24 C
Dar es Salaam
Saturday, October 16, 2021

Watoto 22,000 waondolewa katika mashamba ya Tumbaku

Na Allan Vicent, Tabora

Juhudi za kupambana na vitendo vya utumikishwaji watoto katika mashamba ya tumbaku zilizofanywa na miradi ya PROSPER zimefanikiwa kuokoa watoto 22,000 waliokuwa wakitumikishwa katika kazi hatarishi katika Mikoa mitatu nchini.

Hayo yamebainishwa na leo Jumanne Juni 15, 2021 na Meneja wa Mradi wa PROSPER RESET, Fredrick Malaso, katika maadhimisho ya siku ya kutokomeza utumikishwaji watoto duniani yaliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Mtakuja/Igagala no.5 kata ya Igagala wilayani Kaliua mkoani Tabora.

Amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na miradi ya PROSPER kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali katika kutokomeza vitendo hivyo kwa vipindi tofauti kati ya mwaka 2011 na 2020.

Licha ya kuokoa watoto hao aliongeza kuwa wazazi na walezi 400 walipata elimu ya kusoma na kuandika, vijana 1,600 walipewa elimu ya ufundi stadi na kaya 1,500 ziliwezeshwa mikopo na kuanzisha biashara ndogo ndogo ili kuinua uchumi wao.

Alifafanua miradi hiyo kuwa ni Prosper, Prosper Plus na Prosper Umoja ambayo ilitekelezwa katika Mikoa 3 ya Tabora, Mbeya na Songwe ambapo jumla ya wilaya tano katika mikoa hiyo ilinufaika na sasa wameanza mradi wa PROSPER REST.

“Tathmini inaonesha kupitia miradi hiyo hali ya utumikishwaji watoto katika mashamba ya tumbaku imepungua kwa zaidi ya asilimia 84.3 katika mikoa hiyo, tunapongeza kazi nzuri iliyofanyika,na sasa tunahitaji ushirikiano zaidi,” amesema Malaso.

Malaso amepongeza serikali ya wilaya na Mkoa wa Tabora kwa kutambua mchango na juhudi kubwa zinazofanywa na asasi za kiraia na kuziunga mkono katika kutoa elimu na misaada kwa wazazi na walezi wa watoto ili kupunguza umaskini.

Alieleza kuwa utafiti uliofanyika mwaka 2014 nchini (Tanzania Integrated Labor  Force Survey (TILFS) ulionesha vitendo vya utumikishwaji kuathiri watoto mil 4.2 wenye umri wa miaka 5-17 kati ya watoto mil 15  sawa na asilimia 29.3 na asilimia 94 ya matukio mengi ya utumikishwaji yanafanyika katika sekta ya kilimo.

Amebainisha kuwa mradi mpya wa PROSPER RESET utatekelezwa kwa miaka 3 katika wilaya 5 za Mikoa hiyo ambazo ni Kaliua, Sikonge na Urambo (Tabora), wilaya ya Chunya (Mbeya) na wilaya ya Songwe Mkoani Songwe.

Ametaja malengo ya mradi huo kuwa ni kuwezesha vikundi vya kuweka na kukopa (VSLA), vikundi vya vijana vya mashamba darasa (MFS) na vile vya ufundi stadi kwa kuvipa elimu ya usimamizi wa biashara na kuweka akiba.

Mkuu wa wilaya hiyo, Abel Busalama alipongeza asasi za TDFT na TAWLAE zinazofadhiliwa na Mfuko wa Eliminating Child Labour in Tobacco Growing Areas   (ECLT) na washirika wao kwa juhudi kubwa za kupinga utumikishwaji watoto katika kilimo cha tumbaku.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
161,753FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles