31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI IWASAKE WAHALIFU WANAOCHAFUA SIFA YA NCHI

Na PATRICIA KIMELEMETA

HIVI karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali ya uhalifu ambayo yanahatarisha maisha ya watu na mali zao, huku mengine tayari yakiwa yamesababisha mauaji ya watu wasio na hatia.

Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na kuuawa kwa askari polisi wanane waliokuwa kwenye gari wakitoka doria katika Kijiji cha Jaribu kilichopo Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, ambapo gari walilokuwa wamepanda lilishambuliwa na watu wasiojulikana na kusababisha vifo vya askari hao.

Tukio lingine ni pamoja na kuuawa kwa askari polisi wengine wawili kikosi cha usalama barabarani waliokuwa wakitekeleza majukumu yao katika wilaya hiyo.

Lakini pia katika maeneo hayo kumekuwepo na matukio ya mara kwa mara ya mauaji ya watendaji wa vijiji katika Wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji yanayofanywa na watu wasiojulikana, hali iliyosababisha wakazi wa maeneo kuishi kwa wasiwasi.

Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini lililazimika kuunda kanda maalumu ya kipolisi katika Wilaya ya Kibiti, ambayo pamoja na mambo mengine wamelenga kuimarisha ulinzi na usalama kwa wakazi wa eneo hilo.

Kuanzishwa kwa kanda hiyo kumesaidia kupunguza vitendo vya mauaji kutokana na watu wanaodaiwa kutekeleza vitendo hivyo kukamatwa na wengine kuuawa wakati wa majibizano ya risasi.

Licha ya Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujiepusha na vitendo vya uhalifu, lakini mpaka sasa vitendo hivyo vimeendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Miongoni mwa tukio la kushtukiza ambalo lilitokea Alhamisi iliyopita ni lile la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, kiongozi huyo alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na baadaye kukimbizwa Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya matibabu zaidi.

Juzi tena Meja Jenerali Mstaafu, Vincent Mritaba, alishambuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Tukio hilo lilitokea nyumbani kwake Ununio jijini Dar es Salaam, ambapo alishambuliwa katika maeneo ya mkononi, tumboni na kiunoni na kusababisha kukimbizwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo (GMH) kwa ajili ya matibabu.

Kuongezeka kwa matukio ya mauaji kwa kutumia silaha huku watu wanaodaiwa kufanya hivyo wakiwa hawajulikani, inaleta maswali mengi yasiyokuwa na majibu.

Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi linapaswa kuwasaka na kuwakamata watu wanaodaiwa kutekeleza vitendo hivyo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Lakini bila kuwakamata, hali hiyo inaweza kusababisha wahalifu wengine kuendeleza matukio hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles