24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

WATANZANIA TUUNGANE KUPINGA MATUKIO HAYA

KWA wiki kadhaa sasa taifa linapitia kwenye misukosuko ya matukio ya ajabu ambayo Watanzania kwa muda mrefu hawakuyazoea.

Matukio haya, yamesababisha kuwapo na hofu kubwa miongoni mwa watu na wasijue nini hatima yake licha ya vyombo vya dola kuendelea na kazi ya kusaka wahusika.

Katika siku za karibuni mkoani Dodoma tumeshuhudia kushambuliwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na watu wasiojulikana.

Lissu akiwa ndani ya gari lake alishambuliwa kwa risasi karibu 32 na kumwachia majeraha makubwa yaliyosababisha akimbizwe nchini Kenya kwa matibabu.

Hadi sasa kumekuwapo na msamiati kuwa watu waliohusika ‘hawajulikani’, jambo hilo ndilo linaloumiza vichwa vya Watanzania wengi.

Wakati kila mtu akiendelea kukuna kichwa kuhusu tukio hili, kumeibuka tena tukio la watu wasiojulikana kuvamia ofisi za mawakili wa Kampuni ya Prime.

Hili ni tukio jingine ndani ya kipindi kifupi kabisa, baada ya ofisi za Kampuni ya IMMMA kukumbwa na uvamizi wa aina hii.

Ofisi hizi ambazo ziko karibu na ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), zimeingia kwenye rekodi ya matukio hatari, huku wimbo ule watu wasiojulikana ukiendelea kuchukua nafasi yake.

Pamoja na unyama huo, watu wasiojulikana waliamua kuichoma moto  na kuharibu nyaraka kadhaa, huku kukiwa hakuna sababu zozote za chanzo cha tukio hilo.

Katika tukio hilo, wavamizi hao waliingia kwenye chumba cha mhasibu na kuchukua Sh milioni 3.7 na kubeba kabati la kuhifadhia nyaraka muhimu za wateja wao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema mpaka sasa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku akiwataka wananchi wenye fununu kutoa taarifa.

Meja Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Vicent Mritiba naye alivamiwa juzi na watu wanaosadikiwa  kuwa ni majambazi na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kujeruhiwa kwa Meja  Jenerali ni mwendelezo wa matukio mabaya ya silaha yanayoendelea kutokea nchini.

Katika tukio hili majambazi hayo yalipora Sh milioni 5 alizokuwa amechukua benki.

Katika jambo la kushangaza ofisa huyu mstaafu wa jeshi, alijeruhiwa vibaya akiwa mbele ya geti la kuingia nyumbani kwake eneo la Ununio wakati akijiandaa kuingia ndani.

Tumelazimika kusema haya kwa sababu siku zote Watanzania hatukuwa na utamaduni wa matukio hatarishi jijini Dar es Salaam.

Kutokana na hali hii, tunavishauri vyombo vya dola hasa Jeshi la Polisi ambalo limepewa dhamana ya ulinzi wa raia na mali zake, kujipanga vizuri  na kuja na mikakati makini ambayo kwa namna moja au nyingine itasaidia kupunguza hali hii.

Pia katika jambo hili, umefika wakati sasa polisi kwa uwezo wao kuondoa neno “wasiojulikana’ maana tunaona linalipaka tope katika utendaji kazi wake wa kila siku.

Sisi MTANZANIA, tunasema umefika wakati sasa wa Watanzania kuungana kupinga na kulaani matukio haya kwa nguvu zote kwa sababu si utamaduni wetu.

Tunasema hivyo, kwa sababu inawezekana  kuna sehemu tumekosea, kwa msingi huo hatuna budi kurudi kwenye mstari. Ni aibu kuendele kusikia matukio ambayo hayana tija kwa maendeleo ya Taifa, zaidi ya kuongeza hofu kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles