26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

WATAALAMU WAELEZEA MTI ULIOZUA SINTOFAHAMU

Na GRACE SHITUNDU – DAR ES SALAAM          |         


TAASISI ya Utafiti ya Misitu nchini (TAFORI), imelazimika kuitoa hofu jamii kuhusu mti aina ‘Terminalia Catappa’, ambao katika siku za hivi karibuni baadhi ya watu walianza kuukata kwa kasi, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa na mikosi na hata kusababisha vifo iwapo umeupanda au kuota katika makazi yako.

TAFORI imelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kipande cha video chenye sauti ya mtu anayejiita Mtume Vicent Mkalla wa Kanisa la Victory Faith Church, kueleza madhara ya mti huo alioubatiza jina la ‘mti mfarakano’ au ‘chonganishi’ kuzua sintofahamu.

Mtume huyo alidai mti huo wenye jina la Kigiriki na Kirumi, likimaanisha uume au sehemu za siri za mwanamume, ni mti unaoa na kutawala.

Kwamba mahali popote ambako mti huu umepandwa, huleta majanga mbalimbali, ikiwamo wanandoa kufarakana, zaidi husababisha vifo vya mapema, hususani kwa akina baba au watoto wa kiume, huleta ugumu wa kifedha, madeni na magojwa ya kushtukiza.

Kutokana na kauli hizo, TAFORI imewasihi viongozi wa kijamii na kidini kuacha hulka ya kutafuta umaarufu kwa kutoa taarifa zisizo rasmi na zenye kupotosha jamii, zinazohusisha viumbe na majanga, ikiwamo miti.

Ufafanuzi wa TAFORI umekuja katika wakati ambao baadhi ya watu wamekata na wengine wameendelea kuukata mti huo ambao wengi walipenda kuupanda kutokana na kutoa kivuli.

Mkurugenzi wa TAFORI, Dk. Revocatus Mushumbusi, alisisitiza miti hii ising’olewe kwa kisingizio cha imani potofu kwani haina madhara yanayoelezwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Kuna aina zaidi ya 100 za miti aina ya Terminalia hapa duniani na yote haina madhara yanayotajwa katika taarifa ambazo si rasmi zinazozunguka katika mitandao ya kijamii.

“Hata hivyo, mti unaolaumiwa na kuhusishwa na imani potofu, umetajwa kwa jina la kisayansi kama Terminalia Catappa ‘Mkungu’ japo picha zinazozungushwa kwenye mitandao ya kijamii ni picha za mti unaoitwa kwa jina la kisayansi kama Terminalia Mantaly ‘Panga uzazi’,” alisema.

Alisema aina zote mbili yaani Mkungu ‘Terminalia Catappa’ na Panga Uzazi ‘Terminalia Mantaly’ inafaa kwa bustani na kuboresha mandhari.

Alisema miti ya Mkungu ‘Terminalia Catappa’ inapatikana kwa asili katika sehemu zenye joto la kiasi katika pwani za Bara la Asia, ingawa imepandwa maeneo mengi katika bara la Afrika, hasa karibu na maeneo ya Pwani yenye mwinuko usiozidi meta 600 juu ya usawa wa bahari.

Kwa upande wa miti aina ya Panga Uzazi ‘Terminalia Mantaly’ alisema imepandwa kuanzia uwanda wa chini kiasi hadi maeneo yenye miinuko na baridi kama yale yanayozunguka milima ya Tao la Mashariki mwa Tanzania.

“Aina hizi mbili za miti ya Terminalia zina tofauti kubwa, Mkungu ‘Terminalia catappa’ ikiwa na majani mapana, wakati Panga Uzazi ‘Terminalia Mantaly’ majani yake ni madogo.

“Na pia ‘Terminalia Catappa’ inazaa matunda makubwa yanayoliwa na wanadamu na sehemu nyingi za Tanzania mti huu umejulikana kama Mkungu, maana unazaa kungu na haujawahi kujulikana kama mti chonganishi sehemu yoyote duniani. Kwani sehemu za Asia ambako mti huu unapatikana kwa asili, unajulikana kama India almond au Sea almond, yaani Mkungu wa India au Mkungu wa sehemu za bahari,”alisema

Alisema jina la mti ‘Terminalia catappa’ halina uhusiano na sehemu za siri za mwanamume, kwani sehemu ya kwanza ya jina hili, yaani ‘Terminalia’ inatokana na neno la Kilatini ‘Terminus’ linaloleta neno la Kiingereza Terminal, yaani ya mwishoni, cha mwishoni, mwishoni, ikimaanisha kwamba majani yake yamekusanyika mwishoni mwa tawi au kijitawi.

Kwamba sehemu ya pili ya jina yaani ‘Catappa’, inatokana na neno Ketapang kwa lugha ya Maleshia (Malay), likimaanisha mti wenye mbegu zinazotumika kutengezea dawa.

“Na sehemu nyingi za Asia, ikiwemo mitaa, viwanja vya ndege, watu, wamepewa jina hili la Ketapang, likiwa na maana nzuri tu kwa lugha ya Kimaleshia,” alisema.

Akizungumzia umuhimu wake, alisema miti ya Mkungu ‘Terminalia Catappa’ inafaa kwa matumizi mbalimbali, magome yake na majani hutumika kuweka rangi nyeusi kwenye ngozi, mbao yake ni nzuri na hutumika kwa kutengenezea boti na ujenzi wa nyumba, mbegu zake huliwa na zinatoa mafuta yasiyo na harufu ambayo hutumika kutibu uvimbe tumboni na yakichemshwa na majani yake hutibu magonjwa mengi ya ngozi.

“Tunda lake huliwa, tena lina harufu nzuri japo kwa sababu ya nyuzi nyuzi nyingi halipendelewi sana na watu wengi, hupandwa zaidi kama mti wa kupendezesha mandhari kwenye miji na bustani kwani una matawi yanayosambaa kwa mlalo na majani yake ni mapana, hivyo hutoa kivuli kizuri.

“Mizizi ya mti huu husambaa kwa mlalo ili kuweza kushikilia mti usianguke, hivyo kama ilivyo kwa miti mingine mingi, si vyema kuipanda karibu sana na nyumba kwa hofu ya kuleta nyufa kwenye majengo dhaifu,” alisema.

Alisisitiza wananchi wafanye kazi ili kuboresha hali ya maisha yao na mazingira, lakini sio kusingizia viumbe asili kama chanzo cha majanga na matatizo yao ya kiuchumi na kijamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles