24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri wa Afya ataka wanaosaidia mapambano ya corona kuchangia BoT, kununua vifaa MSD

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amezitaka taasisi na wadau mbalimbali wanaochangia fedha na vifaa kinga na vifaa tiba, kuelekeza fedha hizo kwenye Akaunti ya serikali iliyopo Benki Kuu (BoT) na vifaa kununuliwa katika Bohari ya Dawa (MSD).
Aidha, amehamasisha matumizi ya barakoa za kitambaa ambazo zitatengenezwa hapa nchini kwa kutolewa mwongozo na wizara hiyo utakaosambazwa kote nchini.

Waziri Mwalimu alisema hayo jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akipokea mchango wa fedha na vifaa tiba na vifaa kinga kutoka kwa mashirika, taasisi na kampuni mbalimbali likiwamo Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Kampuni ya Wentworth Gas Ltd, Pavilion Stategic Holdings Ltd na Kampuni ya Pan African Energy.

“Kwa upande wa vifaa tiba na kinga mliotuchangia nasema ahsante sana, naomba niwaambie mchango wenu tunauthamini sana kwa sababu ni sehemu ya motisha kwa watumishi wa afya.

“Nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba kipaumbele cha kwanza katika mapambano ya virusi vya corona ni kuwalinda watumishi wa afya walio mstari wa mbele wasipate maambukizi.

“Ila ninachotaka kuelekeza, badala ya kila mtu kusema alete vifaa tuvikusanye hapa na pale, sisi serikali tunataka vifaa hivi vinunuliwe Bohari ya Dawa (MSD), kwa sababu pale ndipo vina viwango na ubora ambao tunauhitaji.

“Kwa hiyo hata mtu mmoja akisema ananunua katoni moja ya barakoa, fedha hiyo aipeleke MSD si lazima aingize kwenye akaunti hii kubwa tunayosema,” alisema Mwalimu.

Alisema watu wote wanao wajibu wa kujilinda na kulinda wananchi wengine kwa hiyo vifaa vinavyopokelewa kutoka nje watahakikisha vinakidhi viwango vya ubora na usalama kwa matumizi.

Pamoja na mambo mengine, alisema hivi karibuni kumekuwa na wimbi la uingizwaji wa vifaa tiba na vifaa kinga vinavyohusiana na ugojwa wa corona kwa hiyo ni lazima kujiridhisha vina ubora unaohitajika.
“Tumeona pia baadhi ya nchi wanaosha barakoa kisha zinaletwa huku kwetu, hii haikubaliki.

“Kwa hiyo nitumie fursa hii kuwaomba wadau wote ambao wanatoa vifaa hivi kutoka nje ya nchi kuzingatia mwongozo wa serikali wa upokeaji wa dawa na vifaa tiba unaotutaka kuhakikisha tunahakiki ubora na usalama wake na sisi tutahakikisha tunaendelea kuielekeza Taasisi ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), kuhakikisha wanaongeza umakini katika kuhakiki ubora na usalama wa vifaa tiba.

“Ninafurahi kuona vifaa tulivyokabidhiwa leo vinatoka ndani ya nchi, kwa hiyo nitumie pia fursa hii kutoa wito kwa viwanda vya ndani tunahitaji sana barakoa, glovu na vitakasa mikono, tungependa fedha hizi tukazitoa kwa viwanda vinavyozalisha hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles