23.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

Wavulana wang’ara kidato cha sita

Dk. Shukuru Kawambwa
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Shukuru Kawambwa

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam

BARAZA la Mitihani la Taifa (Necta), limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita uliofanyika Mei mwaka huu, huku ufaulu ukiongezeka kwa asilimia 8.13.

Mbali ya kuongezeka ufaulu huo, wavulana wamefanya vizuri zaidi wakati shule maarufu ya Tambaza ya mjini Dar es Salaam ikishika nafasi ya mwisho kitaifa.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, kati ya watahiniwa 10 bora, msichana ni mmoja, huku kundi lote likiwa ni wale waliosoma masomo ya sayansi, wakati wale wa mchepuo wa PCM ni tisa na PCB mmoja.

Matokeo hayo pia yanaonyesha shule zilizofanya vibaya nyingi zinatoka katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Zanzibar.

Ufaulu

Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, alisema mwaka jana ufaulu ulikuwa ni asilimia 87.85 na mwaka huu asilimia 95.98. Waliofaulu mtihani huo mwaka jana walikuwa ni wanafunzi 44,366.

Alisema watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani wa mwaka huu walikuwa 41,968, kati yao wasichana wakiwa ni 12,674, sawa na asilimia 30.20 na wavulana 35,650 asilimia 69.80.

Alisema wasichana waliofaulu mtihani huo ni 12,080, sawa na asilimia 97.66 na wavulana ni 26,825, sawa na asilimia 95.25.

“Mwanafunzi atahesabika kuwa amefaulu somo husika kama atakuwa amepata kuanzia grade ‘D’,” alisema Dk Msonde.

UBORA WA UFAULU

Alisema watahiniwa wa shule 30,225, sawa na asilimia 85.73 walifaulu kwa kati ya daraja la kwanza mpaka la tatu.

Alisema kati ya watahiniwa hao, wasichana ni 9,954 sawa na asilimia 90.59 na wavulana ni 20,271, sawa na asilimia 83.53.

Alisema waliopata daraja la nne ni 4,420, sawa na asilimia 12.54, wavulana wakiwa 3,474 sawa na asilimia 14.31 na wasichana wakiwa 946, sawa na asilimia 8.61.

Watahiwa waliopata sifuri ni 612 sawa na asilimia 1.74, wavulana wakiwa ni 524 sawa na asilimia 2.16 na wasichana wakiwa ni 88 sawa na asilimia 0.80.

Alisema watahiwa waliopata daraja la kwanza ni 3,773 sawa na asilimia 10.70, wavulana wakiwa 2,232 sawa na asilimia 9.20 na wasichana 1,541, sawa na asilimia 14.02.

Waliopata daraja la pili ni 9,631 sawa na asilimia 27.32, wavulana wakiwa ni 6,179 sawa na asilimia 25.46 na wasichana wakiwa 3,452, sawa na asilimia 31.42.

Kwa waliopata daraja la tatu ni 16,821.12.54, wavulana wakiwa ni 11,860 sawa na asilimia 48.87 na wasichana wakiwa ni 4,961 sawa na asilimia 8.61.

Alisema mfumo uliotumika kupanga matokeo hayo ni A (75-100), B+ (60-74), B(50-59), C (40-49), D (30-39), E (20- 29), F (0-19) ambao pia ulitumika kwenye mtihani wa mwaka jana.

Alifafanua kuwa daraja la kwanza lilihesabiwa kwa pointi 3 mpaka 7, daraja la pili pointi nane mpaka tisa, daraja la tatu pointi 10 mpaka 13, daraja la nne mtahiniwa alitakiwa kupata angalau D mbili, au alama isiyopungua C. Waliopata sifuri ni wale waliokuwa na D mbili pekee ama chini ya hapo.

Watahiniwa wa kujitegemea

Alisema watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa 6, kati yao waliofanya ni 5,277 sawa na asilimia 83.52.

Watahiniwa 1,041, sawa na asilimia 16.48 hawakufanya mtihani huo.

Watahiniwa 10 bora

Watahiniwa waliofanya vizuri kwa ujumla kitaifa na michepuo yao kwenye mabano ni Isaack Shayo kutoka shule ya St. Joseph Cathedral ya Dar es Salaam (PCM), Doris Hoah kutoka Marian Girls ya Pwani (PCM), Innocent Yusufu kutoka Feza Boys (PCB), Placid Pius kutoka Shule ya Sekondari Moshi ya Kilimanjaro (PCM).

Wengine ni Benni Shayo kutoka Ilboru ya Arusha (PCM), Abubakar Juma kutoka Mzumbe ya Morogoro (PCM), Mwaminimungu Christopher kutoka Tabora Boys ya Tabora (PCM), Chigulu Japhaly kutoka Shule ya Mzumbe ya Morogoro (PCM), Hussein Parpia kutoka Shule ya Alimuntazir Islamic Seminary ya Dar es Salaam (PCM) na Ramadhani Msacgi kutoka Feza Boys ya Dar es Salaam (PCM).

Watahiniwa hawa ndio pia walio kwenye kundi la wale waliofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi.

WATAHINIWA 10 BORA WA MASOMO YA BIASHARA

Waliofanya vizuri kwenye masomo ya biashara ni Jovina Leonidas kutoka Shule ya Ngaza (Mwanza), Nestory Makendi (Kibaha), Imma Anyandwile (Umbwe) na Teresia Cyprian Marwa na Grace David Chelele wote kutoka Loyola, Dar es Salaam.

Wengine ni Betrida Rugila (Baobab), Jacqueline Kalinga (Weruweru), Tajiel Elisha Kitojo (Shule ya Sekondari ya Arusha), Shriya Sanji Ramaiya (Shaban Robert) na Mwanaid Mwazema (Weruweru).

WANAFUNZI 10 BORA MASOMO YA LUGHA NA SANAA KITAIFA.

Lisa Victoria Mindu (St. Mary Goreti), Rosalyn Tandau (Marian Girls), Joseph Ngobya (St. Joseph Cathedral), Aneth Mtenga na Idda Michael Lawenja (Marian Girls), Catherine Kiiza (St. Marys Mazinde Juu), Nancy Adon Swai (Mwika), Mohamed Salmin (Mwanza Sekondari)na Idrisa Hamis (Mwembetogwa).

SHULE 10 BORA

Alizitaja shule 10 bora kuwa ni Igowole (Iringa), Feza Boy’s (Dar es Salaam), Kisimiri (Arusha), Iwawa (Njombe), Kibaha (Pwani), Marian Girl’s (Pwani), Nangwa (Manyara), Uwata (Mbeya), Kibondo (Kigoma) pamoja na Kawawa (Iringa).

SHULE 10 ZA MWISHO

Shule zilizoshika mkia katika mtihani huo ni BenBella (Unguja), Fidal Castro (Pemba), Tambaza (Dar es Salaam), Muheza (Tanga), Mazizini (Unguja), Mtwara Tech (Mtwara), Iyunga Teck (Mbeya), Al-Falaah Muslimu (Unguja), Kaliua (Tabora) pamoja na Osward Mang’ombe (Mara).

MATOKEO YALIYOZUILIWA

Dk. Msonde alisema matokeo ya watahiniwa 150 yamezuiwa kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutolipa ada za mitihani.

“Kati ya hao, watahiniwa tisa hawakufanya kwa sababu za kiafya zilizowafanya washindwe kufanya baadhi ya mitihani, tumewapa tena fursa ya kufanya mitihani ambayo hawakuweza kuifanya kwenye mitihani itakayofanyika Mei 2015,” alisema.

Alisema pia kuwa baraza limefuta matokeo ya watahiniwa wawili kwa sababu za udanganyifu.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Matokeo haya ni mazuri. Yanatia moyo. Shule nyingi ambazo hazikujulikana sana huko nyuma zimejitokeza vizuri. Inashangaza kuona kuwa shule zile zilizozoeleka kwa kuongoza safari hii zimerudi nyuma kidogo. Hii ndiyo changamoto tunayoihitaji katika elimu. Hapa wizara inahitaji kupongezwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles