uchangiaji wa elimu katika shule za awali na msingi kwa Unguja na Pemba limeondolewa na Serikali inatoa elimu ya msingi bila malipo kama ilivyoamuliwa baada ya mapinduzi.

Katika hatua nyingine, alisema Serikali inazitambua changamoto za walimu na itaendelea kuchukua hatua katika kukabiliana nazo na kwa sasa vipaumbele ni kuimarisha ubora wa elimu, miundombinu kwa kujenga shule mpya, kuyakamilisha majengo yaliyojengwa na wananchi, kuzitengeneza shule za zamani, kuzipatia vifaa vya maabara, samani na vitabu.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alisema wataendelea kuimarisha sekta ya elimu na kuhakikisha kuwa juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakisha walimu wanatoa elimu bora.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles