29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Jopo la usuluhishi Katiba Mpya latoa ripoti

Profesa Patrick Lumumba
Profesa Patrick Lumumba

Na Arodia Peter, Dar es Salaam

JOPO la wataalamu wa masuala ya katiba na usuluhishi wa migogoro, limesema chimbuko la matatizo yaliyojitokeza kwenye Bunge Maalumu la Katiba ni kutozingatia misingi ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Limeshauri Bunge hilo linalotarajia kuanza tena Agosti 5, mwaka huu kuheshimu Rasimu ya Katiba na kuifanya kuwa ndio msingi wa mjadala katika bunge hilo ili kunusuru mchakato huo na baadaye Tanzania iweze kupata katiba iliyo bora.

Jopo hilo linalofanyakazi chini ya Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), linaundwa na maprofesa watatu wakiongozwa na Profesa Patrick Lumumba, kutoka Shule ya Sheria ya Kenya, Bertha Koda wa Taasisi ya Taaluma na Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Gaudens Mpangala kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha Iringa.

Mbali na hilo, pia wameshauri Umoja wa vyama vinavyotetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurudi bungeni katika kikao kinachotarajiwa kuanza Agosti 5, mwaka huu na kuendelea na majadiliano kwa msingi wa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Profesa Lumumba alisema, Tanzania ni nchi ya mfano katika kulinda amani na utulivu katika nchi zote za Afrika hivyo kushindwa kupata katiba bora kunaweza kuiondolea sifa hiyo.

Profesa Lumumba ambaye alizungumza Kiswahili fasaha na mifano kadhaa, alisema jambo muhimu walilobaini katika utafiti wao ni kwamba, Watanzania wengi wanataka Katiba Mpya yenye kulinda maslahi yao.

Akitoa ripoti ya utafiti kuhusu kutofautiana kwa wajumbe na kusababisha tishio la kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya, Mwenyekiti wa JUKATA, Deus Kibamba, alisema chimbuko la matatizo hayo ni Bunge Maalumu kuibeza na kuiponda Rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Tatizo lingine alisema lilitokana na mazingira ya uzinduzi wa Bunge lenyewe, mjadala kugubikwa na lugha zisizostahili zikiwemo za matusi, kukebehiana, kubaguana na kukashifiana pamoja na upungufu katika sheria ya Mabadiliko ya Katiba hususan muundo wa Bunge Maalumu la Katiba.

Katika utafiti huo, jopo hilo limeshauri kanuni zilizopo za kuendesha Bunge hilo ziangaliwe upya ili ziweze kusaidia kuendesha vikao kwa ufanisi.

“Kamati ya Maridhiano ndani ya Bunge imeonekana kuwa na upungufu, hivyo tunashauri liundwe jopo la watu 15 nje ya bunge wanaoheshimika na kuaminika kitaifa, wanaweza kuchaguliwa kutoka makundi ya wanasiasa wastaafu, viongozi wa dini, asasi za kiraia na wanataaluma.

“Kazi yake itakuwa ni kusaidia kutatua matatizo yanayojitokeza bungeni na ambayo bunge lenyewe litashindwa kutatua,” alisema Kibamba.

Katika hatua nyingine wataalamu katika ripoti yao wameshauri Bunge la Katiba lirejee kwenye sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012, kifungu cha (37) kinachotamka wazi kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavunjwa na Rais baada ya kura ya maoni.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Napenda kuwapongeza JUkata na Bwana Kibamba hongereni sana. pamoja na Hongera hizo na kamati yako ya usuluhishi ya akina Lumumba toka Kenya ambaye mimi namfahamu pia wakati nasoma media huko lakini swali la msingi ni hili” JE RAIS KIKWETE NA WANACCM PAMOJA NA WAJUMBE WAO WAMEKUBALI KUHESHIMU RASIMU YA MAONI YA WANANCHI YALIYOSIMAMIWA NA TUME YA MZEE WARIOBA? Kama wamekubali basi Atoe tamko kwamba wamekubali kuheshimu raismu hiyo, alkini hadi sasa ni watu wa nje wanataka usuluhisho. Unajua ni sawa na kusuluhisha ugomvi katika Ndoa. Wewe hata ukiwa malaika, Askofu padre, mchungaji gani, huwezi ulazimisha watu ndoa kurudiana, wao ndiyo waamue au mmoja wao awe ameridhika kurudi na hivi kukubali kubadilika. Je, CCM wamebadilisha msimamo wao, namna nyingine ni kutwanga maji katika kinu. Ukawa wameshasema, hawana shida, ili mradi CCM wakubali kujadili rasimu iliyopo mezani, namna nyingine nanyi mnaingia katika mtego ule ule wa kuegemea upande mmoja na hivi kukosa kutenda haki. Wenye tatizo ni CCM siyo Ukawa, je Mmeongea na Rais, Spika wa Bunge la Katiba na wajumbe wa CCM? Wakikubali hao, Ukawa wamesema hawana shida, mbona mnashindwa kuona kiini cha nani kasababisha tatizo, je nanyi mnaiogopa CCM kama viongozi wa dini?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles