29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

UDHIBITI UBORA WA MAZAO SULUHISHO LA USALAMA WA CHAKULA

Na ISMAIL NGAYONGA

USALAMA wa ubora wa chakula na ulinzi wa afya za walaji ni miongoni mwa masuala ya kimsingi yaliyopewa kipaumbele katika ngazi za kitaifa na kimataifa, kwa kuwa magonjwa yatokanayo na chakula yanaelezwa kuwa ni chanzo cha vifo vingi duniani.

Milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu na homa ya matumbo pamoja na vifo vitokanavyo na magonjwa hayo ni mambo ambayo yamekuwa yakiripotiwa kuiathiri jamii yetu katika suala la usalama wa chakula.

Masuala ya usalama na ubora wa chakula yana uhusiano wa moja kwa moja na akiba ya chakula, hii ni kutokana na kwamba, iwapo chakula kitabainika kutokuwa salama na bora, itakuwa na madhara.

Hapa nchini, zipo taasisi zinazohusika na masuala ya usalama na ubora wa chakula, ikiwamo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambazo zilianzishwa kwa ajili ya majukumu ya kisheria ya kutoa huduma za udhibiti wa ubora wa chakula na bidhaa nyingine.

Pamoja na kutambua umuhimu wa usalama na ubora wa chakula na mahusiano yake katika suala zima la chakula nchini, ziko tetesi kwamba, kwa sasa bado wakulima nchini ambao ndio wazalishaji wakubwa wa chakula hawajui wala hawajanufaika vya kutosha na jitihada za kitaifa na za taasisi husika katika usalama na ubora wa chakula.

Kwa kutambua hivyo, Serikali ilianzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP), ili kuhakikisha kuwa wakulima wanaelimishwa kuhusiana na masuala ya usalama wa chakula.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, anasema wizara hiyo kwa kushirikana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) na halmashauri za wilaya imetoa mafunzo kwa maofisa ugani 180 katika Wilaya za Kondoa, Chemba, Mufindi, Kilolo, Kilombero, Mbalizi na Mpwapwa kuhusu athari na mbinu za kudhibiti sumu kuvu.

Dk. Tizeba anasema Serikali imeendelea kudhibiti nzi waharibifu wa matunda kwa kutoa mafunzo na usambazaji wa kuvutia wadudu aina ya Methyl eugenol (ME), ambapo kiasi cha lita 105 ziligawiwa katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Morogoro, kwenye vituo vya Utafiti vya Kilimo vya Naliendele, Kibaha na Mikocheni.

Anasema Serikali imeendelea na ukaguzi wa usafi wa mimea na mazao katika vituo vya ukaguzi vya sehemu ya afya ya mimea vilivyoko katika viwanja vya ndege, bandari na mipakani, ambapo hadi kufikia Machi mwaka huu, tani 776,379.16 za mimea na mazao zilikaguliwa na kusafirishwa nje ya nchi.

Aidha, Dk. Tizeba anasema Jumla ya tani 597,837.33 za mimea/mazao zilikaguliwa na kuingizwa nchini, vyeti 8,736 vya usafi wa mimea kwa ajili ya kusafirisha mazao nje ya nchi na vibali 1,232 vya kuingiza mazao na mimea nchini vilitolewa, ambapo jukumu hilo limewezesha biashara ya mazao ya kilimo kukidhi masharti ya soko la kikanda na kimataifa.

“Pia zoezi la ukaguzi wa maduka ya pembejeo za kilimo lilifanyika, ambapo lita 14,671 za viuatilifu visivyo na ubora vilikamatwa na kuhifadhiwa ili kusubiri taratibu za uteketezaji, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kufunga baadhi ya maduka ya wafanyabiashara waliohusika na kuuza viuatilifu vilivyo chini ya ubora na ambavyo havijasajiliwa.

Akifafanua zaidi, Dk. Tizeba anasema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wakulima ili kubaini milipuko na jinsi ya kudhibiti na itaendelea kuimarisha vituo vya ukaguzi vya mipakani ili kudhibiti mazao yanayosafirishwa na yanayoingia nchini pamoja na kuimarisha kituo cha kudhibiti milipuko cha KILIMO ANGA, ili kutoa huduma bora ya udhibiti wa milipuko ya visumbufu vya magonjwa ya mazao na mimea.

Pamoja na utoshelevu wa chakula uliopo nchini kwa sasa, ni vyema kwa taasisi binafsi na mashirika ya kimataifa yakaendelea kutoa elimu kwa wakulima, uhifadhi wa chakula hicho ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele kwa kuzingatia kuwa, wakulima wengi wanamwaga mazao ya chakula kama mahindi chini kwa ajili ya kuyaanika na baadaye kuhifadhiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles