24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Uingereza akosoa Sheria ya Vyama vya Siasa nchini

Na mwandishi wetu – Dar es Salaam

WAZIRI Kivuli wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Liz McInnes, amesema amesikitishwa na kitendo cha kupitishwa kwa Sheria ya Vyama vya Siasa hapa nchini, aliyodai inaminya vyama vya upinzani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC – Swahili), McInnes ambaye ni mbunge wa Chama cha Labour, amekaririwa na mtandao wa chama chake akisema wapinzani inabidi waachiwe uhuru wao.

“Inasikitisha kusikia kuwa Bunge la Tanzania limepitisha sheria inayozuia vikali shughuli za kisiasa na kutoa mamlaka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuvifutia usajili vyama vya upinzani..

“Wanasiasa wa upinzani wanapaswa kuwa na uhuru wa kuipa changamoto Serikali na si kuhofia kufungwa kwa kutoa maoni yao, ikizingatiwa kuwa kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani,” alisema McInnes.

Pia aliomba kuwe na tahadhari kwa sababu suala hilo linaweza kuleta athari za kiuchumi kwa taifa kwa namna ambavyo wahisani na wawekezaji wa kigeni wanavyoingiwa na hofu kuhusu mazingira ya siasa ya sasa. 

“Serikali imefanya jitihada kuokoa fedha za nchi ya tatu kwa uchumi mkubwa Afrika Mashariki tangu ilipochaguliwa mwaka 2015, lakini kuwe na tahadhari kuhusu sheria hii mpya,” alikaririwa McInnes. 

Itakumbukwa kuwa kabla ya kusainiwa na Rais kuwa sheria, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018, ulipitishwa bungeni Dodoma Januari, mwaka huu.

Kabla ya kupitishwa kwa muswada huo uliowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, kuliibuka mvutano mkali kati ya wabunge wa upinzani na CCM.

Vyama vya upinzani na asasi za kiraia vimekuwa vikilalamikia sheria hiyo, vikidai inafanya shughuli za siasa kuwa kosa la jinai. 

Mhagama akinukuliwa na chombo kimoja cha habari (si MTANZANIA), alisema pamoja na mambo mengine muswada huo unalenga kumpa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakiki chama cha siasa wakati wowote.

“Lengo ni kuhakikisha chama cha siasa kinakuwa na sifa za usajili muda wote wa uhai wake na kueleza bayana mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa kuhakiki muda wowote utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa ili kuhakikisha chama cha siasa kinazingatia na kutekeleza masharti ya usajili,” alisema Mhagama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles