Watoto watatu waliotoweka wakutwa wamefariki dunia ndani ya gari Dar *Wengine sita wafariki dunia kwa kupigwa radi Geita

0
1250

LEONARD MANG’OHA Na HARRIETH  MANDARI-DAR/ GEITA


WATOTO watatu wa familia moja wamekutwa wamefariki dunia ndani ya  gari bovu la Toyota Mark X.

Walitoweka tangu Oktoba 15, mwaka huu  katika Mtaa wa Njaro wilayani Temeke,  Dar es Salaam.

Miili ya watoto hao, Jamila Mohamed (9), Amina Kunambi (7) na Yusuph Selemani (2) ilipatikana jana saa 4.00 asubuhi,   ndani ya gari hiyo iliyokuwa imeegeshwa kwenye gereji ya Inshallah inayomilikiwa na raia   mwenye asili ya Asia.

Miili hiyo ilipatikana  baada ya babu yao anayefanya kazi katika gereji hiyo kuhisi harufu ya mzoga hali iliyomlazimu kufanya upekuzi.

Taarifa za tukio hilo zilianza kusambaa katika mitandao ya jamii jana asubuhi ikieleza kuwa watoto hao wa familia moja walionekana wakiwa wamefariki dunia baada ya kupotea kwa siku tatu.

Akizungumza na waandishi wa habari, baba mdogo wa watoto wawili kati ya watoto hao, Kagoda Issa, alisema tukio hilo ni la kutatanisha kutokana na mazingira ya watoto hao kupotea na kupatikana kwao kughubikwa na utata.

Issa alihoji watoto hao waliwezaje kuingia katika gari hilo na kujifungia mlango kiasi cha kushindwa kutoka wakati gari hilo limeharibika kwa muda mrefu.

“Tunashindwa kuelewa waliingia vipi wakajifungia wakati hata mfumo wa milango ya gari umekufa na baadhi ya vifaa vimetolewa.

“Tunashindwa kujua kama ni kweli waliingia kucheza wenyewe au ni mtu kafanya mambo yake halafu kawatupia humu,” alisema Kagoda.

Baba mzazi wa Amina, aliyekuwa akiishi na watoto hao, Omary Thomas, alisema   watoto hao waliondoka nyumbani kwao Mtaa wa Njaro Wilaya ya Temeke saa 10:00 jioni Oktoba 15, mwaka huu kwenda kucheza.

Alisema watoto hao  hawakurejea nyumbani hadi miili yao ilipokutwa kwenye gari hilo jana asubuhi.

“Jumatatu mimi sikuwapo nilivyorudi usiku ndiyo nikapata taarifa hiyo kuwa watoto wamepotea kuanzia saa 10:00 jioni walivyoenda kucheza.

“Kwa hiyo siku hiyo tulihangaika… jana tukazunguka serikali za mitaa na kata hatukupata ufafanuzi wowote ila jana tulipigiwa simu Chanika tulivyoenda tukakuta ni mtoto mwingine tukarudi.

“Baada ya kurudi leo asubuhi nikatoka nikaenda kumfuata mama yangu mkubwa wakati narudi nikakuta taarifa tayari zimekwisha kutokea, mimi sikuwapo eneo la tukio,” alisema Thomas.

Alisema watoto hao mara kadhaa wamekuwa wakienda katika eneo hilo kucheza kwa sababu babu yao hufanya kazi katika gereji hiyo.

Mmoja wa walinzi wa gereji hiyo, Said Ngamwala, alisema jana asubuhi baada ya kukutana na kufanya kikao katika eneo hilo alitoka na kurejea baada ya muda mfupi.

Alisema  aliporudi akakutana na babu wa watoto hao ambaye wanafanya wote kazi akitoka katika gari hilo akilia kuwa ameona miili ya watoto waliokuwa wakiwatafuta ndani ya gari.

“Na mimi nilikwenda kushuhudia kama ni kweli nikaiona miili hiyo nikatoka haraka kuwaita watu wakaja pale. Muda huo huo tukawaita polisi wakaja tukajaribu kufungua mlango ukagoma nadhani ni kwa sababu babu yao aliubamiza sana ule mlango hivyo polisi wakavunja kioo ndiyo tukaweza kuitoa ile miili na tayari ilikuwa imevimba,” alisema Ngamwala.

Baadhi ya mashuhuda walitofautiana katika kauli walizozitoa kutokana na baadhi yao kudai kuwa miili hiyo imetolewa macho.

Hata hivyo,  baadhi yao walikanusha taarifa hizo wakisema kuwa walichokiona ni miili hiyo ilikuwa imevimba kwa kile walichoamini kuwa huenda ni kutokana na joto ndani ya gari hilo.

Mmoja wa mashuduha wa tukio hilo (ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini)  alisema babu wa watoto hao aliyemtaja kwa jina moja la Seif (maarufu kama Mzee Tall) alibaini kuwapo miili hiyo baada ya kuhisi harufu ya kiumbe kilichokufa pamoja na maji maji yaliyokuwa wakichuruzika kutoka katika gari hilo ndipo akaamua kufungua na kuikuta miili ya wajukuu wake.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alidai kiwa watoto hao walikwenda lindoni kwa babu yao ambako waliingia ndani ya gari na kujifungia hivyo wakashindwa kutoka baada ya milango kujifunga.

“Nikiri kupokea taarifa ya vifo vya watoto watatu wa familia moja.

“Siku ya Jumatatu mama yake na mmoja wa watoto waliofariki dunia yaani mama yake Amina Kimambi, alifika na kutoa taarifa polisi, tulipokea hiyo taarifa na tukawashauri warudi wajiridhishe ili baada ya saa 24 waje waandikshe maelezo.

“Kwa hiyo ufuatiliaji wa tukio hilo ulianza na leo saa tano kasoro tulipokea taarifa kuwa mlinzi wa ile gereji alipokuwa akikagua lindo lake alipofungua mlango wa moja ya gari lilizokuwa katika gereji hiyo alithibitisha kuwapo miili ya watoto hao,” alisema Mambosasa.

Kuhusu miili hiyo kutolewa macho Mambosasa alisema hawezi kuthibitisha hilo hadi atakapopewa taarifa ya daktari.

Alisema  macho yanaweza kuharibika kutokana na joto kali lililokuwa ndani ya gari.

Kamanda alisema jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa tukio hilo kubaini kama ni kweli watoto hao walifariki dunia baada ya kujifungia katika gari hilo.

Alisema  endapo watabaini kuwa waliuawa na kutelekezwa hatua   zitachukuliwa kumbaini aliyefanya hivyo.

WANAFUNZI SITA WAFARIKI DUNIA

Wakati huohuo, Mwandishi Wetu, Harieth Mandari kutoka Geita anaripoti kuwa vilio na simanzi, jana vilitawala mkoani Geita baada ya wanafunzi sita wa Shule ya Emaco Vision English Medium, kufariki dunia na wengine 21  na walimu wawili kujeruhiwa na radi wakati wakiwa darasani wakiendelea na masomo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,  ambaye pia ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita, Josephat Maganga, alisema tukio hilo lilitokea saa 3.00 asubuhi katika shule hiyo iliyopo  Kata ya Nyankumbu.

Aliwataja wanafunzi waliofariki dunia kuwa ni Jackiline Josephat, Christina Eric, Lydia Mwemezi, Glory  Glibert, Abdul Abdallah na Yusura Daudi.

Miili yao imehifadhiwa katika  Hospitali ya Rufaa Geita.

Ofisa Elimu Msingi Halmashauri ya Mji wa Geita, Yesse Kanyuma alisema     ajali hiyo ya radi iliyosababisha kupoteza maisha ya wanafunzi hao ni pigo kubwa.

Alisema   kwa sasa majeruhi wote wanaendelea na matibabu na afya zao zinaendelea kuimarika.

Naye  Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu (CCM),  alisema ni tukio kubwa la kusikitisha katika jimbo lake.

Aliwaomba wazazi   na taasisi zinazohusika kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki cha mvua inayoendelea kunyesha mkoani humo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here