21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

WAZIRI MKUU AAGIZA KIGOGO WA WALIMU AKAMATWE

 

 

Na MWANDISHI WETU-LINDI


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Pudencis Protas,  kumkamata Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Wilaya ya Ruangwa, Anthon Mandai, kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa agizo hilo jana baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa walimu wakimlalamikia kiongozi huyo, kwamba ana tabia za kudai rushwa, kutowapandisha madaraja walimu, ulevi pamoja na kuwaita walimu hao kwenye vilabu vya pombe kwa ajili ya kusikiliza matatizo yao.

Waziri Mkuu Majaliwa, alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa akiwa katika siku ya mwisho ya ziara yake ya kikazi  wilayani hapa.

Katika maelezo yake, Waziri Mkuu Majaliwa alisema mbali na kulalamikiwa na walimu kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za ulevi na kuwaita walimu katika vilabu vya pombe pindi wanapohitaji kuhudumiwa.

Pia Mandai anadaiwa kwamba amekuwa akighushi nyaraka za mirathi, jambo linalosababisha baadhi ya familia za waliokuwa walimu kuchelewa kupata haki zao.

“Huyu katibu ameshindwa kuwasaidia walimu katika kutatua changamoto zao na badala yake amekuwa akitumia vibaya majina ya viongozi wakuu.

“Hata mimi alijaribu kutaka kunichakachua kwa kughushi muhtasari wa kikao cha mirathi ya Mwalimu Suwedi Chikawe akitumia jina langu, kwamba nilikuwa mwenyekiti wa kikao hicho kilichokuwa na agenda ya kumbadilisha msimamizi wa mirathi aliyeteuliwa na familia,” alisema Waziri Mkuu.

alimwagiza Kamanda Pudencis afanye uchunguzi wa kina utakaowezesha kukamatwa kwa mtandao wa watu wote wanashirikiana na kiongozi huyo katika kughushi nyaraka za vikao vya mirathi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa umma wabadilike na wafanye kazi kwa bidii badala ya kufanya kazi kwa mazoea.

Aliwataka watumie utalaamu wao vizuri katika kuwahudumia wananchi kwani Serikali haitawavumilia wafanyakazi watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, kuwachukulia hatua watumishi wote wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu wanaitia hasara halmashauri yao na Serikali kwa ujumla.

“Msimamo wa  Serikali ni kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo, hivyo watumishi wajiepushe na vitendo vya rushwa na matumizi mbaya ya fedha za umma. Watendaji lazima wawe na utaratibu wa kuwatembelea wananchi katika maeneo yao hasa hasa waishio vijijini kwa ajili ya kusikiliza kero zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi”, alisema.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,654FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles