25.1 C
Dar es Salaam
Saturday, December 9, 2023

Contact us: [email protected]

WASAMEHE WAZAZI WAKO ILI UOKOE KIZAZI CHAKO

Na Christian Bwaya,

WIKI iliyopita tuliona kwa kifupi uhusiano uliopo baina ya tabia za wazazi na zile za watoto wao. Kwamba mara nyingi tunajikuta tukifanya mambo tusiyoyapenda ambayo yakichunguzwa yanaonekana kufanana na yale tuliyoona yakifanywa na wazazi wetu.

Aidha, tuliona pia kuwa kwa kiasi kikubwa matukio yanayotutokea katika umri mdogo yana nguvu ya kuamua mustakabali wetu wa kitabia kama watu wazima. Ndio maana watu huwa na vijitabia fulani ambavyo hata kama hawavipendi bado hawana uwezo wa kuviacha.

Yale unayoyafanya mzazi, yanaweza kuwaambukiza wanao tabia fulani fulani zinazoweza kuwasumbua kuachana nazo mara watakapokuwa watu wazima.

Katika makala haya tunapendekeza namna tunavyoweza kukata mzizi wa tabia zinazoendelezwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine kwa kuwasamehe wazazi wetu.

Wasamehe wazazi wako

Huenda wazazi wako walifanya vitu usivyovipenda. Pengine walikuwa na tabia ya kutukanana mbele yako ukiwa mtoto. Uliumia kama mtoto. Ukafikiri imeishia hapo. Lakini unapotazama maisha yako sasa hivi ukiwa mzazi, unagundua na wewe unafanya hayo hayo yaliyokuumiza. Huoni shida, kwa mfano, kumkosea nidhamu mwezi wako mbele ya watoto wako kama alivyofanya mzazi wako.

Mahali pa kuanzia katika kushughulikia tatizo hili, ni kuwasamehe wazazi wako kwa yale yote waliyoyafanya pengine bila kujua. Hawakufahamu kuwa yale waliyoyafanya mbele yako yangechangia kukufanya vile ulivyo. Walifikiri ulikuwa mdogo kuweza kuelewa.

Pengine walikuchapa wakiamini kwa kufanya hivyo walikuwa wanakusaidia kujenga tabia njema. Hawakujua kuwa kukuchapa kulikufundisha mazoea mabaya ya kutumia nguvu katika kutatua matatizo yako. Fimbo walizokucharaza zilitengeneza kisasi usichokitambua ndani yako. Ndio maana na wewe umekuwa mwepesi kutumia fimbo kama namna ya kuwaadabisha wanao.

Unahitaji kuondoa kisasi hicho kilichojiumba ndani yako. Namna moja wapo ya kukusaidia kushughulika na kisasi hicho ni kuamua kwa dhati kuwasamehe wazazi kwa makosa yao.

Mara nyingi vijana wametembea na visasi mioyoni mwao bila kujua. Pengine, wakiwa watoto waliomba fedha kwa wazazi wao na kujibiwa bila staha. Akili zao zilihifadhi uchungu wa hisia za kunyimwa mahitaji yao. Leo wakiwa watu wazima wanajikuta wakiwa wazito kuwasaidia watoto wao wenyewe. Wanatamani watoto wao waonje ugumu kama ule walioupitia wao.

Kwa kawaida, ni rahisi kufikiri kwa sababu wewe ulipitia malezi fulani basi na mwanao analazimika kupitia njia ile ile uliyopitia wewe. Unaona kama kumfanya apate wepesi ni kumpendelea isivyo haki. Akili inaamini kumpa mtoto haki ambayo wewe hukuipata ni kumpa asichostahili. Hali hii ya kumnyima mwanao yale anayoyastahili kwa sababu tu pengine wewe hukuvipata ndiyo inayoitwa kisasi.

Wakati mwingine kinyume chake hutokea. Tunajikuta tukifanya kinyume na mabaya yaliyofanywa na wazazi wetu. Kwa mfano; inawezekana leo wewe kama mzazi hujali kufuatilia kile anachokifanya mtoto. Unamwacha awe huru kupindukia kwa sababu tu hukupenda namna wazazi wako walivyokubana enzi za ujana wako. Sasa hivi ukiwa mzazi, unajikuta ukimpa mtoto uhuru holela unaoweza kumletea matatizo.

Inawezekana pia umekuwa mpole kupindukia. Hukupenda ukali wa wazazi wako. Matokeo yake watoto wanaweza kufanya makosa yanayostahili adhabu lakini ukawa mzito kuwaadhibu. Ukimya wako unaweza kumshangaza hata mzazi mwenzako. Lakini kumbe unafanya hivyo kwa sababu hujamsamehe mzazi wako aliyekuadhibu kwa kufanya yasiyofaa.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles