27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Sitta azidi kubanwa

Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

NA WAANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, amezidi kuandamwa baada ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kumtaka kusitisha mara moja mchakato wa Katiba unaoendelea.

Kituo hicho, kimesema Bunge hilo linapaswa kusitishwa hadi muafaka utakapofikiwa kati ya makundi mawili yanayosigana.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa  LHRC, Dk. Helen Kijo Bisimba, alisema kituo kimepata mshituko mkubwa wa kauli za viongozi wa Serikali pamoja na baadhi ya wajumbe wa Bunge  hilo kuhusu mchakato wa Katiba.

Alisema baadhi ya kauli hizo na matamko vinaashiria mwelekeo mbaya na ukiukwaji wa misingi ya demokrasia na utawala bora, kubana vyombo vya habari na haki za kutoa maoni.

Dk. Bisimba alisema kwa kiasi kikubwa matamko hayo yanakiuka haki za binadamu kama zinavyolindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977 ibara ya 18 na 21(2).

“Kituo kinakemea na kusisitiza kuheshimiwa kwa kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, haya mabadiliko yanayofanywa katika kanuni kwa manufaa ya kikundi kimoja yatapelekea kupatikana kwa Katiba ya upande mmoja,” alisema Dk. Bisimba.

Aliyekuwa Mkurugezi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Ananilea Nkya, amekemea vikali itikadi za kivyama zinazoonyeshwa na viongozi wa Bunge, akiwemo Sitta.

“Kiongozi huyu ameonyesha udhaifu wa hali ya juu, anafaa kuwa kiongozi wa nyumba kumi kumi,” alisema Nkya.

WAJUMBE UKAWA

Habari kutoka mkoani Dodoma, zinasema  wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wameendelea kufika mjini Dodoma.

Jana Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema) Said Arfi, alifika kwenye viwanja vya Bunge saa 4 asubuhi na kujiandikisha kwenye orodha ya wajumbe wanaohudhuria vikao hivyo.

Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Hamisi  alitaja wajumbe watatu wa Bunge hilo ambao wanatoka Ukawa na kuwa kwa sasa wamesharudi bungeni na wanahudhuria vikao.

Mwenyeti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema kuwa kwa sasa vikao vya kamati vinaendelea na kuwa kadiri muda unavyozidi kwenda, Ukawa watarejea bungeni kujadili masuala ya wananchi.

Kauli hiyo ya Sitta ilitokana na swali aliloulizwa juu ya kuanza kurejea kwa baadhi ya wajumbe wa Ukawa.

Swali: Kuna baadhi ya wajumbe wa Ukawa wamejitokeza, unazungumziaje hatua hiyo?

Jibu: wataongezeka tu nafahamu, hoja inakuwa vipi, umekaa kwenye jimbo lako, yanazungumzwa mambo huku kwenye Bunge Maalumu masuala yanayohusu wafugaji, wewe unatoka wilaya ya wafugaji, unasema mimi niligomea muundo kwa hiyo, hata wafugaji siwatetei, nani atakuelewa?

Mtaona, tutakapoanza Septemba 2, mwaka huu mambo ya wananchi yanaguswa, unazungumzia ardhi, haki za binadamu na kadhalika, huyo anayegoma kwa sababu tu muundo anaoutaka yeye haujamridhisha basi ni ajabu, sura 17 hazihusu muundo peke yake, ili ndilo tumezidi kusisitiza wakati wote.

Huku kuna mambo yanahusu wananchi wote, vijana, wajasiriamali, watu wanaoishi vijijini, masuala ya kuondoa rushwa, kuwa na Katiba ambayo itatuwekea vyombo huru zaidi vya uchaguzi, haya yote ni mambo ambayo mtu anaweza kuyazungumza kwa halali kabisa, bila kuonekana kama amevunja kitu chochote, lakini tusubiri.

Swali: Mazungumzo na Ukawa yanaendelea?

Jibu: Sina habari kwa sababu sisi walitugomea kabisa, hawati kabisa kuongea na mimi wala na kamati yoyote niliyonayo.

Kwa hiyo, nasubiri kama kuna vyama ambavyo vinaongea sijui, manake hata huko pia walikataa.

Lakini kikubwa ni kwamba sisi tulioko hapa, ndani ya sheria, tunaifuata sheria na katiba ilivyo, na bado mimi nasema utamaduni wa kususia mambo badala ya kujenga hoja hausaidii nchi, unazidi kutugawa tu.

Arfi

Kwa upande wake, Arfi baada ya kujiorodhesha kwenye wajumbe watakaoshiriki Bunge hilo, alisema ameamua kufanya hivyo kwa sababu yeye atakuwa ndani ya Bunge hadi Katiba itakapopatikana.

Alisema yeye ni mwana Chadema na siyo msaliti kwa wenzake, ila kwenye masuala ya Katiba vyama vinawekwa pembeni.

Swali: Ukawa walisema wanachama wao wasije, wewe umekuja. Je,  umekuwa msaliti?

Jibu: Anayesema kuwa mimi ni msaliti, yeye kasema, lakini tukumbuke sisi ndio tumetunga sheria, kama sheria ilikuwa mbovu basi tubebe lawama sisi kama wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati tunatunga sheria na kusema wajumbe wa Baraza la Katiba watakuwa ni wajumbe wote wa Bunge la Jamhuri, Baraza la Wawakilishi na hilo kundi maalumu ambalo Rais kaliteua ndio wanaofanya wajumbe wa hilo Bunge Maalumu… tulikuwa hatujui kwamba wabunge wa Jamhuri wengi ni wa CCM?

Tulikuwa hatujui wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wengi ni CCM?  Haya tulikuwa hatuyajui? Lakini sisi tulitunga sheria, kama ile sheria ilikuwa mbovu, ni sisi wa kubeba lawama.

Lakini tumetunga sheria tukijua kabisa wengi watakuwa ni CCM na kanuni inasema wachache wasikilizwe wengi waamue, sasa tupeleke hoja ndani ya Bunge tukazishindanishe ndani ya Bunge, siyo kutoka, hayo ndiyo mawazo yangu mimi.

Swali: Wenzako wamesua Bunge wewe mbona umerudi?

Jibu: Mimi ni mwana Chadema, lakini tunapoingia kwenye Bunge la Katiba vyama vyetu tunaviweka pembeni, tunaangalia masilahi mapana ya nchi yetu.

Swali: Viongozi wa Ukawa ambao wajumbe wake ni wabunge wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi wamezuia wabunge wao wasishiriki Bunge hili hadi maridhiano kati yao na CCM yafikiwe, lakini wewe umerudi, huoni kwamba umewasaliti wenzako?

Jibu: Unayapataje maridhiano? Kwa sababu ukisoma tamko la chama changu, ni kwamba mpaka tupate ufafanuzi wa kifungu namba 25 cha sheria ya mabadiliko ya Katiba.

Unapataje Ikulu? Huo ufafanuzi unaupata kwa nani? Ni lazima mrudi mahala ambapo mliitengeza ile sheria, na sisi ni sehemu ya kutengeza sheria mbovu. Tumetengeza sheria mbovu na sasa tunalalamika tunataka ufafanuzi wa kifungu namba 25. Kwanini tusihoji wakati tunatengeza sheria, ni akili tu ya kawaida.

Swali: Msimamo wako ni serikali tatu au mbili?

Jibu: Mimi ni serikali tatu.

Swali: Wewe umeamua kurudi bungeni na sasa mnajadili sura zote zilizobaki huku ikiwa hamjui ni mfumo gani wa serikali mtakuwa nao, hivyo vifungu mtaviweka vipi wakati haijulikani vitafanya kazi chini ya Serikali ya mfumo gani?

Jibu: Tutaona kadiri tunavyoendelea kwenda, lakini ni kwamba sisi tumeshashiriki katika hatua ya kwanza, kama chama, kama wabunge wa Ukawa, tumeshiriki katika sura ya kwanza na ya sita na tumetoa mawazo bungeni pale.

Tumetoa mawazo ya wengi na wachache, na mawazo yetu kama wachache yamesikilizwa, lakini leo tumeshatoa mawazo alafu tunarudi nyuma tunatoka, usiwe muoga, pambana.

Katibu wa Bunge

Katibu wa Bunge, Yahya Hamisi, alitaja majina ya wajumbe wengine watatu ambao wanatoka Ukawa.

Aliwataja kuwa ni Ally Omar Juma, Fatma Mohamed na Jamila Abeid wote kutoka kundi la vyama vya siasa Zanzibar.

Alisema wajumbe wengine wa Ukawa waliorudi bungeni ni Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda na Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere, wote kutoka Chadema.

Mjumbe mwingine ambaye alitajwa na katibu huyo ni Mbunge wa Viti Maalumu, Clara Mwaituka (CUF).

Alisema wajumbe hao watatu kutoka Zanzibar, walikuwapo kuanzia mkutano wa kwanza wa Bunge na wanashiriki katika kamati namba 11 inayoongozwa na Mwenyekiti, Anne Kilango.

“Kwa upande wa Shibuda, Mwaituka na Nyerere, tulivyofuatilia katika daftari la mahudhurio hawapo na hawajachukua posho kutokana na mkanganyiko uliotokea uhasibu ambapo walivyojua Ukawa hawatakuja,  hawakuwapa fedha, lakini tumetoa maelekezo kila anayesajili apewe fedha zake.

Kwa wale waliohudhuria kwenye kamati walilipwa posho zao kama kawaida na wanaendelea na vikao vya kamati,” alisema.

Akizungumzia kuhusu wajumbe wa Ukawa waliogoma kurejea bungeni hadi sasa, alisema kugoma kwao kunawapa wakati mgumu wananchi na akawataka kurejea kwani milango iko wazi.

Alisema wananchi hawawaelewi ni kwanini wanagoma wakati bado kuna mambo mengi ya kujadili ukiachilia mbali muundo wa Serikali.

“Walichokikosa ni Serikali tatu, kwa hali ilivyo jambo hilo haliwezekani, sasa hilo kama hawajalipata kama viongozi haiwezekani kupigania vingine?” alihoji.

Makamu Mwenyeki wa Bunge hilo, Samia Suluhu Hassan, alisema kuna wajumbe wengi wa ukawa wanaudhuria vikao vya kamati mbalimbali.

“Waliotoka wengi wapo kwenye kamati, na walio nje wanatamani kurudi, natumaini watarejea tu,” alisema.

Samia ambaye hakutaja idadi wala majina ya wajumbe hao, alisema pia kuwa akidi imetimia hivyo vikao kila kamati vinaendela bila shida.

Taarifa hii imeandaliwa na Fredy Azzah na Esther Mbusi (Dodoma) na Michael Sarungi (Dar).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles