23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Watu 419 wahitimu mafunzo ya sensa mwanza

Na Clara Matimo, Mwanza

Watu 419 mkoani Mwanza wamehitimu mafunzo ya ukufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi ngazi ya Mkoa ambao wanatarajiwa kwenda kutoa elimu hiyo kwa makarani na wasimamizi wa sensa katika ngazi ya wilaya.

Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi mkoani Mwanza, Goodluck Lyimo, akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya wakufunzi wa sensa ya watu na makazi ngazi ya mkoa ambao wanatarajiwa kwenda kutoa elimu hiyo kwa makarani na wasimamizi wa sensa katika ngazi ya wilaya.

Wakizungumza na Mtanzania Digital baada ya kuhitimu mafunzo hayo ya siku 21 yaliyofika tamati Julai 26, 2022 yaliyofanyika katika Chuo cha Mtakatifu Augustino(SAUT) jijini Mwanza, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema wanaahidi kutoa mafunzo ya sensa ya watu na makazi kwa weledi kwa makarani na wasimamizi wa sensa ngazi ya wilaya ili yalete matokeo chanya kwa taifa kwani wanaelewa umuhimu wa zoezi hilo.

Aidha wameishukuru serikali ambavyo imerahisisha  zoezi la sensa kwani litafanyika kidigitali kwa kuwa wamejengewa uwezo katika suala zima la sensa ikiwemo uadilifu na kuelewa mambo muhimu yanayopaswa kufanyika wakati wa zoezi la sensa.

“Nina imani sensa ya mwaka huu itakuwa nzuri kwa sababu tumeambiwa ni sensa ya kidigitali hakuna makaratasi taarifa zote zitaingizwa ndani ya kishikwambi kwa hiyo naamini itafanyika kwa wakati na majibu yatatoka kwa wakati kwa sababu teknolojia iliyotumika mwaka huu ni teknolojia ya tehama, Tanzania sasa hivi ni Tanzania ya kidigitali, Tanzania ya tehama,” amesema Mwalimu Nyambui.

Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi Mkoani Mwanza, Goodluck Lyimo, amebainisha kwamba wakufunzi hao wamepata uelewa wa kutosha muda wote wa Mafunzo hayo yakiwemo utumiaji wa Madodoso yote manne ya Sensa hivyo watakuwa sehemu ya mafanikio ya zoezi hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, alisema  zoezi la sensa ya watu na makazi ni muhimu kwani litaiwezesha serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa dira ya maendeleo ya mwaka 2025 hivyo wakufunzi hao wakalete matokeo chanya kwa taifa.

“Sensa ya watu na makazi itakayofanyika Oktoba 23, 2022 itakuwa ni katika kutunga sera na kupanga mipango ya nchi yetu pamoja na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kitaifa, kikanda na kimataifa nyie mmeaminiwa na serikali katika zoezi hili muhimu lililoko mbele yetu mmepata mafunzo bora yanayotakiwa ambayo yamefuata miongozo yote ya kitaifa na kimataifa tunawategemea sana kufanikisha zoezi hili,” alisisitiza mhandisi Gabriel.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Mwanza, Julius Peter, aliwataka wahitimu wa mafunzo hayo kutumia vizuri elimu waliyoipata  kwa umakini na weledi mkubwa kwani ni heshima  kubwa kwao kuaminiwa kupata mafunzo hayo maana Mkoa wa Mwanza una watu wengi sana ambao wanasifa kama zao hivyo wakatimize lengo la serikali inayoongozwa na CCM kuhakikisha zoezi la sensa ya watu na makazi linafanikiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles