24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Warioba, CCM jino kwa jino

Jaji Joseph Warioba
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba

NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka tena na kumshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuwa anatumia mchakato wa Katiba kama mradi binafsi wa kujitafutia maisha, historia na heshima mbele ya jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, alimshutumu Warioba na wajumbe wake kwa kutoa lugha zisizo na staha, chuki, dharau na kejeli dhidi ya Rais Jakaya Kikwete.

Alisema Warioba na wenzake katika mdahalo uliofanyika Jumatatu iliyopita jijini Dar es Salaam, walitumia muda mwingi kuitupia lawama CCM.

Alisema si mara ya kwanza kwa Jaji Warioba na wenzake kujitafutia umaarufu kwa kutojenga hoja, na badala yake kutumia lugha zisizokuwa na staha kwa kiongozi mkuu wa nchi.

“Jaji Warioba amekuwa akifanya hivyo kupitia midahalo mbalimbali hali ambayo ameiendeleza, wajumbe wenzake walitumia muda mwingi kujaribu kupotosha umma na kuwashambulia wale walio na mitazamo tofauti na wao,” alisema Nape.

Alisema inaonekana kuna baadhi ya wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Jaji Warioba waliofanya mchakato huu kuwa mali yao kiasi cha kufanya kila jitihada za kuhakikisha wanajitengenezea hatimiliki ya Katiba hiyo.

Hata hivyo, alisema ameshtushwa na mabadiliko yaliyoonyeshwa na Jaji Warioba na wenzake ambao awali walikuwa wakitumia takwimu kutetea hoja ya Serikali tatu.

Alisema Jaji Warioba na wenzake wanahama na kusisitiza kuwa waliingiza maoni ya Serikali tatu kutokana na busara zao.

“Kinachonisikitisha zaidi ni namna ambavyo wanatumia msimamo mkali usiokubali kusikiliza na kutoa nafasi kwa wale wenye mawazo tofauti na yao.

“Badala yake wanatumia juhudi kubwa kuwalazimisha Watanzania kukubaliana na mawazo yao hata kama yanaipeleka nchi pabaya.

“Kwa sasa wazee hawa wameonyesha hasira kwa kutumia kauli za dharau na kejeli kwa Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.

“Wamekuwa wakitumia lugha kali na hata za vitisho kwa uzee wao kama walivyofanya katika mdahalo uliopita kwa kuwasema wale wote wenye mtazamo tofauti na wao,” alisema Nape.

Alisema Rais Kikwete si kiongozi pekee aliyetoa mawazo na ushauri katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba.

Nape alisema wapo hata marais wastaafu ambao walitoa maoni yao kwa njia ya ushauri kwa kutoa tahadhari.

Kwamba Rais ana wajibu kwa taifa na kwa Watanzania kuhakikisha wanapata Katiba bora.

Alisema Rais na viongozi wengine kwa nafasi zao na katika vikao vyao wanayo haki kama ile waliyokuwa nayo wajumbe wa tume kutoa maoni yao, ikiwamo kuunga mkono, kupingana, kuboresha au hata kupendekeza mabadiliko katika rasimu.

“Haki hii inatolewa katika Katiba yetu na imefafanuliwa kwenye sheria ya mchakato wa Katiba na ipo wazi katika kanuni za Bunge Maalumu la Katiba,” alisema Nape.

Alisema CCM ina haki na wajibu sawa na vyama vingine, asasi mbalimbali na watu binafsi katika kukosoa na kutoa maoni.

Nape alisema anashangazwa na namna ambavyo wajumbe wamekuwa wakikiandama chama hicho juu ya mtazamo wake.

“Hatuoni sababu za msingi za tume kukishambulia na kukisakama chama chetu kwa kufanya uchambuzi na kutoa maoni yake kwa kuzingatia Katiba yake, sera zake na ilani yake,” alisema.

Alisema tume ilipewa uhuru wa kutosha bila kuingiliwa katika kazi yake na ndiyo maana wakafikia walipofika, na hata pale waliposhauriana na Rais wakiwa na mawazo tofauti na yake, bado hakuwaingilia kwani aliahidi kuwapa uhuru wa kutosha.

Nape aliwataka wajumbe kutambua kazi yao imekwisha na hawapaswi kutumia mgongo wa tume kuwapotosha Watanzania.

Alisema kama ambavyo wadau wengine waliwavumilia wakati wanatimiza wajibu wao, nao wana kila sababu ya kuwa wavumilivu.

“Ni muhimu tukumbuke Katiba ni tunda la maridhiano, na ili maridhiano yapatikane ni muhimu kuvumiliana na kuheshimu mawazo au maoni tofauti yanayotolewa na pande zote,” alisema Nape.

Alitaka mchakato wa Katiba utumike kama baraka na fursa ya kuijenga nchi na si kuibomoa kwa kupandikiza chuki na mifarakano.

“Utanzania wetu na Tanzania yetu ni ya thamani kuliko matamanio ya mioyo yetu na heshima zetu, tuvitendee haki vizazi vyetu baada ya wazee wetu kufaidi matunda ya Mungano… vizazi vijavyo vina haki ya kuyakuta matunda haya. Tusiwanyime haki hii,” alisema Nape.

JAJI WARIOBA

Jaji Warioba alipotafutwa na MTANZANIA kuhusu tuhuma hizo, alisema hawezi kusema chochote hadi apate taarifa rasmi iliyotolewa na Nape.

“Leo (jana) siwezi kusema chochote mpaka niione taarifa ya Nape aliyotoa kwa vyombo vya habari,” alisema.

Lakini alipoulizwa zaidi, Jaji Warioba alisema: “Kijana hivi hunielewi? Sisemi chochote mpaka nitakapoiona ‘statement’ ya Nape.”

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles