23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

WAZIRI MKUU AKARIBISHA WAWEKEZAJI WA ITALIA

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Italia, ili waje kuwekeza kwenye viwanda na usindikaji bidhaa za mifugo na uvuvi kwa sababu ni eneo wanalolimudu vizuri.

Hayo aliyasema juzi Dar es Salaam alipokutana na Balozi wa Italia hapa nchini, Roberto Mengoni, kwenye makazi yake Oysterbay.

“Tumedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda, tunawakaribisha wawekezaji kutoa Italia ili waje kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya mifugo pamoja na uvuvi kwa sababu tunatambua kuwa ninyi mmebobea katika eneo hilo.

“Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa umasikini miongoni mwa wananchi wake. Tunahitaji uwekezaji mkubwa kwenye maeneo mbalimbali,” alisema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Balozi Mengoni alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika muda wa miezi minane ambayo ameishi hapa nchini, amebaini kuwa Tanzania ni nchi yenye fursa nyingi za kiuchumi.

“Ni soko kubwa ambalo halijaguswa (untapped market) hasa kwenye masuala ya viwanda na uwekezaji,” alisema.

Hata hivyo, Balozi huyo alikiri kwamba bado wananchi wengi wa Italia wanahitaji kupatiwa elimu zaidi juu ya fursa zilizopo hapa nchini.

“Hadi leo kuna Waitaliano ambao hawajui kuwa Mlima Kilimanjaro uko Tanzania. Wengi wanajua uko Kenya, kwa hiyo elimu zaidi inahitajika katika suala zima la kutangaza utalii wa Tanzania,” alisema.

Alisema tangu afike nchini, wawekezaji kutoka Italia wameonesha nia ya kuwekeza kwenye nishati jadidifu, kiwanda cha kutengeneza nguo za michezo na kwamba wafanyabiashara wengine zaidi wanatarajia kuja hapa nchini.

Ili kutoa uelewa mpana kwa wafanyabiashara na raia wa Italia, ubalozi kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) tumeandaa mkutano mkubwa wa biashara na uwekezaji utakaotoa maelezo kuhusu fursa zilizopo Tanzania katika nyanja mbalimbali.

“Mkutano huo utakaofanyika Mei 6, mwaka huu, utawalenga zaidi wafanyabiashara na utajikita kwenye maeneo makuu sita ambayo ni viwanda vya usindikaji, viwanda vya nguo (textiles), ngozi na mazao yake, miundombinu, nishati na utalii,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles