24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JINSI MBINU ZA KIJASUSI ZILIVYOMPAISHA GINA KUONGOZA CIA

NA MWANDISHI WETU, MITANDAONI        |        


SHIRIKA la Kijasusi la Marekani, CIA la mjini Virginia, limeandika historia mpya ya kuongozwa na mwanamke, Gina Haspel, mwenye umri wa miaka 61.

Hii ni taswira ya kwanza ya mwanamke huyu ambaye amejikita kwenye kazi ya ujasusi kwa zaidi ya miaka 33. Hatua hiyo ni miongoni mwa sifa zilizomfikisha Gina kuwa mwanamke wa kwanza kuliongoza Shirika hilo.

Jasusi huyo mwanamke amepata kulihudumia Taifa lake katika masuala mbalimbali aliyopangiwa na sasa amethibitishwa na Bunge la Seneti kuwa Mkurugenzi Mkuu wa CIA na baadaye kula kiapo cha utiifu.

Kuthibitishwa Gina kuwa bosi wa CIA kumekuja baada ya mapambano ya kisiasa ndani ya shirika hilo, ambayo yalifanyika gizani katika historia ya maisha yake. Gina anasifika kama ‘chuma’ baada ya kuongoza kikosi cha kuwahoji watuhumiwa wa matukio ya ugaidi wanaohusishwa na kundi la Al Qaeda.

Matumizi ya mbinu za ukatili, utesaji yaliyofanywa na CIA yanamhusisha moja kwa moja na Gina. Mbinu za kuwaweka watuhumiwa kwenye maji, kuwakosesha usingizi, kuwapiga na kila aina ya ubabe zilitumika kupata siri za Al Qaeda.

Wakati akithibitishwa kuwa Mkurugenzi wa CIA, Gina alikataa kuelezea lolote kuhusu nafasi yake baada ya tukio la kigaidi la Septemba 11, 2001.

Itakumbukwa kuwa Septemba 11, 2001, Gina alitakiwa kuripoti makao makuu ya CIA kwa madhumuni ya kupangiwa kazi nyingine baada ya kurejea kutoka kwenye mojawapo ya operesheni za siri nje ya Marekani.

Hata hivyo, siku hiyo lilitokea shambulizi la kigaidi katika Kituo cha Kimataifa cha Biashara, World Trade Center, ambalo lilibadilisha kabisa mwelekeo wa majukumu mapya aliyotarajiwa kukabidhiwa na Shirika hilo. Kazi yake ilibadilika upesi mno. Hapo ndipo vita dhidi ya ugaidi ilipoanzia.

Katika mahojianao na gazeti The Economic Times la India, Gina alipata kusema; “Nilifahamu akilini mwangu mara nilipotazama video ya ndege ya kwanza ikishambulia jengo la WTC kule Manhattan, ilikuwa kazi ya Bin Laden.

“Niliinuka kutoka mezani kwangu kama watu wengine, nikatembea kuelekea idara ya kupambana na ugaidi ili kutoa msaada wanaohitaji. Sikuwahi kwenda likizo kwa muda wa miaka mitatu”.

Gina alikataa pia kueleza lolote kuhusiana na gereza la siri lililopo nchini Thailand ambako watuhumiwa waliohusishwa na kundi la Al Qaeda, Abu Zubaydah na Abd al-Rahim al-Nashiri, waliwekwa kwenye mabwawa na kuteswa usiku kucha huku wakikoseshwa usingizi.

Uteuzi wa Gina kuwa mkurugenzi na mwanamke wa kwanza wa CIA, ulifanikiwa baada ya kupigiwa kura ya ndiyo na maseneta 54, wakati kura za hapana zilikuwa 45, idadi ya wapigakura ilikuwa maseneta 100.

Mwanamama huyo alikabiliwa na upinzani mkubwa wakati wa kunadiwa, hususan hali ya nasaba yake na CIA na mbinu zake za namna ya kuhoji watuhumiwa zilivyokuwa za kipekee.

Gina anatajwa kuwa msimamizi wa gereza moja la siri lililoko nje ya Marekani ambako watuhumiwa wa ugaidi walikuwa wakizamishwa katika kina cha maji, wengi huona kama mateso makubwa.

Seneta wa Chama cha Republican John McCain, ni miongoni mwa watu waliokumbana na mateso ya namna hiyo kipindi alipokuwa akiteswa kwa miaka mitano kwenye jela mojawapo nchini Vietnam.

McCain alipopata fununu za uteuzi wa Gina aliupinga uteuzi huo bila kusita na kusema haukuwa wa afya njema kwa Taifa hilo, lakini Bunge la Seneti limemwidhinisha rasmi na sasa ndiye mtendaji mkuu wa CIA.

Miongoni mwao seneta wa Virginia, Mark Warner, anamuelezea Gina kuwa aliwahi kumwambia kwamba Shirika hilo halipaswi kutumia mbinu kama hizo tena, na kuahidi yeye binafsi kutorudia hata kama Rais wa Marekani, Donald Trump, ataamuru zitekelezwe.

Warner anasema anaamini misimamo ya Gina kwamba anaweza kusimamia kauli zake hata kama Rais Trump ataamuru.

“Yeye hana hofu ya kusema ukweli kwa mamlaka za juu endapo amri zinaweza kuwa haramu ama uovu ndani yake hasiti kukataa kutekeleza na endapo atakubali amri hizo, basi kwake itakuwa ni sawa na kurejea kwenye utesaji,” anasema Warner.

Kabla ya zoezi la upigaji kura, maseneta wengi walifahamu mambo hayo pekee kumhusu Gina. Hata hivyo, inaonyesha mwanamama huyo ni mtu wa ndani wa CIA na ameshiriki kwenye operesheni nyingi tata.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Bunge la Seneti ya mwaka 2014, inasema mwaka 2002 Haspel alichaguliwa na CIA kuongoza kitengo kilichoitwa “Black Site” huko nchini Thailand, mahali ambako mbinu za mahojiano ya kikatili, utesaji na kuwakosesha usingizi watuhumiwa zilitekelezwa. Bunge la Seneti liliona mbinu hizo ni mateso makali kuliko inavyotakiwa.

Inabainisha kuwa, mtuhumiwa Abd al-Tahim al Nahiri alipelekwa katika kitengo cha Black Site, inadaiwa kuwa alitendewa ukatili uliopindukia kwa kutumia njia ambazo zilipigwa marufuku baadaye na Rais Barack Obama.

Al-Nashiri, ambaye alifanyiwa mahojiano baada ya Gina kuchukua nafasi hiyo, anasema aliamuru kupewa adhabu ya kutopata usingizi, kudhoofishwa kwa kila hali, kuachwa utupu, kuwekwa mahali penye joto kali, kuwekwa kizuizini kwenye boksi dogo hata kupigizwa ukutani mara kwa mara.

Miaka mitatu baadaye siri hizo zilivuja, hali ambayo ilimlazimu Gina kuamuru kuharibiwa kwa mikanda ya video 92 ambazo ndani yake alionekana akifanya mahojiano hayo na watuhumiwa wa ugaidi Al-Nashiri na Abu Zubaydah, huku akionekana kushikiliwa mahali fulani nchini Thailand.

Aidha, ripoti ya Bunge la Seneti ya mwaka 2014 inaeleza kuwa, takribani wanaume 119 walipitia mateso makubwa baada ya shambulio ya majengo pacha na Wizara ya Ulinzi ya Marekani la mwaka 2001.

Vikundi vya kutetea haki za binadamu vimeonyesha wasiwasi mkubwa tangu uteuzi wa Haspel ulipothibitishwa. Vikundi hivyo vinasema Gina ameondoka nchini Thailand kwenda nchini Marekani, kuendeleza mateso zaidi, lakini haijulikani ni jukumu gani alilitekeleza kiasi cha rekodi yake halisi kutambuliwa na CIA.

Hata hivyo, inaarifiwa kuwa, Rais Trump amesema Marekani itaendelea na mbinu hizo hizo za kumfunga mtuhumiwa wa ugaidi kitambaa usoni, akiwa amelala kwenye ubao na kutupwa kwa kasi kwenye kina cha maji huku mtu huyo akiwa ametanguliza kichwa.

Yapo maswali kadhaa yameibuliwa, miongoni mwa maswali hayo ni pamoja na kutaka kujua kuwa ni kweli Gina alitesa watuhumiwa?

Swali hili ni gumu kwa kila mmoja anayefuatilia visa na mikasa ya kijasusi ya shirika la CIA na mengineyo duniani. Lakini lililo muhimu ni kwamba, katika mfumo wa madaraka yeye ndiye mtu anayetakiwa kutoa taarifa za kitengo chake, hivyo yote yaliyofanyika iwe kwa agizo lake moja kwa moja au wataalamu waliofanya hivyo kama njia ya kupata ukweli, basi anatakiwa kuwatetea. Kama inavyosemwa madaraka ya pamoja ndiyo msingi wa kuendesha taasisi yoyote, hivyo Gina anahusika moja moja.

Mathalani Machi 15, mwaka huu kabla ya uteuzi wa Haspel, Mkuu wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA), Michale Hayden, amethibitisha habari kwamba, Gina amehusika na utesaji dhidi ya watuhumiwa na washukiwa wa ugaidi.

Hayden aliyasema hayo katika mahojiano na Televisheni ya CNN ya nchini humo kuhusiana na kuhusika kwa Gina katika vitendo vya utesaji wa kutisha dhidi ya watuhumiwa na washukiwa wa ugaidi, sambamba na kuthibitisha suala hilo, amedai kwa kusema, haifai kuwalaumu watu waliotenda vitendo hivyo katika kutekeleza majukumu yao.

Inaelezwa mara kadhaa Gina alitoa amri ya utesaji dhidi ya watuhumiwa na washukiwa wa ugaidi katika jela ya Thailand.

Historia fupi ya Gina Haspel

Uteuzi wa Gina Haspel ulitangazwa na Rais Donald Trump Machi na kuthibitishwa Mei, mwaka huu. Hii ni historia ya kwanza kwa mwanamke kuongoza CIA.

Gina amechukua nafasi iliyoachwa na Mike Pompoe, ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani baada ya kufukuzwa Rex Tillerson. Gina anakuwa mkuu wa pili kuongoza CIA, akitokea kitengo cha operesheni. William Colby alikuwa wa kwanza kuteuliwa kuwa mkuu wa CIA akitokea kitengo cha operesheni mwaka 1973.

Alijiunga na CIA mwaka 1985. Amewahi kuwa mkurugenzi wa vitengo mbalimbali vya ujasusi, ikiwamo cha kupambana na ugaidi kilichokuwa chini ya Jose Rodriguez.

Jina lake kamili ni Gina Cheri Haspel. Alizaliwa Oktoba 1, 1956, huko Ashland, Kentucky. Baba yake alikuwa mwanajeshi wa Jeshi la Anga la Marekani.

Elimu yake ya sekondari na chuo kikuu aliipata nchini Uingereza. Alianza kusoma Chuo Kikuu cha Kentucky kwa miaka mitatu na baadaye kumaliza mwaka wa mwisho katika Chuo Kikuu cha Louisville, ambako alihitimu Shahada ya Sanaa katika Lugha na Uandishi.

Kuanzia mwaka 1980 hadi 1981, alikuwa mratibu wa Maktaba ya Fort Devens huko mjini Massachusetts. Mwaka 1982 alitunukiwa cheti cha mafunzo ya awali ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Northeastern.

Operesheni alizoshiriki

Tangu alipojiunga na CIA mwaka 1985 Gina ameshiriki operesheni tofauti kama jasusi wa shirika hilo katika nchi mbalimbali. Operesheni ya kwanza aliyopangiwa kufanya ilikuwa nchini Ethiopia, Uturuki na Eurasia kutoka mwaka 1987 hadi 1989. Kisha alifanya operesheni nyingine Ulaya na Eurasia kuanzia mwaka 1990 hadi 2001.

Kuanzia mwaka 1996 hadi 1998 alikuwa Mkuu wa Kituo cha Ujasusi cha Marekani mjini Baku, nchini Azerbaijan. Kila sehemu aliyopelekwa alikuwa mkuu wa kituo. Kuanzia mwaka 2001 hadi 2003 alitajwa kama naibu mtendaji wa kikosi cha kupambana na ugaidi. Kati ya Oktoba na Desemba mwaka 2002 alikabidhiwa dhima ya kuongoza gereza la siri la CIA liitwalo Green.

Gina analo jina la siri la kijasusi, anaitwa ‘Jicho la Paka’ (Cat’s Eye). Kuanzia mwaka 2004 hadi 2005 alikuwa naibu mtendaji wa idara ya rasilimali watu CIA. Baadaye mwaka 2009 alihamishiwa kituo cha CIA cha jijini London, na mwaka 2011 alipelekwa New York.

Maisha binafsi

Gina Haaspel aliwahi kuolewa na mwanajeshi Jeff Haspel mwaka 1976, hata hivyo mwaka 1985 walitalikiana. Gina hatumii mitandao ya kijamii. Hadi sasa hajaolewa tena na hana mtoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles