31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: HAMUWEZI KUJUA MATESO NINAYOYAPATA

Na JANETH MUSHI-ARUSHA

WAKATI Novemba, mwaka huu anatimiza miaka miwili tangu aapishwe, Rais Dk. John Magufuli, ameelezea ugumu wa urais na kusema kuwa ni kazi inayohitaji kumtanguliza Mungu na ameamua kujitoa sadaka kwa Watanzania kwa kuwanyoosha mafisadi waliozoea kuwaibia.

Kauli hiyo aliitoa jijini hapa jana alipowahutubia wananchi katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid baada ya kuwatunuku Kamisheni ya Cheo cha Luteni Usu maofisa wanafunzi 422 wa kundi la 61 la mwaka jana kutoka Chuo cha Kijeshi Monduli (TMA), Shule ya Mabaharia na Shule ya Anga.

“Naifahamu kazi hii, ni ngumu, ni msalaba, inahitaji kumtanguliza Mungu kwelikweli kwa sababu ni kujitoa sadaka, lakini nimeamua niwe sadaka ya Watanzania kwa ajili ya kuwanyoosha mafisadi hawa ambao wamezoea kuwaibia Watanzania,” alisema.

Pia alisema anaamini inawezekana hapatatokea rais mwingine atakayejitoa kama yeye anavyojitoa.

“Najua siku moja mtakumbuka ninavyojitoa, hamuwezi mkajua mateso ninayoyapata, ni shida kuwa rais, ndiyo maana Baba wa Taifa aliwahi kusema pale ni mateso, mimi nimeyaona mateso ya kuwa Ikulu, niliomba kwa kujaribu nikasukumiziwa huko.

“Nikasema hawa Watanzania wananipa mimi urais, lakini ni hivyo na kwa sababu nimeingia bila kutoa rushwa ya aina yoyote na nilikuwa najaribu, sasa ni lazima nifanye kazi kwa Watanzania hawa wanyonge, siku zote nitasimama, hakuna mtu mimi aliyenichangia hela, hakuna fisadi aliyenichangia, wala siogopi kumtumbua kwa sababu sikula hela yake.

“Hili la kutumbua wataumbuka kweli kweli na kama wapo mafisadi na wanaotaka kula hela za watu, wajiandae watubu na kama wamezificha hizo hela zitawaozea,” alisema.

Si mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuelezea ugumu wa kazi ya urais tangu aingie madarakani Novemba 5, mwaka juzi.

Alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa maabara ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mwaka jana, alimweleza mtangulizi wake, Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa amemwachia kazi ngumu.

Alikuwa akielezea jinsi alivyoikuta nchi ikiwa na wanafunzi na wafanyakazi hewa katika idara mbalimbali.

Pia Novemba 4, mwaka jana, alipozungumzia safari yake ya mwaka mmoja wa urais wake, alisema kuna makaburi amelazimika kutoyafukua kwa sababu yanaweza kumshinda kuyafukia.

Alisema kazi ya kuiongoza nchi si nyepesi na kuwashangaa wale wanaoutaka urais.

Agosti 7, mwaka huu, akiwa Korogwe mkoani Tanga, alisema hawezi kukaa madarakani baada ya kipindi chake kwisha, kwa kuwa anaheshimu katiba na kwamba kazi ya urais ni ngumu.

Alitoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani (CCM), kusema kwa kuwa Rais Magufuli anafanya kazi nzuri, itakuwa vizuri akiongezewa hata miaka 20 madarakani.

 

AJIRA 3,000 JESHINI

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametangaza nafasi 3,000 za ajira mpya kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), huku kipaumbele akitaka kitolewe kwa waliopitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Alisema kuwa mwaka huu Serikali imetangaza ajira 50,000 na kati ya hizo, 3,000 zitatolewa kwa JWTZ, lengo likiwa ni kuhakikisha jeshi hilo linakuwa na askari wa kutosha na kuwa la kisasa zaidi, huku akiahidi kuanza kushughulikia matatizo yanayowakabili.

“Jana (juzi) nilikutana na makamanda wakiongozwa na mkuu wa majeshi, nilieleza kuanzia wiki inayokuja tutaanza kushughulikia baadhi ya madai yenu ili tuwe na jeshi la kisasa kabisa. Lakini pia tumepata maofisa 422, unapokuwa na jeshi la maofisa, ni lazima pawepo na ‘junior officers’, huwezi ukawa na jeshi lote una maofisa tu,” alisema na kuongeza:

“Kwa kutambua hili, najua hili nilikuwa sijawaeleza hata jana (juzi), natangaza rasmi kwamba nitatoa nafasi 3,000 za kuajiri wanajeshi wapya na hawa watakaoajiriwa mzingatie hasa wale waliomaliza JKT, lengo ni kuhakikisha jeshi letu linakuwa na maaskari wa kutosha na tuwe na jeshi la kisasa zaidi.”

 

SAFARI ZA NJE

Kuhusu safari za nje ya nchi, alirudia kusema kuwa amekuwa akipokea mialiko katika nchi mbalimbali na kudai hawezi kwenda kwa sababu anasafisha nyumba yake (Tanzania) kwanza.

“Wanakuja kwa sababu Tanzania inaaminika kimataifa na ndiyo maana kila mara wananialika kule na hadi sasa nimeshaacha mialiko karibu 60, tunaomba uje huku, mimi nije kufanya nini? Ninasafisha kwanza hapa, nikienda huko pataharibika, nasafisha kwanza nyumba yangu.

“Niliomba urais wa Tanzania, sikuomba urais wa kutembelea nchi nyingine, nchi zingine nilitembelea nikiwa mwanafunzi kote kule, nimefika Uingereza, najua sasa ni wakati wangu wa kuchapa kazi, fedha  nyingi zilikuwa zikitumika kwa safari za nje, kuna watu walikuwa wanapishana angani hawaendi hata nyumbani kwao kwa gharama za Watanzania masikini, nimesema hapana,” alisema.

 

KUHAMIA DODOMA

Akizungumzia kuhusu Serikali kuhamia Dodoma, alisema tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameshahamia na mwaka huu Makamu wa Rais, Samia Suluhu, anatarajiwa kuhamia na yeye atahamia mwakani na wafanyakazi ambao hawatahamia na kuendelea kubaki Dar es Salaam kazi zao zitaisha.

 

BEI YA SUKARI

Kuhusu sukari, Rais Magufuli alisema wakati anaingia madarakani, alikuta kilo moja inauzwa kati ya Sh 5,000 hadi 6,000, lakini sasa hivi imeshuka na itashuka zaidi vikianzishwa viwanda.

Pia alisema saruji mkoani Kagera ilikuwa Sh 17,000 ila sasa hivi imeshuka na Arusha alipowauliza wananchi, alijibiwa kuwa inauzwa Sh 12,000 na kabla ya hapo ilikuwa inauzwa Sh 14,000 hadi 15,000.

 

TANZANIA MPYA

Pia alisema anataka Tanzania mpya ya viwanda, hivyo tangu aingie madarakani ameanza kushughulikia uozo uliokuwapo nchini na anapoamua kushughulikia masuala hayo, kuna baadhi ya watu hawafurahi kwa sababu walikuwa wamezoea kufaidika na jasho la masikini.

 

WATEULE WAKE WAJITATHMINI

Rais Magufuli aliwataka wateule wake wote kuanzia Waziri Mkuu Majaliwa hadi ngazi za chini, kujitathmini katika utendaji wao wa kazi katika kipindi walichopewa dhamana ya uongozi, iwapo wametekeleza majukumu yao ipasavyo na kuwa hata yeye atajitathimini katika kipindi cha miaka miwili alichokaa madarakani.

 

MKUU WA MAJESHI

Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, alisema kuwa wameandika historia moja kwa kufanyia shughuli hiyo katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid wakati kwa kawaida imekuwa ikifanyika TMA.

Aliwataka wanajeshi kulinda na kutekeleza kiapo chao cha utii kinachowataka kumtii na kumlinda rais na katiba ya nchi.

“Leo (jana) tumeandika historia kwa shughuli hizi za kuwavika kamisheni kufanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, tunashukuru kwa miongozo na ushauri wako (Rais Magufuli) uliowawezesha wananchi kushuhudia,” alisema.

 

RC GAMBO

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema kazi ya kutunuku kamisheni uwanjani hapo haikuwa rahisi.

Kuhusu hali ya Arusha, alisema hivi sasa vurugu zimepungua katika mkoa huo, huku maandamano yakiwa hayapo tena kama kipindi cha nyuma.

“Tumefarijika na kazi kubwa nzuri unayoifanya, umeamua kujitoa mhanga, changamoto ni nyingi, lakini wakati wa uongozi wako umeamua kunyoosha rula, nikuthibitishie kama mkuu wa mkoa, hali ya ulinzi ni salama,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles